UCHAMBUZI: Kumbe wabunge wanaweza kunena lugha moja

Wednesday February 13 2019

 

By Alex Malanga

Si ajabu wabunge kugawanyika katika pande mbili huku wakitoana jasho kwa hoja pindi miswada ya sheria inapowasilishwa bungeni.

Lakini, hali ilikuwa tofauti Jumamosi ya Februari 10, 2019. Siku hiyo Bunge liliridhia kwa kauli moja kuyapandisha hadhi mapori ya akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika kuwa hifadhi ya Taifa, hivyo kufanya hifadhi za Taifa kuongezeka kutoka 16 na kufikia 21.

Sehemu ya 3 ya Sheria ya Hifadhi ya Taifa inampa Rais mamlaka ya kupandisha hadhi mapori ya akiba kuwa hifadhi za Taifa, endapo Bunge litaridhia.

“Ndiyooooooo” ilisikika sauti ya ‘wabunge wote’ bila kujali itikadi ya vyama vyao walipohojiwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai iwapo wanakubali mabadiliko hayo.

Pengine ni kutokana na unyeti wa suala husika hasa ukizingatia Serikali imejikita katika kuhakikisha inaongeza tija ya sekta ya utalii inayo changia zaiid ya asilimia 17 katika Pato la Taifa.

Swali ni je, tafsiri ya muswada huu kupita bila kupingwa kama ambavyo tumeona miswada mingine inapita baada ya kuwagawa wabunge?

Pengine hii inaashiria umuhimu wa mabadiliko hayo kwa Taifa na inaweza kusaidia kuepusha wabunge kunyosheana vidole baadaye mabadiliko hayo yatakapoonekana hayana tija kwa Taifa.

Wiki iliyopita akichangia muswada wa mabadiliko ya sheria mbalimbali Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alisema wabunge wanapaswa kuzungumza lugha moja wakati wa kujadili masuala yenye maslahi ya Taifa.

“Tunapaswa kuangalia maslahi mapana ya Taifa ili kuepusha mabadiliko ya sheria ya mara kwa mara,” alisema Mdee.

Lakini, licha ya kuridhia kupandisha hadhi mapori, wabunge wameingiwa na wasiwasi kuwa Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (Tanapa) itaelemewa na mzigo.

Alianza Spika wa Bunge, Job Ndugai akasema Tanapa inakabiliwa na mzigo mkubwa wa kodi, hivyo ikiongezewa hifadhi tano inaweza ikaathiri utendaji wake.

Tanapa wanatakiwa kisheria kulipa kodi ya kampuni asilimia 30, ichangie mfuko wa hazina asilimia 15 ya mapato yake ghafi, itenge asilimia sita kwa ajili ya tafiti na mafunzo na asilimia tatu kwa ajili ya tozo za kuendeleza utalii.

Ndugai akasema hana uhakika ikiwa Tanapa inapata msamaha wa kodi kwenye mashine zinazoagizwa nje kwa ajili ya kuboreshea miundombinu, kama walivyokubaliana na Serikali.

Wasiwasi mwingine ulielezwa na Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema) kuwa mapori hayo yatakuwa mzigo kwa Tanapa kwa kuwa kati ya hifadhi 16 zilizo za sasa ni tano tu zinazojiendesha kwa faida.

Hivyo, endapo Tanapa haitaongezewa fedha za uwekezaji, hifadhi chache zinazojiendesha kwa faida zitaongezewa mzigo zaidi na kuzifanya zihudumie nyingine 16 zinazopata hasara.

“Serikali inapaswa kumaliza jambo moja wanalolianzisha kabla ya kuanzisha lingine. Nina wasiwasi ule mpango wa kuvutia vivutio vya utalii vya kusini ‘SouthernCircuit’ utasahaulika.”

Lakini Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangalla anaweka mkazo akisema serikali haitarudi nyuma katika mpango wake wa kuwekeza kwenye vivutio vya kusini, vyovyote iwavyo umuhimu wa wabunge kunena lugha moja umeonekana.

Advertisement