Kwa nini timu Maalim Seif haikujiunga Chadema?

Mwanachama wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari.Kulia ni Zitto Kabwe na kushoto ni  Juma Haji Duni. Picha ya Maktaba.

Muktasari:

  • Nilikuwa na sababu za kusema hivyo lakini sikusema ili kuweka akiba, baada tu ya uamuzi ya Mahakama Kuu juu ya shauri lililohusu uhalali wa uenyekiti wa Ibrahim Lipumba, timu ya Maalim Seif ilijiunga ACT-Wazalendo.

Najua Watanzania wengi wamebaki na swali kubwa, kwa nini aliyekuwa Katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na wenzake hawakuhamia Chadema, chama ambacho kinaonekana kuwa na mtandao mkubwa Tanzania Bara kuliko vingine vya upinzani.

Kama ningelichambua ni wapi Maalim Seif na wenzake wanaenda kabla hawajaamua kwenda ACT, ningelijenga hoja zangu kuonyesha kuwa wangelienda ACT, NCCR-Mageuzi au hata vyama vingine vidogo na visivyo na mtandao mkubwa Bara.

Nilikuwa na sababu za kusema hivyo lakini sikusema ili kuweka akiba, baada tu ya uamuzi ya Mahakama Kuu juu ya shauri lililohusu uhalali wa uenyekiti wa Ibrahim Lipumba, timu ya Maalim Seif ilijiunga ACT-Wazalendo.

Kwa nini haikuwa Chadema

Kiuchambuzi, hakukuwa na uwezekano wa timu ya Maalim Seif (Bara na Zanzibar) kujiunga Chadema. Mtu ambaye angelidhani hilo linawezekana hana fikra kubwa za mienendo ya kisiasa. Na bado hata hii leo ikitokea ACT-Wazalendo inapata mgogoro na kufutika, na ikawapasa Zitto na Maalim Seif kuondoka kwenye chama hicho kwa pamoja, bado hawataenda Chadema, wataenda kwenye vyama vidogovidogo.

Kwanza, kuna kutoaminiana baina ya vyama na viongozi wa vyama vya upinzani nchini. Viongozi wa vyama vyenye nguvu vya upinzani hata kama wangelionekana hadharani, kwenye mikutano na kampeni, bado hawaaminiani. Na hata unapokaa nao unaona kutoaminiana katika macho yao, midomo, nyuso na nafsi zao.

Mambo yanayousumbua upinzani hayajatafutiwa suluhisho na hakuna dalili za kufanya hivyo ndani ya vyama vyenyewe. Vyama vimekuwa vikipambana zaidi na mashambulizi vinayopewa kutoka CCM bila kuchukua hatua za kutatua matatizo ndani ya vyama vyenyewe.

Vyama vyetu vinajiendesha kwa hofu kubwa za ndani, majaribio ya kupinduana kila kukicha, majaribio ya kuangushana na kutaka kudhibiti chama kila siku. Hali hii inaweza kuwa hatari ikiwa vyama vyenye nguvu vinaamua kuungana na kuwa chama kimoja.

Hofu ya kuporana madaraka

Hadi leo, mfumo wa vyama vyetu vya upinzani hapa Tanzania umejengwa juu ya watu wenye madaraka na siyo taasisi zenye madaraka. Madaraka ya vyama vyote vya upinzani yamo kwa watu na siyo kwa vyama.

Kinyume na haya, vyama vya upinzani vinajiendesha kwa sababu ya ufuasi wa viongozi kuliko vyama vyenyewe. Ndiyo maana baada ya Maalim Seif kuondoka CUF ameondoka na mtandao karibia wote wa chama hicho upande wa Zanzibar na sehemu ya mtandao wa Bara, Lipumba amebaki na mtandao mdogo sana.

Haya yanatokea kwa sababu hizo za vyama kujengwa juu ya watu binafsi kuliko taasisi zenyewe. Ndiyo maana Lipumba na Maalim Seif wamegawana watu.

Nguvu za viongozi

Freeman Mbowe akisema anaondoka Chadema, chama chake kinaweza kupata matatizo makubwa. Na wapo viongozi waandamizi wa Chadema wanaamini akiondoka chama hicho kitayumba. Kwa ACT-Wazalendo huko kuna shida zaidi, kama Zitto anaacha uongozi lazima kitakata roho moja kwa moja Bara nzima. Kitabakia Zanzibar kwa mtandao uliotoka CUF.

Maalim Seif na Zitto wakiondoka ACT na kujiunga NLD, ACT itakufa hapohapo na siasa zitahamia NLD kwani wao ndio wanaaminika kushikilia ajenda za kupigania jambo fulani badala ya vyama.

Vivyo hivyo kwa CUF iliyobaki na majengo na bendera, ikiwa Lipumba anaondoka na kujiunga chama kingine au anastaafu siasa, hata majengo na bendera ya CUF havitakuwepo.

Kwa sababu siasa za upinzani zinategemea zaidi viongozi kuliko taasisi zenyewe, viongozi wanapoondoka kwenye chama kimoja kwenda kingine, kule ugenini kunapaswa kuwa na nafasi ya kuwabeba na hali hiyo huwafanya baadhi ya wenyeji wapoteze nafasi zao kwa maumivu makali. Kwa hiyo ni rahisi kwa watu wenye mtandao mkubwa Zanzibar kama Maalim Seif kujiunga ACT kuliko kujiunga Chadema. Hii inaenda sambamba na falsafa ya mafahali wawili kutoweza kukaa zizi moja.

Lazima kubadilika

Vyama vinavyojengwa juu ya misingi ya viongozi na madaraka vitakuwa na shida kubwa ya kuaminika katika uongozi wa dola. Vyama vinavyojijenga juu ya migawanyiko na mikikimikiki ya kimadaraka ndani kwa ndani haviwezi kuziishi siasa za Afrika, huishia kuparaganyika na kutawanyika. Tukumbuke, Watanzania kwa maana ya wapiga kura ni watu wenye ajenda muhimu za maisha yao ya kila siku, wanataka kuona vyama vinashughulika na masuala yao, hasa maendeleo yao, kuliko minyukano ya madaraka na uongozi.

Wakati muungano wa Maalim Seif na Zitto na wafuasi wao unaweza kuwa urafiki wa mashaka kwa kiasi fulani, muungano wa Freeman Mbowe na Maalim Seif (ikiwa Maalim na wenzake wangelijiunga Chadema) ungelikuwa na mashaka makubwa zaidi ambayo yangeambatana na vita kubwa ya madaraka ya ndani.

Huenda CUF – Maalim Seif ikapata pumziko la muda kiasi ndani ya ACT, lakini hiyo itategemeana pia ikiwa Zitto ataaminika na kujiaminisha kiasi gani kwa Maalim Seif na wenzake, kwa kuzingatia kuwa siasa za Zitto zimekuwa zikiambatana na utata mwingi mno.

Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Mfuatiliaji wa Utendaji wa Serikali barani Afrika;Aliwahi kuwa Naibu katibu mkuu na Mwenyekiti wa Kamati ya uongozi CUF. Sasa ni kada wa CCM. Simu; +255787536759; [email protected]).