Terehe uchaguzi mitaa wingu zito

Dodoma. Tarehe ya uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu bado kizungumkuti huku Serikali ikisema itaitangaza baada ya kukamilisha maandalizi yanayoendelea.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo amelieleza Mwananchi hivi karibuni kuwa uchaguzi huo “utafanyika mwishoni mwa mwaka huu” na kwamba tarehe kamili ya uchaguzi itatajwa wakishamaliza maandalizi.

Ingawa Jafo hakueleza maandalizi hayo ni yapi na yatakamilika lini, hivi karibuni naibu wake, Mwita Waitara alilieleza Bunge kuwa Serikali imeanza kufanyia marekebisho mapungufu yaliyojitokeza katika uchaguzi wa mitaa uliopita.

Waitara aliyekuwa anajibu hoja za wabunge waliochangia taarifa ya Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba, alisema yapo malalamiko yaliyotolewa na wananchi katika uchaguzi wa mwaka 2014 ambayo yanafanyiwa kazi na wataalam na wakimaliza yatarudishwa halmashauri, vyama vya siasa na wadau wote watashirikishwa katika kuandaa kanuni.

Mapema, Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini aliitaka Serikali kuwashirikisha wadau katika maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa.

“Maandalizi yawe wazi wananchi wote washirikishwe, uchaguzi uliopita ulikuwa na fujo. Tunaomba wadau tushirikishwe ili tuweze kupitia kanuni na uchaguzi uweze kupita vizuri,” alisema.

Suala la kutangaza tarehe ya uchaguzi wa mitaa limekuwa likizua mjadala kila unapofanyika na katika uchaguzi uliopita mwaka 2014, tarehe ya uchaguzi ambayo ilikuwa Desemba 14, ilitangazwa Septemba 14 siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kukutana na vyama vya siasa kupitia Kituo cha Demokrasia (TCD).

Kwa muda mrefu vyama vya upinzani vimekuwa vikilalamika kuwa kuchelewa kutangaza tarehe ya uchaguzi kunainufaisha CCM ambayo hupata fursa ya kujinadi kupitia viongozi wa Serikali.

Katika uchaguzi wa 2,014, CCM ilinyakua vijiji 9,378 kati ya 12,443 sawa na asilimia 75.4, Chadema vijiji 1,754 (asilimia 14) na CUF vijiji 516 (asilimia 4). Vyama vingine vilipata chini ya asilimia 1.

Vitongoji CCM ilipata 48,447 kati ya 60,688 sawa na asilimia 79.8, Chadema 9, 145 (asilimia 15) na CUF 2,561 (asilimia 4.2). Mitaa CCM 2,583, Chadema 980 na CUF 266.