Mashauriano ya wastaafu na Rais Magufuli yazae matunda

Sunday July 8 2018

Rais John Magufuli akizungumza na viongozi

Rais John Magufuli akizungumza na viongozi wakuu wastaafu wakiwemo, marais, makamu wa rais, mawaziri wakuu, maspika wa Bunge na majaji wakuu katika kikao kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam. Picha na Ikulu 

Hivi karibuni, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwakaribisha Ikulu wazee muhimu wa taifa hili, marais wastaafu, makamu wa rais wastaafu, mawaziri wakuu wastaafu, maspika wastaafu na majaji wakuu wastaafu.

Mkutano huo wa Rais Magufuli na wazee wastaafu ulikuwa ukilenga kujenga ukaribu wa viongozi wa nchi waliopo na waliomaliza muda wao wa kazi ili pande hizo mbili zijadili hali ya nchi na kutoa maoni yao kwa Rais. Yako masuala ambayo wataalamu wa mikutano ya namna hiyo wanaweza kuona umuhimu wake na ni muhimu tukayajadili.

Mpangilio wa ukaaji

Mpangilio wa ukaaji katika makaribisho na mkutano huo wa mashauriano kati ya wastaafu na Rais Magufuli ni jambo ambalo haliwezi kupita hivihivi. Kwa mtizamo wa dunia ya sasa, viongozi wachache kama 10 hadi 20 wanapokutana katika ukumbi wakiwa ni viongozi wastaafu na walioko madarakani ni muhimu kukawa na mpango wa ukaaji wa kirafiki ambao unajenga dhana kuwa watu walioko mahali hapo ni wakuu wa nchi wastaafu na mkuu wa nchi aliyeko madarakani.

Nadhani hakukuwa na haja ya kumuweka Rais, Waziri Mkuu na Katibu Mkuu Kiongozi mbele kisha viongozi wastaafu wakakaa kwenye viti kama vile wanapokea maelekezo.

Mpangilio huu wa ukaaji ambao kitaalamu unaweza kuitwa mfumo wa mwalimu na mwanafunzi, unaweza kutumiwa zaidi wakati wa vikao vya mkuu wa nchi na mawaziri wake au na watendaji wake au na watu wengine wa chini yake.

Dhana pana ya kimahusiano katika nchi ni kwamba, marais wastaafu wana hadhi ya ki-rais na wanastahili kupewa itifaki za urais hata kwenye ukaaji, hasa katika shughuli ambayo inawahusu wao na rais aliyeko madarakani peke yake.

Kwa hiyo, watendaji wa Ikulu walipaswa kuweka mpango wa ukaaji wa meza ya mduara wa jumla ambapo baadhi ya wakuu wa nchi kama Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi, wangeweza kukaa sambamba na Rais Magufuli; Waziri Mkuu Kassim Majaliwa angeliweza kukaa kwenye meza moja na mawaziri wakuu wenzake kina Cleopa Msuya, Edward Lowassa, Joseph Warioba, Frederick Sumaye, Mizengo Pinda, Dk Salim Ahmed Salim na John Malecela.

Jambo hili linaweza kuonekana ni dogo, lakini lina maana kubwa kwenye dunia ya majadiliano na mashauriano hasa kwa watu ambao wote au wanashikilia au wamewahi kushikilia wadhifa wa aina moja kwenye chumba kimoja.

Mfumo wa ukaaji wa mwalimu na mwanafunzi unajenga dhana kuwa kuna mmoja amekuja kumiliki mawazo na maoni ya wengine hasa yule aliyekaa mbele ya wenzake. Mara nyingine lazima Ikulu izingatie mfumo wa kisasa wa ukaaji wa viongozi wa aina hii.

Vyombo vya habari

Kumekuwa na kusuasua kwingi kwa kile kilichozungumzwa na viongozi wakuu wastaafu kwenye mashauriano hayo. Hakuna video yoyote ndefu kabisa inayoonesha mazungumzo yote kuanzia mwanzo hadi mwisho, naamini viongozi wakuu walikutana kwa nia njema sana, njia ya mashauriano – kile hakikuwa kikao cha maamuzi yoyote zaidi ya kuwashauri waliopo madarakani, ilikuwa ni jambo la busara kwamba vingealikwa vyombo vya habari vya kutosha kushuhudia mazungumzo hayo na hata kupewa nafasi ya kuuliza maswali mwishoni ili dhana na maono yaliyotolewa na pande zote mbili yafafanuliwe zaidi kimitizamo.

Kinachoonekana huku nje ni vipande vidogovidogo vya viongozi hao wakizungumza, jambo ambalo nadhani kwa dunia ya sasa halina maana sana.

Wananchi huku mitaani wanapenda sana kuona viongozi wakizungumza na wao wananchi wakishuhudia kile kinachozungumzwa. Tabia ya dola ya Tanzania kujaribu kudhibiti taarifa za mambo muhimu ambayo hayana athari zozote kwa wananchi, na kufanya mambo hayo kuwa ghali kuwafikia wananchi si tabia nzuri katika ujenzi wa taifa imara.

Mtu aliyezungumza kwa kirefu na mazungumzo yake ya dakika 13 kuweka hadharani ni Rais Magufuli pekee, nadhani alikuwa akitoa shukrani na kufafanua mambo mbalimbali – kama kweli mashauriano yalikuwa na nia njema na yakiwa ya pande zote mbili, ni muhimu sana maoni ya viongozi wastaafu yakawekwa wazi kwa urefu wake na kama yalivyotolewa, ili kuisaidia jamii kujua viongozi wake wanafikiria nini kuhusu mwenendo wetu.

Sheria

Masuala ya kisheria yalishauriwa vizuri sana japo kwa vipande vifupi vya video ambavyo vilitolewa. Jaji Samata aliontesha kuwa haridhishwi na mfumo wa usimamizi na uzingatiaji wa sheria hapa Tanzania. Japokuwa aliwataja wakuu wa mikoa na wilaya kama vinara wa kuvunja sheria zetu wenyewe, lakini kwenye uhalisia Jaji Barnabas Samatta alikuwa anakumbusha kuwapo viongozi wa Serikali ambao ni kinara wa kutoziheshimu sheria za nchi – Wito wa Jaji Samatta ndiyo hali halisi ya nchi.

Kile wanacholaumiwa kutenda wakuu wa wilaya na mikoa ndicho ambacho kimekuwa kikitendwa na watendaji wengine kuanzia juu hadi chini. Ni muhimu sana Rais akazingatia saa wasia huo. Nchi ambayo viongozi wake wanadharau sheria zake na wanazikanyaga, si nchi salama, maana hakuna ustawi wowote unaoweza kujengwa kwenye taifa ikiwa hakuna heshima kwa sheria, na hasa sheria zilizo za haki.

Amani tunda la haki

Mchango wa Jaji Ramadhani ulikuwa na maana kubwa na ya dhati. Amani haiwezi kuja kama hakuna haki. Jaji Ramadhani amesisitiza kwamba juhudi zote ambazo zinafanywa na serikali ya awamu ya tano ambazo zinaweza kuwa muhimu na nzuri, hazitakuwa na maana kama nchi haina haki.

Jaji Ramadhani anashikilia msimamo ambao unashikiliwa pia na wazalendo wengi nchini wa kutaka tujenge taifa la haki, msimamo ambao Mwalimu Nyerere aliuimba tangu tunatafuta uhuru.

Katika Afrika, viongozi wengi wamekuwa wakililia amani lakini wamekuwa hawawatendei haki wananchi wao, matokeo yake haki hutokomea kabisa.

Nidhamu

Suala la nidhamu lilizungumza vizuri na Mzee Mwinyi, msisitizo wake ulikuwa kwamba Rais Magufuli amerejesha nidhamu ya watendaji serikalini. Hata hivyo, msimamo huu haukuzingatia masuala mengine muhimu ya upande wa pili.

Pamoja na Serikali kusifiwa kwa kudhibiti nidhamu za wafanyakazi, lakini kuna malalamiko juu ya wajibu wa serikali kwa wafanyakazi hao. Mfano, kwa miaka ya 2016/17 na 2017/18, Serikali imeshindwa kuwalipa wafanyakazi wa Serikali ongezeko la mshahara ambalo lipo kisheria, ongezeko hili hupaswa kufanyika kila mwaka na lenyewe halijali ukuaji wa bajeti wala hali ya uchumi.

Huo ni mfano mmoja mkubwa ambao tunaweza kuutizama na kuujadili kwa kuwa nidhamu zinaambatana na wajibu wa Serikali kwa wafanyakazi.

Ukuu wa Serikali

Mzee Ali Hassan Mwinyi anaamini kuwa lazima serikali ijioneshe kuwa ipo kila wakati, mtizamo huu unajikita kwenye hoja ya ukuu wa serikali ambayo ni pana. Mzee Mwinyi anaamini chini ya utawala wa awamu ya tano serikali imechomoza makucha yake na kuonyesha ukuu wake.

Kila baada ya miaka mitano wananchi huchagua serikali na serikali hiyo ipo siku zote. Serikali hizi huja na kuondoka na kila mara na kila wakati zenyewe ndizo husimamia maamuzi ya kuwajenga au kuwaumiza wananchi.

Ni wazi kuwa ukuu wa serikali lazima uambatane na kuheshimu ukuu wa wananchi walioiweka madarakani. Kama ambayo Mzee Mwinyi angependa Serikali iogopwe na ijulikane kuwa ipo, ndivyo ambavyo Serikali nayo ilipaswa kuwaogopa wananchi na kujua kwamba wapo na wao ndiyo wana mamlaka makubwa zaidi kwenye nchi yao na kuamua aina za serikali wazitakazo.

Naamini mara nyingine viongozi wetu watakapoitwa kwenye mashauriano mengine ya namna hii watazingatia misingi hii, wao ni wastaafu na kila mara wanapaswa kuwa sauti ya wananchi.

Rais wa nchi anapowaiteni kwenye mashauriano ni muhimu kumshauri yale asiyoyaona au ambayo anayaona lakini huwa hayapi kipaumbele.

Katika mashauriano, unapotumia muda mwingi kumsifia kiongozi aliyekuita juu ya masuala ambayo watu wengi wamekuwa wakiyatizama kwa mtizamo tofauti, haumjengi kiongozi huyo.

Julius Mtatiro ni mchambuzi wa mfuatiliaji wa utendaji wa Serikali barani Afrika; ni mtafiti, mwanasheria, mwanaharakati na ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF. Simu; +255787536759 [email protected])

Advertisement