Tale afunguka Diamond kuwa na walinzi wengi

Muktasari:

  • Asema anatembea na vito vyenye thamani ya zaidi ya Sh140 milioni ambapo kama hakuna ulinzi wa kutosha anaweza kuvamiwa na kuporwa kama ilivyotokea Mtwara

Umewahi kujiuliza Diamond Platnumz anavaa madini ya kiasi gani shingoni na mikononi, lakini bila shaka utakuwa unajiuliza kwa nini anaongozana na walinzi wengi.

Babu Tale ambaye ni meneja wa msanii huyo ameeleza ni kwa nini Diamond anaongozana na walinzi wengi.

Ufafanuzi wa Tale umekuja wiki moja baada ya staa huyo kuongozana na walinzi 11 na kuzuia maswali na taharuki kwenye maeneo aliyokuwa akipita ikiwamo kwenye Hoteli ya Hyatt Kilimanjaro Hoteli alipoenda kwa shughuli zake binafsi.

“Diamond huwa anavaa vito vyenye thamani ya zaidi ya Sh140 milioni akiwa matembezini, akiwa jukwaani gharama inaongezeka kadri anavyovaa vingi, lakini pia ni mkakati wa kibiashara, yule ni staa na anapaswa anapopita ijulikane anapita nani? Anasema Babu Tale, alipofanya mahojiano na gazeti hili kuhusu suala hilo.

Akitolea mfano Tale anasema cheni ambayo Diamond aliwahi kunyang’anywa akiwa jukwaani mkoani Mtwara, thamani yake ilikuwa Sh40 milioni, unaweza kuona ni hasara kiasi anaweza kupata iwapo hakuna ulinzi wa kutosha.

Tale anafafanua kuwa Diamond ana mashabiki wengi, wengine wakimuona huwa wanalia ni rahisi hao kumvamia kwa nia njema lakini wakiwa wengi wanaweza kumuumiza au kujiumiza wao wenyewe.

‘Mpaka mnaomuona Diamond hapo alipofika leo ni kwamba ametengenezwa na ndio maana sehemu yoyote anayopita lazima shughuli zisimame na suala la kuwa na walinzi ni moja ya kutengeza jina hilo.

“Pia katika biashara lazima uwe na ubunifu, hivyo kuwa na walinzi wengi ni moja ya ubunifu wa kumfanya msanii wetu aendelee kuwa juu,” anasema Tale.

Tale anasisitiza kuwa kwa msanii nyota kukwepa ulinzi madhubuti ni kujiweka hatarini.

“Unaona hata viwanjani wapo mashabiki wanampenda mchezaji na kuamua kupenya uwanjani bila kujali ulinzi na mbwa wakali waliopo, sembuse msanii mwenye mashabiki wengi kama Diamond, mlinzi mmoja au wawili wananchi wanavyopagawa wakimuona hawataweza kuwazuia ndiyo maana hata iweje lazima awe nao wengi.

Tale anasema hataki kuzungumzia wasanii wengine kwa sababu hajui wanakuwa nao kwa sababu gani.