Membe afungasha wanasiasa waliotia fora mwaka 2018

Mwaka 2018 unakwisha ukiacha alama katika ulingo wa kisiasa ambapo baadhi ya viongozi wa siasa wameng’ara kwa utendaji mzuri wakipata sifa serikalini na mbele ya wananchi.

Miongoni mwa viongozi waliong’ara ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka ambaye Septemba 8, Rais John Magufuli alimtangaza kuwa Mkuu wa Mkoa anayeongoza wa kufanya kazi vizuri.

Pia, CCM imeingia katika vita mpya dhidi ya wagombea urais wa mwaka 2015, baada ya katibu wake mkuu, Dk Bashiru Ally kumtuhumu hadharani Bernard Membe kuwa anakwamisha mikakati ya urais 2020.

Mwanri

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Agrey Mwanri naye ametoa fora kutokana na utendaji wake, lakini kubwa zaidi ni kauli zake za kusisitiza jambo zilizoonekana kama vichekezo lakini akiwa akionyesha umakini wa kufuatilia mambo.

Miongoni mwa kauli zake zilizotia fora ni ile ya ‘nyoosha mkono jifanye kama unajikuna’ ambayo aliitoa wakati akitaka kujua nani anaona maagizo yake ni ya kipuuzi.

Kauli nyingine ni ile ya ‘Fyekelea mbali’ ambayo pia alikuwa akiwaonya watendaji mkoani humo, ikifuatiwa na kauli ya sasa ya ‘Injia soma ramani’.

Kauli zote hizo zimemfanya Mwanri kuwa maarufu kwenye mitandao ya jamii huku pia akionekana kusimamia vyema maendeleo ya Mkoa wa Tabora.

Biteko

Mwanasiasa mwingine anayechipukia ni Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko aliyeteuliwa Januari mwaka huu baada ya kuongoza kamati ya muda iliyochunguza madini ya Tanzanite.

Biteko aliteuliwa kumsaidia Waziri Angela Kairuki baada ya Wizara hiyo kuundwa ikinyofolewa kutoka kwa iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini.

Kamati aliyokuwa akiiongoza Biteko iliundwa na Spika wa Bunge Job Ndugai Juni 2017, akiipa kazi ya kuchunguza Sekta nzima ya Madini ya Tanzanite.

Mbali na Doto Biteko ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wajumbe walikuwa ni pamoja na Mohammed Mchengerwa, Ezekiel Maige, Balozi Adadi Rajabu, Dk Merry Mwanjelwa, Subira Mgalu, Juma Omari, Abdalla Mtolea na Joseph Ole Millya.

Ripoti ya kamati hiyo ilikabidhiwa kwa Rais John Magufuli Septemba 2017 Ikulu jijini Dar es Salaam.

Miongoni mwa kazi alizofanya Biteko ni pamoja na kukamata madini ya vito aina ya Rhodilite yenye uzito wa takribani tani saba yaliyokuwa yamefichwa nyumbani kwa mchimbaji wa madini hayo, Juvenal Mnene ambaye ni mmiliki wa kampuni ya J. J. Mnene & Partners Julai 2018 wilayani Gairo Morogoro.

Zitto

Licha ya umaarufu wake wa muda mrefu, Zitto aliibuka upya mwaka huu pale alipoibua hoja ya Sh1.5 trilioni alizodai kuwa hazijulikani zilipo kutoka na ripoti Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2016/17 iliyotolewa Aprili mwaka huu.

Baada ya Zitto kulipua bomu la Sh1.5 trilioni, Chama cha Mapinduzi kupitia Katibu wake wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole kilijibu ambapo kiongozi huyo alitumia ‘flip chart’ kufanya hesabu kufafanua kuwa hakukuwa na upotevu wa fedha hizo.

Hoja ya Zitto ilimkera Rais Magufuli ambaye katika hotuba yake ya Aprili 20 Ikulu ya Dar es Salaam alikanusha madai hayo. Pia, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alitoa taarifa bungeni Dodoma kufafanua fedha hizo.

Licha ya ufafanuzi wote huo, hoja ya Sh1.5 trilioni iliendelea kushika kasi kwenye mitandao ya jamii kama moto kichakani, jambo lililompa umaarufu Zitto ambaye ni Mbunge pekee katika chama cha ACT Wazalendo.

Nape

Nape aliyetimuliwa uwaziri mapema mwaka 2017 ameendelea kung’ara, mwaka huu akijikita zaidi kutetea wakulima wa korosho.

Nape aliuanzisha mtiti mapema Mei mwaka huu akishikilia shilingi ya aliyekuwa waziri wa kilimo, Dk Charles Tizeba kwa kutoridhishwa na majibu ya Serikali kuhusu fedha za ushuru wa mauzo ya nje ya korosho (export levy).

Wiki moja baadaye Mei 24, Nape aliibua tena hoja hiyo na kumfanya Spika Job Ndugai kutoboa siri ya Waziri Tizeba kulia kama mtoto mbele ya kamati ya bajeti.

Hata hivyo, mzozo huo uliokuwa pia ukipinga mabadiliko ya sheria ya korosho yalikwisha kwa sheria hiyo kubadilishwa, huku Rais Magufuli akiwaonya wabunge 17 wa mikoa ya Kusini.

Kwa upande wake Nape akionyesha kunywea katika suala hilo aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter akiwataka wananchi kuiunga mkono Serikali katika sheria mpya Export Levy halafu baada ya msimu huu wa zao la korosho kupita itathaminiwa tena ili kuona mafanikio na changamoto zake.

Hata hivyo, Nape ameonyesha kuguswa na hatua ya Serikali ya kununua korosho akipinga njia zinazotumika akisema hazitamaliza njia haramu za ununuzi maarufu kama Kangomba.

Membe aibuka upya

Hivi karibuni, CCM imeingia katika vita mpya dhidi ya wagombea urais wa mwaka 2015, baada ya katibu wake mkuu, Dk Bashiru Ally kumtuhumu hadharani Bernard Membe kuwa anakwamisha mikakati ya urais 2020.

Awali Membe aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika utawala wa awamu ya nne alikuwa kimya huku CCM ikielekeza nguvu zake upinzani.

Akihutubia Mkutano Mkuu wa CCM mkoani Geita hivi karibuni, Dk Bashiru alisema Membe anatuhumiwa kuandaa mipango ya kumkwamisha Magufuli katika uchaguzi wa Rais na kwamba tangu ateuliwe hajawahi kuonana naye.

Baada ya wito huo, kulisambaa ujumbe katika mitandao ya kijamii ulioandikwa na mtu aliyejiita Bernard Membe akisema yuko tayari kumwona.

Mzozo huo uliendelea kushika kasi ukiwahusisha viongozi wastaafu wa chama hicho, akiwemo Spika mstaafu Pius Msekwa aliyemkosoa Dk Bashiru, huku Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba akimuunga mkono Dk Bashiru.

Ester Bulaya na kikokotoo

Baada ya Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kutangaza utekelezaji wa kanuni za sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii, Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya (Chadema), amesema anakusudia kuwasilisha muswada binafsi bungeni kupinga matumizi ya vikokotoo vya pensheni kwa madai kuwa vinamnyonya mfanyakazi.

Harakati za Bulaya zilitiwa nguvu na pongezi kutoka Spika wa Bunge Job Ndugai akimsifia Bulaya kwa kuibua hoja hiyo. Pia, vyama vya wafanyakazi vimeunga mkono hoja ya mbunge huyo.

Mnyika

Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika ameumaliza mwaka 2018 kishujaa baada ya kumwambia Rais John Magufuli kuwa licha ya kupiga marufuku watu kusema vyuma vimekaza, ukweli ni kuwa vyuma vimekaza.

Mnyika aliyasema hayo Desemba 19, 2018 katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la upanuzi wa barabara ya Morogoro jijini Dar es Salaam eneo la Kimara Stop Over alipopewa nafasi ya kusalimia.

Pia, aliitaka Serikali kuwalipa fidia wananchi waliokuwa wanaishi kando ya barabara hiyo ambao nyumba na maeneo yao ya biashara yalibomolewa, huku akimtaka Rais Magufuli kuondoa vikwazo vya demokrasia nchini.