Ijue namna bora ya makapi inavyoweza kunenepesha kuku

Tunaendelea kutembea katika ndoto za ufugaji na kumulika fursa zake. Tunaweza kufanya mambo mengi kibiashara kupitia ufugaji mbalimbali, lakini ufugaji wa kuku tumeupa kipaumbele kwenye ukurasa huu kutokana na kubeba ndoto za watu wengi. Zipo sababu nyingi zilizosababisha kujikita kwenye uchambuzi huu. Moja ya sababu za uchambuzi huu ni kuongeza uwezo wa wafugaji na kunufaika na miradi yao.

Ukiondoa dhamira hiyo zipo sababu muhimu za watu kupenda mazao ya kuku(nyama na mayai)kwa ubora na gharama nafuu kifedha. Hivyo basi dhana ya ufugaji wa kuku imebeba ndoto za wafugaji, walaji na wadau wengine.

Kuna usemi usemao ‘nyumba haijengwi kwa tofali moja’ makala hizi ni moja kati ya matofali yanayojenga uchumi kwa wafugaji na wadau wake kupitia maelekezo juu ya ufugaji bora. Tuungane sote kwani ufugaji ni kama biashara zingine ambazo hazikosi changamoto.

Kama ndiyo unajiunga na wasomaji wa makala hizi, napenda kukudokeza kuwa tumejifunza mambo mengi huko nyuma huu ni mwendelezo wake. Makala yaliyopita tulijifunza namna gani ya kuepukaulishaji wa vyakula vyenye sumu. Tuliona kwamba vyakula vilivyohifadhiwa muda mrefu hutengeneza fangasi ambayo ni sumu kwa mifugo na kuharibu mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na kusababisha maradhi au vifo kwa mifugo. Vilevile tuliona kuwa chakula hupoteza nguvu ya lishe kwa mnyama.

Mbali na hapo tulijifunza namna ya kutumia soya kama chakula mbadala kwa vyakula vya asili ya wanyama na samaki kama vile dagaa, uduvi na damu iliyokaushwa ambavyo mara nyingi hupatikana kwa bei kubwa. Soya isiyochakatwa au kutolewa mafuta sharti ikaangwe au kuchemshwa hadi ganda la nje liive. Bila kufanya hivyo, soya mbichi ina kiambata chenye kuzuia mmeng’enyo wa baadhi ya virutubishi tumboni na kusababisha madhara kwa mifugo.

Makala ya leo tuangalie faida na hasara za kutumia makapi ya mazao kama vile pumba za nafaka na mashudu ya mazao ya mafuta na mengineo kulisha kuku na mifugo mingine. Kama tunavyofahamu makapi ya mazao hupatikana baada ya kuondoa viini lishe vya zao husika. Kitendo hicho cha kukamua mafuta au kukoboa nafaka hubakiza kiasi kidogo sana cha virutubisho kwenye makapi hayo. Sehemu kubwa ya lishe huenda kwenye matumizi ya binadamu huku makapi yaliyobakiwa na lishe kidogo badala ya kutupwa hutumika kama chakula cha mifugo.

Zipo sababu nyingi za kutumia makapi haya kama chakula cha mifugo; kwanza makapi haya hupatikana kwa gharama nafuu, pili wanyama wengi huweza kuyameng’enya na kupata virutubishi kuliko binadamu anavyoweza. Sifa hizi mbili ndizo husababisha wafugaji watumie makapi kama chakula cha mifugo yao.

Kwa upande mwingine, zipo sababu za lazima kuangalia matumizi ya makapi ya vyakula vya binadamu kwa mifugo. Moja kati ya mambo ya kutizamwa ni baadhi ya mifugo kuwa na uwezo wa kujipatia virutubishi kwa wingikutoka kwenye makapi hayo na baadhi kushindwa kutokana na asili ya matumbo yao.

Kwa mfano; wanyama wanaokula majani (ng’ombe, mbuzi na wengineo) husifikia kuwa na tumbo lenye matumbo manne ambayo chakula humeng’enywa kwa kiwango cha juu kuliko nguruwe, kuku na wengineo ambao hutumia tumbo moja.

Kwa hiyo wanyama hawa wenye asili ya tumbo moja kitaalamu hawawezi kuwa na afya nzuri endapo watapewa malisho ya makapi bila kuongezewa vyakula halisi kwenye mchanganyiko wa lishe zao. Mifugo yenye asili ya tumbo moja hushindwa kusaga vizuri makapi hayo tumboni. Vilevile makapi hayo nguvu yake ya lishe huwa haimtoshi mnyama kukua na kuzalisha vizuri; upungufu wa kushambuliwa na magonjwa huwa mwingi. Afya ya mnyama huzorota, hamu ya kula na ulaji wenyewe mnyama hujilazimisha.Kiwango cha madini, protini, vitamin na wanga huwa chini sana hata kama mnyama atakula kiasi kikubwa cha malisho hayo bado atakumbwa na upungufu.

Kutokana na sababu hizo hapo; wanyama wasio cheua (kuku, nguruwe na wengineo) wapewe makapi kama vile pumba na mashudu kwa kipimo na kuongezwa lishe halisi ambayo itaongeza nguvu ya makapi kwenye mchanganyiko wa chakula ili kukidhi mahitaji ya mwili wa mnyama kukua na kuzalisha kwa wingi.

Lengo la kutumia makapi ya vyakula kulisha mifigo ni kupunguza gharama za ulishaji lakini kujikita kulisha makapi pekee ni kuongoza gharama kwani baadhi ya mifugo kama iliyotajwa ikiwamo kuku hudumaa na kushindwa kutaga na kushambuliwa na magonjwa mara kwa mara. Hivyo ni vizuri kufuata kanuni bora za ulishaji kwa manufaa zaidi.