Chadema Bukoba wanyemelea mitaa 36 ya CCM

Wednesday January 9 2019

 

By Phinias Bashaya, Mwananchi [email protected]

Bukoba. Chadema katika Manispaa ya Bukoba imeanza kupiga hesabu ya kukomboa mitaa 36 inayoshikiliwa na CCM katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye mwaka huu.

Akizungumza na Mwananchi baada ya kutetea nafasi ya Mwenyekiti wa chama hicho katika Manispaa ya Bukoba kwa awamu ya tatu mfululizo, Victor Sherejey amesema mikakati ijayo ni pamoja na kupata mafanikio makubwa zaidi katika chaguzi zinazokuja.

Manispaa ya Bukoba ina jumla ya mitaa 66, kati yake chama hicho kilifanikiwa kunyakua mitaa 29 katika uchaguzi wa 2014, CUF mtaa mmoja na CCM mitaa 36.

Mwenyekiti huyo alisema ushindi wake wa asilimia 88 katika nafasi ya mwenyekiti, umechangiwa na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi kilichomalizika.

“Ukiangalia kila uchaguzi kura zangu zinapanda, vipaumbele ni pamoja na kuhakikisha tunapata mafanikio zaidi katika chaguzi zinazokuja,” alisema Sherejei.

Alisema pamoja na kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara watazidi kujiimarisha kupitia vikao vya ndani.

Wagombea wengine wa nafasi hiyo ya Mwenyekiti wa Wilaya walikuwa ni pamoja na Happiness Peter ambaye hakupata kura yoyote na Victor Herman aliyepata kuwa 21 wakati yeye, Sherejei, alipata kura 109.

Advertisement