Tamthilia ya Sultan Visa na mikasa yake

Saturday April 6 2019

 

Siku 10 kuanzia leo, tamthilia ya Sultani inayoonyeshwa na kituo cha televisheni cha Azam itatimiza mwaka mmoja tangu ianze kuonyeshwa nchini.

Majina kama Şehzade Mehmed, Mihrimah Sultan, Rüstem Pasha au Beyhan Sultan yamekuwa sehemu ya gumzo la wafuatiliaji wa tamthilia nchini.

Tofauti na tamthilia zilizowahi kutamba nchini kama vile La Revange, The Promise au Shade of Sin za Amerika ya Kusini na Ufilipino, Sultan imekuwa na mvuto wa kipekee hasa kwa kuwa imenakilishwa kwa Kiswahili.

Tamthilia hiyo yenye asili ya Uturuki ambayo hufahamika kama Muhteşem Yüzyıl, imeanza kuruka nchini ikiwa tayari na umri wa miaka saba tangu ilipozinduliwa Januari 1, 2011.

Tanzania kinara

Tanzania ni nchi ya kwanza Afrika Mashariki na ya nne Afrika kuionyesha tamthilia hiyo. Nchi nyingine zilizoionyesha Afrika ni Algeria, Misri na Tunisia.

Advertisement

Misri ilianza kuionyesha tamthilia hiyo miezi michache baada ya kuzinduliwa mwaka 2011 na ilionyeshwa tena katika kituo kingine cha televisheni nchini humo mwaka 2014.

Algeria ilianza kuonyeshwa mwaka 2015 na Tunisia ilionyeshwa mwaka 2013.

Hurrem aliondolewa baada ya kupata msongo wa mawazo

Mmoja wa waigizaji wakuu wa tamthilia hiyo Meryem Uzerli maarufu Hurrem alicheza katika msimu wa kwanza hadi wa tatu lakini katika ule wa nne ikachezwa na Vahide Perçin.

Mtayarishaji wa tamthilia hiyo, Timur Savci alisema Meryem aliugua ugonjwa wa ‘burnout syndrome’ unaosababishwa na mtu kukinai jambo fulani na hivyo kushindwa kuendelea kulifanya.

Hata hivyo pia kulikuwa na tetesi kwamba walishindwana katika malipo na hivyo mwanamke huyo akaamua kutimkia Ujerumani ambako mmoja wa wazazi wake wanatokea.

Hata hivyo, Hurrem na watu wake wa karibu walisisitiza kuwa kilichomuondoa ni tatizo la kiafya na siyo malipo.

Yapingwa kila kona

Pamoja na kufurahia matokeo chanya ya kazi yao kupendwa, waandaaji wa tamthilia hiyo wamekuwa wakikumbana na vigingi vya kutokubalika katika nchi mbalimbali.

Kwa mfano Uturuki yamewahi kufanyika maandamano kupinga uonyeshwaji wa tamthilia hiyo.

Vituo vya redio na televisheni vinavyomilikiwa na Serikali ya Uturuki vimewahi kukiri kupokea malalamiko kutoka kwa watu zaidi ya 70,000 wakilalamikia namna ujumbe ulivyowasilishwa kwamba unadanganya kuhusu himaya ya Ottoman.

Waziri mkuu wa Uturuki wa wakati huo ambaye sasa ni Rais, Recep Tayyip Erdoğan aliwahi kutishia kuzuia uonyeshwaji wa tamthilia hiyo akisema unawavunjia heshima watawala wa Taifa hilo waliotangulia.

Nchini Ugiriki ambako tamthilia hiyo ilionyeshwa kati ya mwaka 2012 na 2014 ilikumbana na misukosuko, baada ya kuwapo azimio la kuipiga marufuku kwa madai kuwa inaweza kuambukiza tamaduni za Kituruki.

Chama cha siasa cha Golden Dawn nchini humo kilitoa tamko kwamba, tamthilia hiyo ni muhimu ikapigwa marufuku kwa sababu umaarufu wake unaweza kuchangia mabadiliko ya kitamaduni kwa wananchi wao.

Tamthilia hiyo pia ilisababisha mabadiliko ya sheria katika nchi ya Macedonia baada ya kupata umaarufu mkubwa. Sheria mpya ilipiga marufuku tamthilia kutoka Uturuki na badala yake zionyeshwe za kwao ili kuenzi na kukuza utamaduni wao.

Nchini Pakistan huenda tamthilia hiyo isingemalizika kama wananchi wasingekuja juu kudai iendelee. Mara kadhaa ilikuwa ikikatishwa baada ya kupigwa marufuku na mamlaka.

Hata hivyo, wafuatiliaji wake walikuwa wakali wakitaka iendelee ndipo serikali ilipoweka mikono juu na kuicha imalizike.

Muhimu kufahamu

Mwandishi mkuu wa tamthilia hiyo, Meral Okay alifariki Aprili 9, 2012, ikiwa ni mwaka mmoja tangu kuanza kwa tamthilia hiyo.

Hurrem (Meryem Uzerli) aliwahi kukataa ofa ya dola 500,000 sawa na wastani wa Sh1.1 bilioni ili kuhudhuria sherehe ya tajiri. Badala yake alimwambia apeleke fedha hizo kwenye taasisi zinazosaidia wasiojiweza na yeye apewe risiti tu. Alipojiridhisha fedha hizo zilipelekwa mahali husika alihudhuria sherehe hiyo.

Advertisement