Hivi hapa vikwazo vya elimu wilayani Momba

Tuesday December 11 2018

 

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Kwa mujibu wa takwimu za hali ya elimu zilizotolewa na Twaweza mwaka 2015 zinaonyesha kuwa ni asilimia 1.8 pekee ya wanafunzi katika Wilaya ya Momba ndiyo huanza shule wakiwa na umri wa kati ya miaka 5 hadi 6.

Wilaya hiyo ambayo kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya 2012 inatajwa kuwa na wakazi 182,641 kati yao asilimia 37 ni watoto walio kati ya miaka 0 hadi 9.

Licha ya kuwa wilaya hiyo ina watoto wengi lakini ni asilimia 1.8 ya watoto walio na kati ya umri wa miaka 5 hadi 6 ndiyo walioanza elimu ya awali.

Wakati hali ikiwa hivyo katika Wilaya ya Momba takwimu zinaonyesha kuwa Wilaya ya Kinondoni inaongoza kwa kuandikisha watoto wengi pindi wanapofikia tu umri wa kuanza shule.

Asilimia 71.6 ya watoto wote waliopo katika Wilaya ya Kinondoni wanapofikisha umri wa kati ya miaka 5 hadi 6 wanakuwa tayari wameandikishwa.

Licha ya kuwa watoto 322,004 wanaopatikana katika Wilaya ya Kinondoni ni mara nne ya wale 67,577 waliopo katika Wilaya ya Momba lakini mwamko wao katika suala la elimu bado limeonekana kuwa changamoto.

Changamoto gani wanapata watoto Momba?

Umbali wa shule zilipo ni changamoto kubwa ambayo wanafunzi, wazazi, walimu na viongozi wameeleza kuwa chanzo kikubwa cha watoto kuchelewa kuanza masomo kama ilivyo Kinondoni ambayo inaongoza

Mwendo wa zaidi ya saa moja na nusu kutoka kijiji kimoja kwenda kingine chenye shule ni jambo mtoto Selina Simkanga ambaye hulazimika kutembea umbali mrefu.

Moyoni mwake akiwa azma moja tu ya kutaka kuhakikisha kuwa ndoto yake ya kuwa mwalimu inakamilika.

Selina (11) anasoma darasa la tatu katika Shule ya Msingi Yala akitokea Kijiji cha Nsala safari yake ya kuelekea shuleni akilazimika kupanda mlima, kupita katikati ya msitu na kukatisha eneo la mto Momba kabla ya kufika shuleni.

Mbali na baadhi ya watoto wa Kitongoji cha Nsala kutembea umbali huo kuifuata shule pia watoto watokao katika Kitongoji cha Kanyala nao hulazimika kutembea mwendo wa zaidi ya dakika 40 kufika shuleni hapo.

Jambo hilo lilichangia kumfanya Selina na baadhi ya watoto wengine kutoka vijiji jirani wanaosoma shuleni hapo kuchelewa kuanza elimu yao ya awali katika umri unaotakiwa na badala yake kuanza darasa la kwanza wakiwa na umri wa miaka angalau kuanzia 8 hadi 9.

Mkazi wa wilaya hiyo Mustapha Thomas, anasema kama kungekuwa na uwezekano wa kuwajengea shule katika makazi yao ili kuwaepusha watoto na maeneo korofi ingekuwa ni suluhisho la malalamiko hayo.

“Lazima tufuate uongozi ili utusaidie licha ya kuwa watoto wanatakiwa kusoma lakini bado kuna mvutano kwa sababu huko ni mbali na mtoto mdogo hawezi,” anasema Thomas.

Lakini wakati wazazi wilayani Momba wakilalamikia umbali ambao watoto wao hutembea ili kufuata elimu, hali ni tofauti na Wilaya ya Kinondoni.

Licha ya kuwa baadhi ya wanafunzi pia hutumia muda mrefu kuzifikia shule wanazosoma lakini wengi wao hutumia usafiri wa daladala, pikipiki na hata bajaji ili kuwahi darasani tofauti na Momba wanaotembea kwa miguu.

Pamoja na kwamba muda mwingine wamekuwa wakikutana na vikwazo vya kunyanyapaliwa na baadhi ya makondakta wa daladala lakini imekuwa afadhali kwao.

“Nikichelewa sana huwa natumia dakika 15 hii ni kutokana na daladala kusimama katika vituo kuchukua abiria,” anasema Brian Paschal anayesoma Shule ya Msingi Mbezi na Mkazi wa Kimara Stopover.

Mbali na kuwa na umri wa miaka 11 Brian anasoma darasa la sita huku elimu yake ya awali aliinza akiwa na miaka 4 tofauli na Selina wa Momba mwenye miaka 11 akisoma darasa la tatu.

Brian pia anawakilisha kundi kubwa la watoto wa Wilaya ya Kinondoni wanaoanza shule pindi tu umri unapofikia.

Kinondoni inaongoza kwa asilimia 71.6 ya uandikishaji wa watoto walio na umri wa kati ya miaka 5 hadi 6 katika darasa la awali.

Jambo hilo linachangiwa kiasi na kuwepo kwa shule 90 za binafsi ambazo hivi sasa huandikisha hadi watoto walio na umri wa miaka mitatu tofauti na Momba ambako shule zote 75 ni za Serikali.

Changamoto ya uandikishaji Momba

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Yala, Amasha Mteka anasema shuguli ya uandikishaji watoto huanza kufanyika Septemba kila mwaka kwa kupita nyumba kwa nyumba.

Anasema licha ya kufanya hivyo baadhi ya wazazi wamekuwa hawatoi ushirikiano wa kutosha kwa kuficha umri sahihi wa watoto jambo ambalo linaleta ugumu kutambua ukweli.

“Mtoto anaweza kuwa na miaka mitano akakuambia mitatu, anaweza kuwa na miaka 6 akakuambia 4 inakuwa ngumu kwetu kujua ukweli kwa sababu hawana vyeti vya kuzaliwa na sisi ni wageni wa maeneo haya,” anasema Mteka.

“Licha ya kuwaandikisha pia, wazazi wamekuwa hawawaleti shuleni muda wa kuanza masomo unapofika hadi tuwatumie barua za vitisho. Wengi wanaanza kuja shuleni Machi hadi Aprili.”

Akizungumzia hali ilivyo Momba, mkurugenzi mtendaji wa wilaya hiyo, Adrian Jungu anasema ili kukabiliana na umbali wanaotembea wanafunzi hao wako mbioni kujenga zaidi ya shule shikizi 12 katika maeneo yenye sifa za kuwa na shule.

“Kwa sababu katika wilaya yetu kuna mito ya muda na kudumu hivyo hii itakuwa ni njia sahihi ya kupata wanafunzi wengi katika umri unaotakiwa,” anasema Jungu.

Advertisement