Mbinu mpya kuwafikia walio hatarini kupata VVU

Katika kuhakikisha wananchi walio katika hatari ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), wanapima afya zao, mbinu mpya itatumika ili kuwapata.

Watendaji wa mradi wa Afya Kamilifu kwa ushirikiano na wataalamu wa afya wa kliniki za Serikali na hospitali teule, watawatumia waliogundulika na VVU kuwapata walio katika mazingira hatarishi ikiwamo marafiki zao, ndugu, jamaa na watu wao wa karibu.

Mradi huo unalenga kuimarisha utoaji wa huduma na matibabu ya kufubaza VVU mkoani Tanga na visiwani Zanzibar, kwa muda wa miaka mitano.

Mkurugenzi mkaazi wa Amref Afrika, Dk Florence Temu anasema badala ya kupima watu ambao hawapo kwenye hatari ya maambukizi watawatumia ambao wamejitokeza kupima na kukutwa na virusi kuwaleta watu waliowazunguka ili kupima.

“Hawa wana jamaa zao, watoto, wenza na hata marafiki wanaowazunguka. Tunaamini hii itatusaidia kuwapata walio katika hatari ya kupata au wameshapata maambukizi ya VVU na kadri watakavyokuwa wanakuja wapya, ndivyo tutakavyokuwa tunawafikia na kupanua mtandao,” anasema Dk Temu.

Pia, anasema hatua hiyo itasaidia kutumia vizuri rasilimali iliyopo badala ya kuitawanya kwa watu ambao hawapo katika hatari ya kupata maambukizi.

“Lakini watakaopenda kupima kwa hiari pia watapata nafasi hiyo kila mahali ambako mradi huo utakuwapo, lengo ni kuwafikia wananchi wengi zaidi,” anasema Dk Temu.

Anafafanua kuwa watawatumia viongozi wa dini ambao watakuwa na fungu maalumu la fedha kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi kujitokeza kupima, kutumia dawa na kuacha unyanyapaa kwa wanaotumia dawa.

“Tunajua Serikali haina dini, lakini inasemekana asilimia 85 ya watu wanaamini imani za dini zao hivyo kwa kuwatumia viongozi wa imani kuwa wahamasishaji, waumini wanaweza kuona umuhimu wa kupima, kutumia dawa na kufubaza virusi vya Ukimwi (ARVs).”

Meneja Mradi wa Afya Kamilifu, Dk Edwin Kilimba anasema mradi huo utagharimu Dola milioni 11 za Marekani (Sh24 bilioni) kwa mwaka wa kwanza na kila mwaka utakuwa na bajeti yake hadi kukamilika mradi.

Anasema mradi huo wa miaka mitano kuanzia 2018 hadi 2022 umefadhiliwa na Shirika la Marekani la kuzuia na kudhibiti magonjwa (CDC ).

Dk Edwin anasema watatekeleza mradi huo pia kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali ya Tanzania Communication and Development Center (TCDC)na Chuo Kikuu cha Maryland Baltimore (UMB).

“Mradi huu unalenga uhamasishaji wa kufikia 90 ya upimaji na kutambua hali za watu, 90 ya kutumia dawa na 90 ya kutokuwa na maambukizi mapya,”anaeleza Dk Kilimba.

Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa linalopambana na Ukimwi (UNAIDS) iliyozinduliwa Machi 13 mjini Geneva Uswisi inaonyesha pamoja na kupungua kwa maambukizi mapya duniani kote, bado maambukizi miongoni mwa wanaotumia sindano kujidunga dawa za kulevya, yanaongezeka.