Kutilia mkazo maumivu mbele ya goti kwa mwanamichezo

Monday June 11 2018Dk Shita Samwel

Dk Shita Samwel 

Patellofemoral Pain Syndrome kifupi PPS ni neno lakitabibu linalomaanisha maumivu katika eneo la mbele ya goti kuzunguka kifupa kidogo cha duara kijulikanacho kama Patela au Kneecap.

Tatizo hili linawakuta mara kwa mara wanamichezo wakimbiaji, waruka vihunzi, wapanda milima pamoja na washiriki wa michezo wa kila siku hasa wanawake na vijana wadogo.

Tatizo hili huambatana na mkazo na maumivu mbele ya goti hivyo kusababisha ugumu kupanda ngazi, kupiga magoti na kufanya kazi za kila siku.

Goti ndiyo ungio kubwa kuliko yote mwilini na limeumbwa kwa ufanisi wa hali ya juu.

Ungio hili lina mfupa wa paja, wa ugoko na wa nyuma ya ugoko na kifupa duara cha goti inayounganishwa na nyuzi za ligamenti na tendoni.

Tendoni huunganisha misuli kwenye mifupa, tendoni ya misuli minne ya mbele ya paja huunganisha sehemu ya mbele ya paja na kifupa duara cha goti (Patella)

Unapoonyoosha goti lako chini ya kifupa duara cha goti unaweza kugusa tendoni yake ambayo imeunganishwa na mfupa mkubwa wa ugoko.

Maumivu haya mbele ya goti yanatokea baada ya mishipa ya fahamu kupata msisimko wa hisia za maumivu katika tishu laini na mifupa inayoizunguka kifupa cha goti.

Chanzo cha tatizo hili ni kutumika kulikopitiliza kunakosababishwa na mazoezi magumu kama vile kukimbia sana, kuchuchuma na kupanda vilima au ngazi mara kwa mara. Vile vile mabadiliko na kuongezeka kwa ghafla kwa mazoezi au mafunzo ya mchezo.

Mambo mengine ni pamoja na kufanya mbinu mbaya za mafunzo ya michezo, kutumia vifaa visivyosahihi na kubadili viatu au eneo la kuchezea.

Udhaifu wa misuli ya mbele ya paja , wakati wa kupinda na kunyoosha goti tendoni ya misuli hiyo hushindwa kudhibiti kifupa cha goti katika pango lake hivyo kukaa vibaya.

Hitilafu ya mguu kutojipanga sawa sawa kati ya hipsi na kifundo cha mguu husababisha kifupa cha mguu kwenda uelekeo hasi.

Dalili ni pamoja na mkazo na maumivu mbele ya goti yanayoanza taratibu na kuongezeka unapofanya kazi, huweza kutokea kwa goti moja au yote mawili.

Kupata maumivu wakati wa mazoezi au shughuli za kila siku zinazokufanya kupinda goti kama kupanda ngazi na kukimbia.

Maumivu baada ya kukaa muda mrefu na kupinda goti ikiwamo kukaa ofisini au kusafiri katika magari, treni au ndege.

Maumivu yanayojitokeza pale unapobadili kasi na kiwango cha mazoezi, eneo la kuchezea au vifaa vya mazoezi.

Kusikia mlio wa mgongano katika goti unapopandisha ngazi au vilima.

Tatizo hilo linaweza kupona bila dawa kwa kufanya mabadiliko ya mazoezi yanayosababisha maumivu gotini, kutumia matibabu salama ya nyumbani au mazoezi tiba ya viungo.

Advertisement