Majanga ya usafiri majini hadi kiama!

Katika miaka ya karibuni nchi yetu imekuwa ikikumbwa na majanga ya usafiri wa majini yaliyosababisha maafa makubwa.

Baada ya kila muda mfupi ni kawaida kutokea ajali ya meli, jahazi au boti iliyopakia zaidi ya uwezo wake kwa kuzama baharini au katika ziwa.

Kinachofuata ni zoezi la uokoaji, kuopoa maiti na kuzika (wengine kaburi moja) na maombolezi. Baadaye tunaambiwa juhudi zipo mbioni kudhibiti maafa ya aina hiyo yasitokee tena.

Nisingependa kuorodhesha maafa yaliyotokea kwa vile itakuwa kama kuchoma msumari wa moto kwenye kidonda.

Lakini, tukumbuke ukitaka kutibu kidonda ni lazima na ukisafishe na hapo hutokea maumivu na baada ya hapo ndio unaweka dawa. Hivi karibuni nilifurahi kuona Serikali ya Zanzibar ikifungua jengo maalumu la uokoaji na uzamiaji pembezoni mwa Bandari ya Mkoani, kisiwani Pemba.

Vilevile Serikali imenunua boti na vifaa vya kisasa vya uokoaji na tumeambiwa upo mpango wa kutumia ndege zisizokuwa na rubani kuimarisha ulinzi na usafiri salama baharini.

Hii ni hatua nzuri ya kujali na kulinda maisha ya wasafiri na mali zao katika bahari inayozunguka visiwa vya Unguja na Pemba.

Hata hivyo, nataka niweke wazi kwamba kuwa na vifaa na nyenzo za kisasa za uokoaji baharini hazitoshi. Lililo muhimu ni kuhakikisha vifaa vinatunzwa na wakati wote vipo katika hali nzuri ya kutoa huduma.

Vilevile pawepo na utaratibu mzuri wa matunzo. Uzoefu umetuonyesha kutokea ajali na kusikia boti haikuweza kutumika kuokoa watu kwa vile ilikuwa haina mafuta.

Jingine la kuzingatiwa ni kuhakikisha askari wenye uzoefu wa kuokoa maisha ya watu baharini wanakuwa kazini wakati wote na sio kuanza kutafutwa inapotokea ajali. Mara nyingi hushangaa nikisafiri kwa meli kati ya Unguja, Pemba na Dar es Salaam kuona hapana askari wenye vifaa vya kuokoa abiria gatini.

Hili ni hatari kwa vile katika harakati za kupanda au kuteremka melini upo uwezekano wa mtu kuteleza na kutumbukia majini.

Badala yake huwaona askari wanamaji wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) wakipekua mizigo ya wasafiri.

Kazi ya askari wanamaji ipo baharini na si kwenye meza ya kupekua mizigo ya abiria. Tuheshimu mgawanyo wa kazi kwa kila mtu kuelewa kazi aliyopangiwa kuifanya.

Siku moja nilishangaa kumuona askari wa kiume wa kikosi cha Usalama Barabarani anapekua mkoba wa mwanamke bandarini. Sikutarajia kumuona askari wa salama barabarani anapekua mizigo na hasa mwanamume kukagua begi la mwanamke. Sheria, mila na desturi hazikubali mwenendo huu.

Lakini, lililo muhimu zaidi ni wakati wote kuchukuliwa hatua za kuzuia ajali zisitokee.

Sielewi inakuaje meli au jahazi kuruhusiwa kuondoka bandarini kama si salama kufanya safari.

Hii ni kusema hakuna ukaguzi unaofanywa na kama unafanyika si wa uhakika au ujanja (rushwa) hutumika na kuhatarisha maisha ya abiria.

Vipi chombo kinachotarajiwa kupakia abiria 200 kitaondoka bandarini na watu zaidi ya 300 na shehena kubwa zaidi ya mizigo kuliko uwezo wake wa kubeba?

Hakuna asiyetambua hali ya bahari au ziwa hubadilika na gharama zake za kuipuuza ni kubwa.

Ni vizuri pakiwapo taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinazoeleza hali si nzuri safari za majini zisimamishwe.

Ni vizuri tukajifunza kwa yaliyotukuta siku za nyuma na kujikinga na maafa kama yaliyotokea na kupelekea mamia ya watu katika nyakati tafauti Bara na Visiwani kupoteza maisha.