Matatizo yatokanayo na upungufu wa vichocheo vya homoni kijinsia

Muktasari:

Kutokana na kuongezeka kwa matangazo ya waganga wa jadi wanaotoa tiba ya kuongeza nguvu za kiume nchini, hii ni ishara kuwa kuna ongezeko kubwa la matatizo ya upungufu wa vichocheo vya jinsi katika jamii

Vichocheo vya jinsi ni homoni zinazohusiana na mabadiliko ya ukuzi wa wanaume na wanawake wanapofikia umri wa kuzaa.

Homoni hizi kwa wanaume huwezesha uzalishaji wa tezi zinazotengeneza mbegu za kiume na kwa wanawake mayai. Kuna aina mbalimbali za vichocheo vya jinsi kama vile testosterone, progesterone, estradiol, inhibin B, activin na homoni zijulikanazo kama antimullerian (AMH).

Wanaume

Kwa upande wa wanaume upungufu wa vichocheo vya jinsi unahusiana kwa kiasi kikubwa na upungufu wa homoni ya testerone. Na kwa wanawake tatizo hili hujitokeza zaidi pale homoni ya progesterone inapopungua mwilini.

Upungufu wa vichocheo vya jinsi ni tatizo linaloweza kuathiri vibaya hali ya ubora wa maisha, hasa kwa wanandoa. Mbali na matatizo ya kiafya, upungufu huu unaweza kusababisha kuvunjika kwa ndoa na kusambaratika kwa familia.

Ni muhimu pia kutambua kuwa tatizo hili pia kwa namna moja ama nyingine linaathiri kazi za ubongo, mishipa ya damu, afya ya moyo, afya ya mifupa na mchakato wa kikemikali unaosaidia mwili kuendeleza utendaji mzuri wa seli zake.

Wanaume wenye upungufu wa vichocheo ya jinsi wanaweza kupata matatizo ya kupungukiwa hamu ya tendo la ndoa, upungufu wa nguvu za kiume, kushindwa kutungisha mimba, kupungua kwa ukubwa wa misuli ya mwili na kupotea kwa tabia za kiume.

Matatizo mengine ni uchovu wa mwili, udhaifu wa mifupa na matiti kuwa makubwa. Mara nyingi chanzo cha tatizo hili kwa wanaume ni maradhi yanayoathiri korodani, sehemu ya ubongo ijulikanayo kama hypothalamus na tezi ya pituitary. Matibabu ya saratani na mionzi pia ni mambo mengine yanayosababisha tatizo hili.

Umri mkubwa nao unachagia kutokea kwa tatizo hili. Chama cha Wataalamu wa Vichocheo Mwilini cha Marekani (American Association of Clinical Endocrinologists) katika utafiti wake uliochapishwa mwaka 2001 katika jarida liitwalo Jornal of Clinical Endocrinology & Metabilism, toleo namba 86, kinadai kuwa wanaume wenye umri zaidi ya miaka 75 kufikia kiasi cha asilimia 30 wana upungufu wa vichocheo vya jinsi.

Mambo mengine yanayoweza kuchangia kutokea kwa tatizo hili ni pamoja na maradhi ya kuambukiza kama vile Kifua Kikuu (TB), Ukimwi na uambukizo wa virusi vinavyosababisha uvimbe wa tezi za mate (mumps). Unene wa kupindukia na matumizi holela ya dawa zenye homoni pia ni mambo mengine yanayochangia.

Wanawake

Kwa wanawake, upungufu wa vichocheo vya jinsi unaweza kusababisha hali ya mwili kuchoka mara kwa mara, upungufu wa hamu ya tendo la ndoa, msongo wa mawazo, wasiwasi, hali ya kushindwa kuzingatia mambo na kukosa usingizi. Matatizo mengine ni nywele kunyonyoka, udhaifu wa mifupa na kuvurugika kwa mtiririko wa siku za hedhi.

Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa watu wengi wanaokabiliwa na tatizo la upungufu wa vichocheo vya jinsi mwilini, chanzo ni kemikali zinazopatikana katika bidhaa za matumizi nyumbani kama vile shampoo, baadhi ya sabuni za unga, rangi za kucha, spray za nywele na vifungashio vya plastiki.

Utafiti huo unaonyesha kuwa, bidhaa zenye kemikali ya phthalates, ambayo inaongezwa katika vifungashio na bidhaa za plastiki ili kuongeza uangavu na uwezo wa kukunjika kwake zinachangia kwa kiasi fulani kutokea kwa tatizo hili.

“Tulipata ushahidi kuwa kupungua kwa kiasi cha homoni ya testosterone ndani ya damu kuna uhusiano na ongezeko la watu kugusana na kemikali ya phthalate, hali hii inahusisha wavulana wenye miaka sita hadi 12, na wanaume na wanawake wenye miaka 40 hadi 60,” anasema Dk John D. Meeker wa Chuo Kikuu cha Michigan, mmoja wa viongozi wa utafiti huo.

Kutokana na kuongezeka kwa matangazo ya waganga wa jadi wanaotibu tatizo la nguvu za kiume hapa nchini, hii ni ishara kuwa kuna ongezeko kubwa la matatizo ya upungufu wa vichocheo vya jinsi katika jamii.

Jamii inashauriwa kutafuta huduma za kitabibu zenye ushahidi wa kisayansi ili kukadiria tatizo hili. Ili kupunguza hatari ya kupata tatizo hili ni busara kujiepusha na matumizi holela ya dawa za hospitalini na vipodozi ambavyo vimepigwa marufuku na Serikali.

Homoni ni kichocheo kinachozalishwa ndani ya kiumbe hai na husafiri kupitia vimiminika ndani ya mwili kama vile damu kwa ajili ya kuchokoza au kuhamasisha tishu au seli fulani zifanye jambo fulani.

Zipo aina nyingi za homoni kama vile kuendeleza ukuaji, umeng’enyaji wa vyakula, kufanikisha tendo la ndoa, kudhibiti joto la mwili na kutoa taarifa ya ukosefu wa maji mwilini kwa kupata kiu.

Homoni huzalishwa kwenye tezi maalumu ndani ya mwili kama vile kwenye ubongo, shingo, ini, kende kwa upande wa wanaume na ovari kwa wanawake.

Wataalamu wanasema homoni inatolewa kwa kiwango kidogo sana, lakini huweza kutoa amri kwa haraka sana ili kufanikisha jambo fulani la mwili.