Ndoa zinavyochanganya mabinti mjini

Muktasari:

  • Babu akamwambia nenda kwa wanawake wote watatu, wagawie kiasi sawa cha pesa kila mmoja. Kisha kati yao, atakayetumia kwenye mambo ya msingi ya kukusaidia wewe, yeye na kesho yenu, huyo ndiye ana sifa ya kuwa mke.

Tuifufue hii hadithi – mwanaume mmoja alikwenda kuomba ushauri kwa mzee mwenye hekima. Akamuuliza, ‘Babu, nina wanawake watatu, nataka kuoa mmoja, nioe yupi?’

Babu akamwambia nenda kwa wanawake wote watatu, wagawie kiasi sawa cha pesa kila mmoja. Kisha kati yao, atakayetumia kwenye mambo ya msingi ya kukusaidia wewe, yeye na kesho yenu, huyo ndiye ana sifa ya kuwa mke.

Ikawa hivyo, akawagawia wanawake wote watatu kiasi sawa cha pesa.

Wa kwanza akaenda saluni, akaweka nywele mpya, kope mpya, kucha mpya, akanunua nguo mpya, manukato mapya na makokoro kibao ya urembo. Hela yote ikaishia huko. Akarudi kwa mwanaume kumuonyesha jinsi alivyopendeza.

Wa pili akaenda saluni pia, akajitia mazagazaga yote ya urembo, akapendeza kumkaribia yule wa kwanza, lakini yeye hakutumia pesa yote. Iliyobaki akaenda kumnunulia mwanaume nguo mpya na kumpelekea kama zawadi.

Watatu hakuichukua ile pesa, ila akamwambia mwanaume, ‘mpenzi, hii pesa ni nyingi, inatosha kuwa mtaji wa biashara yenye kueleweka kabisa. Kwanini tusifungue.’ Ikawa hivyo, kwa msaada wa mwanamke ile pesa ikatumika kufungulia biashara ambayo baada ya muda ikaanza kuingiza faida na wakapata zaidi ya walichokuwa nacho.

Basi mpaka hapo ilikuwa wazi kuwa mwanamke aliyestahili kuwa mke kwa mujibu wa ushauri wa babu ni huyu wa tatu.

Basi mwanaume naye wala hakufanya ajizi kuchagua wa kumuoa. Na alichokifanya ni alimuoa mwanamke mwenye wowowo kubwa.

Kwa nini nimetaka tuirudie hii hadithi? Kwa sababu mijini siku hizi moto umewaka. Wadada wanatafuta ndoa kwa kasi na mbinu zote kama mwanasiasa anayependa faida za kupigiwa kura lakini hapendwi na wapiga kura.

Wanawake wanatumia kila namna kupata ndoa. Kauli mbiu kwao ni kuolewa, kuolewa na kuolewa.

Lakini kama ndoa ni jambo jema, kwa nini lipiganiwe sana na upande mmoja? Swali hili likaniletea jibu kwamba, wanawake wengi wanatafuta sana ndoa kwa sababu wengi wao hawana malengo yoyote. Wakitazama kesho, wanachokiona ni kuolewa, kupata watoto, kisha wajukuu, kisha kuzeeka, halafu kufariki. Kwa hiyo ukiitoa ndoa Kesho yao inakuwa ni kuzeeka na kufa – hawataki.

Wakati vijana wengi wa kiume, wenyewe wakitazama Kesho, wanaona wanamiliki biashara kubwa, wanamiliki kampuni, wanavumbua vitu vikubwa vya kuisaidia jamii, wanaanzisha miradi na zaidi. Kwa hiyo hata ukichomoa ndoa bado wana sababu nyingine za kuendelea kuishi.

Sote hapa tuna mabinti. Tuna Watoto wa kike, dada zetu na zaidi, hivyo ni bora tuwaeleze ukweli wa maisha. Ndoa ni suala la bahati tu, halihitaji maandalizi ya kiasi kikubwa kama wanavyoamini. Anaweza mtu akakudanganya kama unataka kuolewa kuwa hivi, ukawa hivyo na ukazeeka bila ndoa.

Lakini tatizo liko wapi kuzeeka bila ndoa ilihali ukiwa mwanamke uliyefanikiwa katika malengo yako. Kwa hiyo ni vyema kabla hawajawaza ndoa, waweke malengo binafsi ya maisha yao ambayo hayategemei ndoa – hiyo ni bora zaidi.

Hatusemi kwamba kuolewa ni jambo baya, hapana. Tunachosema ni kwamba dunia haijawahi kumkumbuka mwanamke kwa sababu ameolewa, inawakumbuka wanawake waliokuwa na malengo ya kufanya mambo makubwa, na wakatimiza malengo yao. Wasichanganywe na siasa za ndoa.