Hivi inawezekana kumlea mtoto hapa Tanzania bila viboko?

Sunday March 10 2019

 

Juma hili mwalimu Respicius Mtazangira wa Shule ya Msingi Kibeta iliyoko Manispaa ya Bukoba amehukumiwa kunyongwa baada ya kumpiga viboko vilivyopelekea kifo cha mwanafunzi wake. Tumefuatilia mijadala mbalimbali mtandaoni na kubaini kuwa wananchi wengi hawaamini kuwa mtoto wa Tanzania anaweza kulelewa pasi na viboko. Fuatilia sehemu ya majadiliano hayo hapa.

Ndugu Semkae Kilonzo anayetambulika mtandaoni kama @Semkae anaandika, ‘Sipendi kuona mwalimu au mtu yeyote kuhukumiwa kifo ila hii habari isaidie kurudisha mjadala wa kitaifa kuhusu adhabu ya viboko mashuleni. Ukisoma vitabu vichache vya saikolojia utagundua adhabu hii haifai kwa maendeleo ya afya ya akili ya watoto achilia mbali kuhatarisha maisha.’

Ndugu Lucy Shao @LucyLinus3 aliongeza kuwa wengi wanaochapa watoto, ni wale ambao hawana ukaribu na watoto hao. Au wale wanaopenda sifa za kuonekana wakali. Kwamba uchapaji wa viboko pia uwe na aina yake, sasa unakuta mtu anamchapa mtoto wa miaka sita na fimbo ya fagio ngumu, unampiga kama mwizi halafu bila kuangalia sehemu anazompiga mtoto, mara kichwani begani, nk.

@Asia_Masaba yeye anasema mama yake hakuwahi kuwachapa mara kwa mara kwani anakumbuka alimchapa mara moja tu, na hakuwa mtu wa kutumia kauli za karaha kwa wanae. Cha ajabu watoto wanamsikiliza mno mpaka leo. Anasema lakini baba yao ambaye alikuwa mtu wa fimbo walimpa shida kuliko mama yao aliyekuwa si mtu wa fimbo.

@meddy_88 yeye anajiuliza, watoto wanaosoma shule za serikali wanaochezea viboko kila siku, adhabu hizo zinawafanya kuwa na uwezo kwenye masomo kuliko wenzao wa shule binafsi (private schools) wasiochapwa shuleni? Swali lake linajibiwa na @Semkae kwamba (intelligence) – ujuzi wa mambo unazo nyuso nyingi. Upo ushahidi wa kisa cha mtoto ‘mkali’ wa hisabati kushindwa kujizuia kihisia na kumchoma kisu mwalimu wake. Hizi nyuso za uelewa zinafanya swali lako kuwa gumu. Wapo wa shule binafsi wamelelewa mazingira ya kikatili na wapo wa shule za serikali wamelelewa kaya zenye amani.

Mwalimu wa saikolojia Ndugu Christian Bwaya anayejulikana mtandaoni kama @bwaya yeye anasisitiza fimbo ni ishara ya kuishiwa mbinu. Tuboreshe mafunzo ya ualimu kwa kupitia upya namna somo la Saikolojia ya Elimu linavyofundishwa. Mwalimu akifunzwa kumfahamu mwanafunzi vizuri hatalazimika kumuumiza kumshinikiza amsikilize. @Semkae anakubaliana na @bwaya kwa kutoa mfano, ‘Mdogo wangu aliniambia kutumia viboko “ni njia rahisi” kwa wazazi. Njia ngumu ni kuelekezana na mtoto. Binamu yangu aliniambia zama za wazee wetu hawakuwa na nyenzo za kutosha za kisasa za malezi. Karne ya 21 hizo nyenzo na mbinu zipo za kutosha. Ukichapa ni uvivu wa kujifunza.’

Mwalimu @bwaya anasema Daniel Goleman anatukumbusha umuhimu wa kuwajenga walimu kihisia. Tusiwekeze kwenye ufahamu tu, tujenge mioyo yao pia. Mwalimu/mzazi mwenye Emotional Intelligence (uwezo wa kujali hisia za wengine na kudhibiti hisia zako) ana uwezo mkubwa wa kudhibiti hisia anaposhughulikia matatizo ya wanafunzi wake. Hakurupuki kutumia bakora.

@Semkae anaongeza kuwa si tu mwalimu, mtu yeyote. Uzuri wa ‘emotional intelligence’ unaweza kuijenga kwa kusaidiwa si kama uwezo wa kukimbia mbio. Cha kwanza uwe na ‘self-awareness’ yaani kujitambua. Ukiona mtu anakimbilia kumzabua mtoto kibao kwenye pantoni kisa “anasumbua” hapo mzazi ndiye ana matatizo!

Hapo likaja swali la mwalimu Mudhakiru Dauda, @mudhakiru_dauda: ‘Mzee waweza tusaidia kidogo njia mbadala kadhaa za kumuadhibu mwanafunzi mwenye utovu wa nidhamu?’@Semkae akajibu kwa kutoa mfano kuwa mwanae sasa miaka 9 kila akikosea anamweka kwenye kiti kwenye kona ya chumba. Hajawahi pata shida tena, hadi ajabu na anashangaa.

Ndugu Gaza @noorg6961 yeye anasema kumchapa mtoto ni kumjengea nidhamu ya hofu na kumuondolea kujiamini katika maisha yake – ni kumdumaza kiakili na sio kumfunza. Mjadala bado upo

Advertisement