Kasi bado ndogo ufugaji ng’ombe wa maziwa

Muktasari:

  • Licha ya kuwa na ng’ombe wengi, Tanzania ina ng’ombe milioni 1.1 pekee ambao wanazalisha maziwa. Ng’ombe hao wa maziwa wanazalisha lita bilioni 2.4 za maziwa kwa mwaka, kiasi ambacho kinaelezwa kuwa kiko chini.

Tanzania ni nchi yenye fursa kubwa ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa. Ni nchi ya pili baada ya Ethiopia kwa kuwa na ng’ombe wengi barani Afrika ambao wanafikia milioni 30.5 pamoja na mbuzi milioni 18.

Idadi hiyo ya ng’ombe pamoja na ukubwa wa ardhi ya Tanzania vinaongeza fursa kwa Taifa hili kukuza uchumi wake kupitia sekta ndogo ya maziwa pamoja na mazao mengine ya ng’ombe kama vile ngozi, nyama na kwato.

Licha ya kuwa na ng’ombe wengi, Tanzania ina ng’ombe milioni 1.1 pekee ambao wanazalisha maziwa. Ng’ombe hao wa maziwa wanazalisha lita bilioni 2.4 za maziwa kwa mwaka, kiasi ambacho kinaelezwa kuwa kiko chini.

Soko la maziwa ni kubwa hapa nchini kwa sababu kuna viwanda vya bidhaa za maziwa ambavyo vinaagiza maziwa kutoka nje ya nchi wakati Watanzania wenyewe wanaweza kulisha viwanda hivyo bila kuagiza nje.

Katika mkutano wa Jukwaa la Maziwa la Ulimwengu (GDP), Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina alisema Tanzania inatumia Sh30 bilioni kila mwaka kuagiza maziwa nje ya nchi, licha ya kwamba inashika nafasi ya pili kwa kuwa na mifugo wengi barani Afrika.

Soko la maziwa

Anasema Tanzania ina fursa kubwa ya kuzalisha maziwa kwa wingi kwa sababu ina uwezo na rasilimali za kutosha. Pia, anasema ina ardhi kubwa ambayo inaruhusu kuwa na maeneo ya kulishia mifugo.

“Uzalishaji wa maziwa Kenya ni lita bilioni 5.2, sisi hapa ni lita bilioni 2.4. Inakuwaje tunazidiwa na nchi ambayo haina ardhi ya kuweka mifugo yake? Ni matarajio yangu kwamba mtajadili kwa nini Tanzania iko nyuma na mje na mapendekezo,” anasema Mpina.

Anasema wafugaji wana fursa ya kuzalisha maziwa mengi kwa sababu soko lipo kuanzia utumiaji ngazi ya familia mpaka kwenye viwanda vya maziwa. Anasisitiza wafugaji kugeukia soko la maziwa kwa sababu bado Tanzania haijafanya vizuri.

Waziri huyo anasema Serikali imechukua hatua mbalimbali ili kuongeza uzalishaji wa maziwa nchini ikiwemo kuleta madume ya mbegu kutoka Afrika Kusini na New Zealand kwa ajili ya kusambaza mbegu hiyo kwa wafugaji.

“Tunahakikisha kwamba hakuna mifugo itakayoingizwa nchini kwa magendo, kwa sababu watu wanaleta mazao ambayo yameharibika au kwisha muda wake. Wakileta bidhaa zao zinakuwa na bei ya chini, kwa hiyo wazalishaji wa ndani hawawezi kushindana na afya za walaji zinakuwa shakani,” anasema Mpina.

Mpina anasema Serikali inahakikisha kwamba dawa za mifugo zinapatikana kwa wingi hapa nchini na mpaka sasa, tayari chanjo tano kati ya 11 za mifugo zinazalishwa hapa nchini wakati nyingine sita zikiagizwa nje ya nchi. Anasema mpango uliopo ni kuhakikisha kwamba chanjo zote zinazalishwa hapa nchini kuanzia mwakani.

Changamoto ya ufugaji

Baadhi ya wafugaji wa ng’ombe wa maziwa wanasema tatizo kubwa linalokwamisha ufugaji wa maziwa nchini ni kukosekana kwa mitaji. Wanaitaka Serikali na taasisi za fedha kutoa mikopo kwa wafugaji ili kuinua uwezo wao wa kufuga.

Mfugaji wa ng’ombe wa maziwa kutoka Bagamoyo, Ernest Mrisho anasema ili mfugaji apate maziwa mengi, lazima awe na mbegu nzuri ya ng’ombe wanaozalisha maziwa kwa wingi ndani ya muda mzupi tofauti na ng’ombe wa kienyeji.

Anasema ng’ombe wa aina hiyo wananunuliwa nje ya nchi na wanahitaji fedha za kutosha ili kuwekeza katika sekta hiyo. Anasisitiza kuwa uwekezaji mzuri unakuwa na matokeo mazuri kwa mfugaji.

Mfugaji mwingine, Omary Chambika anasema Watanzania wengi siyo wanywaji wa maziwa ndiyo maana soko la bidhaa hiyo liko chini ukilinganisha na nchi nyingine. Anasema wafugaji hawafugi ng’ombe wa maziwa kwa sababu hakuna masoko ya uhakika.

“Sisi wafugaji wadogo tunategemea tuuze maziwa yetu kwa mtu mmoja mmoja lakini hawanywi maziwa. Ukienda viwandani wanasema hawanunui kiasi kidogo na kwamba maziwa yetu hayatoshelezi kiwango,” anasema Chambika.

Kwa upande wake, Meneja mwandamizi idara ya kilimo katika Benki ya NMB, Carol Nyangaro anasema mwaka 2015, benki hiyo ilipitisha Sh50 bilioni, kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wakulima, ikiwa ni moja ya mikakati yake ya kuwasaidia kuboresha uzalishaji wao.

“Tunatambua kwamba suala la mitaji limekuwa tatizo kwa wakulima wengi ndiyo maana benki yetu ilijielekeza huko kwa kuanza kutoa mikopo. Sasa tunaona kuna fursa pia kwenye ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, tutaangalia mahitaji yakoje ili tuwawezeshe wafugaji,” anasema.