Profesa Qorro: Elimu ya Tanzania inatuandaa kumtumikia mkoloni

Tuesday November 13 2018

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Novemba 11, 2017 Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alisema kuna haja ya kutafakari upya mfumo wa elimu na kushauri kuanzishwa kwa mjadala utakaohusisha makundi yote.

Alisema hayo katika kongamano la wanataaluma lililofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Miezi michache baadaye, Mkapa alizungumzia tena suala hilo wakati wa hafla ya kumuaga makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Idris Kikula aliposema kuna janga katika elimu, akisema anapata taarifa hizo kwa kusoma barua za magazetini, kupelekewa ripoti kutoka sekta binafsi na kusikia minong’ono kutoka vyuo vya umma.

Aprili 18, mrithi wake, Jakaya Kikwete akazungumzia suala hilo katika kongamano la Chuo Kikuu cha Havard lililopewa jina la “Mageuzi ya Afrika Katika Karne ya 21, aliposema wahitimu wengi barani Afrika ni wa elimu ya msingi na hivyo kuna haja ya kuweka mkazo katika elimu.

Wakati mjadala huo ukionekana kama umetulia, Profesa mstaafu, Martha Qorro wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amerejesha tena suala hilo.

“Mjadala wa elimu unahitajika nchini,” alisema mhadhiri huyo wa UDSM.

“Naungana na marais wastaafu wa awamu ya pili, Benjamini Mkapa na ya tatu, Jakaya Kikwete walivyotangulia kusema hilo.”

Profesa Qorro alisema hayo katika mahojiano na Mwananchi wiki hii alipozungumzia masuala mbalimbali ya kielimu. Mahojiano yalikuwa hivi:

Swali: Profesa iwapo kutakuwa na mjadala wa elimu, unapendekeza mambo gani hasa yajadiliwe?

Profesa Qorro: kwa upande wangu naona vitu viwili moja kwa moja vijadiliwe; kwanza ni kujadili falsafa inayoongoza elimu yetu ni ipi. Wakati wa Mwalimu Nyerere ilikuwa ujamaa na kujitegemea na ndiyo maana tulikuwa tunatoka darasani kwenda kufanya kazi kwa vitendo.

Falsafa hiyo ilikuwa inamuandaa mwanafunzi kuishi na watu, kujitegemea na ujamaa. Lakini sasa ni kama imewekwa kando kulingana na sababu mbalimbali, hivyo ipo haja ya kujadili mpya au kuiboresha hiyo.

Lazima mwalimu ajue ninamuandaa huyu mwanafunzi awe nani awe na sifa gani, tofauti na hapo ni vigumu kuandaa silabasi zinazoendana.

Swali: Jambo la pili unalopendekeza ni lipi?

Profesa Qorro: Jambo la pili ni kuangalia mfumo wa elimu uweje, hususani katika suala la uwasilishaji.

Uwasilishaji kwa maana ya lugha, ni muhimu kukawa na uelewa wa pamoja, ili tuelewane matumizi ya Kiswahili yanahitajika na kwangu mimi nasema kama Watanzania lugha hiyo ni lazima kutumika.

Mjadala mmoja uwe na hoja hizi mbili. Kwa mtazamo wangu naona tutapata pa kuanzia.

Swali: Vitabu vya mitaala vinawasaidia wanafunzi?

Profesa Qorro: Kuna mambo mengi, Katika mazingira ya elimu ya kusoma kwa kukariri, wanafunzi wanafaulu mtihani wanajibu majibu sahihi lakini kwa kukariri siyo kwa kuyaelewa.

Ukiwa kwenye mazingira hayo kwa miaka 10, 20 chochote kinawezekana, wala usishangae kuwapo kwa vitabu vilivyokosewa.

Kwa sasa ni kama tumepoteza mwelekeo. Tutafakari tupo wapi. Inaonyesha jinsi gani ilivyo muhimu kukubaliana kuwepo kwa mjadala wa pamoja. Kwanza tukubaliane tunataka vitabu vyetu vitufundishe tuwe nani; tuwe mabepari au wajamaa. Tukishakubaliana hayo tunaweza kuamua kuandika vitabu. .

Swali: Umekuwa ukikitetea Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia, unadhani tuna wataalamu wa kutosha kufundisha lugha ya Kiswahili?

Profesa Qorro: Inawezekana wasiwepo. Kukosa walimu wa Kiswahili wakati hii ndiyo nchi inayojulikana ulimwengu mzima kuwa ni ya Waswahili, ni aibu. Hatupaswi kulalamika. Ni lazima tubadilike, tuwaandaae wataalamu wa Kiswahili wa kutosha hapa nchini na kupeleka nchi nyingine. Tukubali kuwekeza katika elimu ambayo ina tija kwa taifa, siyo tija kwa wengine.

Kwetu kwanza. Elimu iliyopo bado inamtumikia mkoloni hadi leo. Ipo kama tulivyoirithi, hatujabadilisha mambo ya msingi.

Tunaandaa watu wa kuwatumikia Waingereza, haimuandai Mtanzania kwenda kufanya kazi ya asili yake. Utashangaa kwenye usaili wa kazi inatumika lugha ya Kiingereza na baada ya hapo haitumiki tena.

Swali: Kwa nini unadhani ni muhimu kutumia Kiswahili kufundishia?

Profesa Qorro: Ngoja nikupe sababu kwa nini ni muhimu kwa mtiririko ufuatao; mtoto anapofika umri wa miaka mitano anaanza chekechea akifundishwa kwa lugha ya asili--nazungumzia Mtanzania halisi anayetokea kijijini.

Anapofika miaka saba anaanza darasa la kwanza, anajifunza Kiswahili na anaambiwa kuzungumza lugha yake ya asili ni mwiko.

Anahangaika nacho kwa miaka saba, akibahatika kufaulu na kwenda kidato cha kwanza, anafundishwa Kiingereza na anaambiwa Kiswahili marufuku. Unaweza kuona jinsi wanafunzi wanavyopata tabu kujifunza lugha ya kigeni kwa miaka minne.

Utafiti wa Wizara ya Elimu wa mwaka 2014 unaonyesha wanafunzi wanaosoma shule za Kiswahili ni asilimia 98, wanaosoma za Kiingereza ni asilimia mbili tu.

Kwa namna hii atasoma kwa kukariri na atajua Kiingereza kitakuwa kibovu atakachorithi kutoka kwa walimu wake ambao nao walipita kwenye mfumo huohuo.

Swali: Kiingereza bado lakini kimetumika kufundishia wataalamu wengi nchini, huoni umuhimu wake?

Profesa Qorro: Nakubaliana na wewe kuna wasomi, lakini utaalamu walioupata unaifikia jamii? Kuna wanaosema tukiboreshe kuanzia shule ya msingi. Mimi nasema hapana. Tanzania tunapaswa kuendeleza lugha yetu ambayo ni tunu ya taifa; Kiswahili.

Tuseme tumekiboresha kuanzia shule ya awali na wote wameelewa Kiingereza. Wakaendelea na masomo na kuwa wataalamu, ambao wanapaswa kuitumikia jamii isiyo ya wasomi. Watafikishaje ujumbe? Ndiyo maana kuna pengo kubwa kati ya wasomi na jamii.

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Maendeleo na Elimu (ADEA) na uliofanywa na Ngugi wa Thiong’o wote ulikuja na majibu kuwa kilichofanywa na wakoloni ni kupandikiza lugha zao ili kuitenganisha jamii na wasomi.

Kazi ya msomi ni kuunganisha kilichotenganishwa na mkoloni, maana yake tuachane na kutumia lugha ya Kiingereza kufundishia ili tuunganishe jamii na wasomi.

Advertisement