MAKALA YA MALOTO: Bunge halijui alipo Lissu, lakini mahakama inajua

Muktasari:

  • Ndugai akijibu mwongozo huo alisema: “Mbunge hayupo jimboni kwake. Hayupo hapa bungeni tunapofanyia kazi. Hayupo hospitalini. Hayupo Tanzania. Na taarifa zake Spika hana kabisa. Wala hajishughulishi kumwandikia Spika nipo mahali fulani au nafanya hivi.”

Februari 25, mwaka huu Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu ilikataa ombi la Wakili wa Serikali, Simon Wankyo, la kutaka Tundu Lissu, mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) afutiwe dhamana na itoe hati ya kumkamata.

Hakimu Thomas Simba alikataa ombi hilo kwa maelezo kuwa hakuna mtu asiyejua matatizo ya Lissu. Akafafanua kwamba kumfutia dhamana ingekuwa sawa na kukosa ubinadamu.

Siku 16 baadaye, yaani Machi 13, Lissu alitoa waraka kueleza kwamba Bunge limesitisha mshahara wake kuanzia Januari. Kwa kifupi, hajapata mshahara kwa miezi miwili sasa.

Hii ni baada ya tukio la Februari 7 la mbunge wa Geita (CCM), Joseph Msukuma kuomba mwongozo wenye sura ya kumshauri Spika wa Bunge, Job Ndugai kusitisha mshahara Lissu akisema anatambuliwa ni mgonjwa wakati si mgonjwa.

Ndugai akijibu mwongozo huo alisema: “Mbunge hayupo jimboni kwake. Hayupo hapa bungeni tunapofanyia kazi. Hayupo hospitalini. Hayupo Tanzania. Na taarifa zake Spika hana kabisa. Wala hajishughulishi kumwandikia Spika nipo mahali fulani au nafanya hivi.”

Akaongeza, “na kama ni mgonjwa hakuna taarifa yoyote ya daktari. Halafu unaendelea kumlipa malipo mbalimbali. Nadhani hoja yako ina msingi kwamba ipo haja ya kusimamisha malipo ya aina yoyote ile mpaka hapo tutakapopata taarifa rasmi.”

Kwa maelezo ya Lissu mshahara umekatwa tangu Januari. Mwongozo wa Msukuma uliokubaliwa na Spika ulikuwa Februari 7. Kwa maana hiyo kama uamuzi uliendana na mwongozo husika, Lissu angeanza kukosa mshahara Februari.

Ndio maana Lissu katika waraka wake anasema mwongozo ulikuwa kiini macho, kwani uamuzi ulikuwa umeshachukuliwa.

Suala kwamba Lissu alipigwa risasi Septemba 7, 2017, halina ubishi. Lilikuwa tukio lililoifanya nchi izizime. Vyombo vya habari viliripoti. Rais John Magufuli, aliandika ujumbe wa Twitter kulaani kitendo hicho. Spika alilitangazia Bunge na wabunge walimchangia Lissu.

Taarifa ilitolewa pia kwamba baada ya kupigwa risasi, alikiwahishwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, ambako jopo la madaktari lililompatia huduma za awali liliongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya (sasa balozi). Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na Spika mwenyewe walikuwapo hospitalini Dodoma.

Hata mgogoro kuhusu Bunge kugharamia matibabu ya Lissu, unajenga mantiki kwamba suala la Lissu kupigwa risasi na kuumwa halibishaniwi. Lissu alitibiwa Dodoma kisha akasafirishwa Nairobi, Kenya na baadaye Brussels, Ubelgiji anakoendelea na matibabu.

Mapema Februari, akihojiwa sauti ya America (VOA), Lissu alisema matibabu yake yanaendelea na Februari 20 angefanyiwa upasuaji wa 23. Na alipozungumza na BBC, aliahidi kurudi siku madaktari wakimwambia amepona asilimia 100.

Hivyo basi uamuzi wa Bunge kumsitishia mshahara mbunge ambaye alishambuliwa risasi katika mazingira ya Bunge, unaweza kuleta maswali; Hivi kweli Bunge halijui kama mbunge wake ni mgonjwa na anaendelea na matibabu Ubelgiji? Mbona Mahakama inajua na imegoma kumfutia dhamana?

Usahihi wa adhabu

Katika falsafa ya uhalali wa adhabu kuna nadharia ya haki ya uwiano wa kosa na adhabu. Kwamba adhabu inapotolewa, inapaswa kuonekana kweli inafanana na kosa.

Tubaki kwenye msimamo wa Spika kuwa Lissu hayupo bungeni, jimboni, hospitalini na hayupo nchini kabisa tujiulize, je, adhabu inayomstahili mtoro wa bungeni kwa muda mrefu ni kunyima mshahara?

Swali hilo linatuleta kwenye majibu kwamba kuna kitu kinakimbiwa. Ni kama Bunge linatambua hali halisi ya Lissu, ila linataka taarifa ya kimaandishi kuhusu matatizo aliyoyapata.

Lissu hayupo bungeni tangu Septemba 8, 2017. Kanuni ya 117 ya Bunge, inasema mbunge ambaye hatahudhuria mikutano mitatu mfululizo bila ruhusa ya Spika atapoteza ubunge.

Kikanuni, Lisu alipaswa kupoteza ubunge tangu Bunge la Bajeti 2018.