Uelewa matibabu ya figo umeongezeka

Muktasari:

Kwa mafanikio hayo, Hospitali ya Benjamin Mkapa inakuwa ya kwanza nchini kufanya matibabu ya kupandikiza figo kwa mgonjwa kwa kutumia madaktari wazawa jambo ambalo halijafanywa na hospitali nyingine yoyote nchini.

Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) iliyopo Dodoma imetimiza miaka mitano tangu ilipoanza kutoa huduma zake.

Hospitali hiyo ya kanda inajivunia kuwa kitovu cha matibabu ya figo nchini kwa kuwa ndani ya miaka mitano imeshafanya upandikizaji wa figo kwa wagonjwa 13.

Na katika wagonjwa hao waliopandikizwa figo wapo wagonjwa wawili ambao wamepandikizwa figo kwa kutumia madaktari wazawa bila usaidizi wa madaktari kutoka nchi za nje. Hospitali hiyo ilifanikisha upandikizaji wa figo kwa wagonjwa 11 kwa kushirikiana na wataalamu wa matibabu ya figo kutoka Japan.

Kwa mafanikio hayo, Hospitali ya Benjamin Mkapa inakuwa ya kwanza nchini kufanya matibabu ya kupandikiza figo kwa mgonjwa kwa kutumia madaktari wazawa jambo ambalo halijafanywa na hospitali nyingine yoyote nchini.

Akizungumzia matibabu ya figo hospitalini hapo, Ofisa Muuguzi na Mratibu wa shughuli za upandikizaji figo hospitalini hapo, Devotha Mputi anasema kazi hiyo halikuwa rahisi kufanyika.

Anasema wakati wanafanya upandikizaji wa figo kwa mgonjwa wa kwanza mwaka 2018 haikuwa rahisi kwa kuwa ni kitu walichokuwa hawajawahi kukifanya hata mara moja. Anasema kwa kushirikiana na watalaamu wa ndani na Japan, walipandikiza figo kwa mgonjwa huyo Machi 2018 ambaye mpaka sasa anaendelea vizuri.

Upandikizaji huo wa kwanza uliofanyika Machi 23, 2018 kwa mgonjwa Elias Sweti baada ya kuchangiwa figo na dada yake Neema Sweti na hadi sasa taarifa zinasema anaendelea vizuri.

Elias ambaye ni mkazi wa Mvumi mkoani Dodoma wakati akipandikizwa figo alikuwa na umri wa miaka 52 kwa gharama ya Sh24 milioni. Gharama za kupandikiza figo kwa nchi kama India ni Sh77 milioni.

Wakati Elias akipandikizwa figo hospitali hiyo iliunda kamati ya watu 63 wakiwamo wataalamu wa afya, madaktari bingwa wa ndani na nje na viongozi wa dini.

Japo sio wote walioingia kwenye chumba cha upasuaji, lakini walikuwa wakifanya kazi ya ushauri na kwa viongozi wa dini kumuomba Mungu upandikizaji uende salama.

Mputi anasema upandikizaji huo ulifungua milango kwa watu wengine kwa kuwa tangu mwaka huo hadi sasa wamefanikiwa kupandikiza figo kwa wagonjwa 13 wanaoendelea vizuri na afya zao.

Anasema kati ya hao ni mgonjwa mmoja tu ambaye alifanyiwa upandikizaji wa figo Januari mwaka huu kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Japan, alifariki kwa ugonjwa wa shambulio la moyo.

Mputi anasema mgonjwa huyo alikuwa anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa upandikizaji wa figo, lakini alipofika Mei mwaka huu alipata ugonjwa wa shambulio la moyo na alifariki dunia njiani wakati akikimbizwa hospitalini.

“Lakini wagonjwa wengine wote wanaendelea vizuri kwa kuwa tunawafuatilia kwa ukaribu mno, ili kujua maendeleo yao, kwa wale ambao wapo karibu huwa tunawatembelea hadi majumbani kwao,” aansema Mputi.

“Lakini wengine wote wanaendelea vizuri na wanahudhuria kliniki kila mwezi, na wanatumia dawa pamoja na kufuata masharti; hali zao zipo vizuri tofauti na ilivyokuwa mwanzo.”

Mputi anasema pamoja na matibabu ya kupandikiza figo, wanatoa huduma ya kusafisha damu (dialysis) kwa kuwa mgonjwa hutakiwa kusafisha damu mara tatu kwa wiki ili kuimarisha afya yake.

Mputi anasema wagonjwa wanaosafisha damu kwenye hospitali hiyo ni wale ambao hawajafikia hatua ya kupandikizwa figo. Anasema baada ya kazi ya kusafisha damu kushindikana ndipo mgonjwa huanza mchakato wa kupandikizwa figo; hiyo sasa ni hatua ya tano ya matibabu.


Matibabu ya figo

Mputi anasema kuna hatua ambazo mgonjwa akiwa nazo anaweza kutibiwa ugonjwa wa figo na kupona bila kufanyiwa upandikizaji wa figo nyingine.

Anasema wagonjwa wengi hufika hospitalini wakiwa wamechelewa hivyo inakuwa vigumu kuwapatia matibabu ya kutibu figo hizo bila kuwapandikizia figo nyingine.

Mputi anasema lakini matibabu hasa ya mgonjwa wa figo ni kupandikizwa figo ya mtu mwingine ambaye hana matatizo ya figo baada tiba ya kusafisha damu kushindikana.

Mputi anasema zipo sababu nyingi za ugonjwa wa figo lakini sababu kubwa ni kisukari na shinikizo la damu au vyote viwili kwa pamoja.

Anasema kila mtu anayepimwa na kukutwa na ugonjwa wa figo anakuwa na historia ya kuwa na ugonjwa wa kisukari au shinikizo la damu.


Nani anaweza kuumwa ugonjwa wa figo

Mputi anasema mtu yeyote anaweza kuumwa ugonjwa figo kwa kuwa hauchagui mtoto, kijana wala mzee.

Anasema kwenye kitengo chao kuna wagonjwa wa kila rika ambao hupata matibabu kuanzia watoto, vijana hadi watu wazima.

“Tena tuna watoto wadogo wameshavuka hatua ya kusafisha damu sasa wanatakiwa kupandikizwa figo, si hao tu tuna vijana na hata wazee hivyo hatuwezi kusema kuwa kuna rika fulani ambalo ndiyo limeathirika zaidi,” anasema.

Changamoto

Mputi anasema bado kuna changamoto nyingi katika kuwapatia watu matibabu ya kupandikiza figo kwani watu wengi wana elimu ya mitaani kuwa wakitolewa figo moja wanaweza kufa au kuna kilema.

Anasema kutokana na hilo wanalazimika kutoa elimu ya ugonjwa wa figo kwa ndugu jamaa, marafiki pamoja na majirani ili kuwatoa elimu potofu waliyonayo kwenye akili zao kutoka mitaani.

Anasema mpaka sasa mtu anayetakiwa kupandikizwa figo anatakiwa kuipata kutoka kwa ndugu yake wa karibu kabisa na kama hatapatikana ndipo anaweza kwenda kwa mama mdogo, baba mdogo, wajomba na mashangazi.

Anasema lakini pamoja na hayo bado kuna changamoto kadhaa ikiwamo hofu kwa mtu anayetakiwa kutoa figo kwa mwingine hivyo kusababisha wengine kukosa wa kuwasaidia.

Anasema mpaka sasa kuna zaidi ya watu 40 ambao wapo kwenye hatua mbalimbali za kupandikizwa figo hospitalini hapo.

Hali ikoje?

Mputi anasema wakati wanaanza matibabu ya figo hospitalini hapo mwaka 2018 idadi ya wagonjwa ilikuwa ni ndogo kwa kuwa kwa siku mbili za kliniki walikuwa wanapata wagonjwa kati ya saba na nane.

Anasema lakini kwa sasa idadi hiyo ya wagonjwa imeongezeka hadi kufikia watu kati ya 25 hadi 30 kwa siku za kliniki kila wiki.

Mputi anasema ongezeko hilo sio kwamba wagonjwa wameongezeka bali ni uelewa wa watu umeongezeka wa kwenda kupata matibabu hospitalini tofauti na zamani.

Anasema watu wote wanaokutwa na matatizo ya figo wamekuwa wakufuatilia matibabu yao kwa umakini mkubwa na hakuna hata mmoja anayeachia njiani.

Mputi anasema pamoja na hayo, gharama za matibabu ya figo zimekuwa zikiwashinda watu wengi hivyo wanapotajiwa wakiondoka kwenda kutafuta pesa hawarudi kwa wakati na hata wakirudi hali inakuwa ni mbaya sana.

Anasema wengi wanafuata masharti ya matibabu kama kuhudhuria kliniki kila wanapohitajika pamoja a kutumia dawa kwa usahihi.

Mgonjwa azungumza

Mmoja wa wagonjwa wanaopata huduma ya kusafisha damu katika hospitali hiyo, Mathew Kalema (71) mkazi wa Mkoa wa Kagera anasema huduma katika hospitali hiyo ni nzuri kuliko hospitali nyingine hapa nchini

Kalema anasema huu ni mwaka wa pili anapata matibabu ya kusafisha figo zake; na mwaka mmoja wa kwanza alikuwa anapata Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Anasema wakati akiendelea na matibabu alisikia Hospitali ya Benjamin Mkapa inatoa huduma ya kusafisha damu, ndipo alipohamia hapo na anaendelea kupata matibabu kwa mwaka mmoja sasa.

Kalema anasema tangu ameanza matibabu amepata nafuu kubwa kwa kuwa vifaa vilivyopo ni vya kisasa na wataalamu wa kutosha

.“Nililazwa ICU (chumba cha uangalizi maalumu) mara tatu kutokana na tatizo la figo lakini baada ya kuanza kusafisha damu, afya yangu imeimarika naweza hata kufanya shughuli zingine,” alisema .