Taswira ya kivuko Mv Nyerere katika kesi ajali ya Mv Bukoba

Wednesday October 3 2018

 

Kufuatia ajali hiyo kumekuwa na sauti zikipazwa kutoka kwa watu mbalimbali, wakiwamo wanasiasa na wanaharakati wa haki za binadamu wakitaka hatua za kinidhamu na za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na ajali hiyo.

Tukio hili linaibua kumbukumbu nyingine ya miaka 22 iliyopita, kwenye tukio kama hili wakati meli ya MV Bukoba ilipozama na kuua mamia ya watu kwani kuna mambo na au mazingira ama yanayofanana au yanayokaribia kufanana.

Ajali ya MV Bukoba ilitokea alfajiri ya siku ya Jumanne ya Mei 21, 1996 ndani ya ziwa hilohilo, wakati ikitokea Bukoba kwenda Mwanza na kuua watu zaidi ya 800.

Ingawa mpaka sasa hakujawahi kupatikana uthibitisho wa kitaalamu wa chanzo cha ajali ya MV Bukoba, lakini sababu kubwa iliyokuwa na inayoweza kutajwa mpaka sasa ni uzito kupita kiasi, hoja ambayo inafanana na ya Mv Nyerere.

Tayari Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kwa maelekezo ya Rais Magufuli imetangaza kuunda tume kuchunguza chanzo halisi cha ajali hiyo huku taarifa za awali zikisema kivuko hicho kilikuwa kimebeba watu na mizigo kuliko uwezo wake.

Kivuko hicho inaelezwa kina uwezo wa kubeba abiria 100 hadi 101 tu na mizigo ya uzito wa tani 25 tu, lakini taarifa zinaeleza kuwa kilikuwa kimebeba mizigo yenye uzito mkubwa kuliko uwezo wake ingawa pia bado uzito huo haujabainika.

Safari ya uchukuaji wa hatua za kisheria imeshaanza, baada ya Rais Magufuli kuamuru kukamatwa kwa baadhi ya watendaji wa kivuko hicho na wa mamlaka nyingine zinazosimamia vivuko na usafiri majini.

Miongoni mwa watuhumiwa waliokwishakamatwa ni pamoja na nahodha wa kivuko hicho, ambaye inasemekana yeye hakuwamo katika safari hiyo, na mhandisi wa kivuko aliyeokolewa baada ya kukaa majini kwa siku mbili.

Hatua nyingine ambazo zimeshachukuliwa ni uamuzi wa Rais Magufuli kuvunja Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) na Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Majini (Sumatra), huku Waziri Mkuu Majaliwa naye akimsimamisha mtendaji mkuu wa Temesa ili kupisha uchunguzi wa ajali hiyo.

Mzunguko wa hatua zote hizi unaweza kuishia katika kuchukuliwa hatua za kisheria na kufikishwa katika vyombo vya kisheria.

Hatua hii ndio inayorejesha kumbukumbu ya kesi ya ajali ya Meli ya MV Bukoba na hitimisho lake.

Kesi ya Mv Bukoba

Hatua za kisheria dhidi ya wale watakaobainika kuhusika kwa namna yoyote katika ajali hii ya MV Nyerere zinaibua kumbukumbu ya kesi ya ajali ya MV Bukoba si tu jinsi mahakama ilivyoamua, bali pia hukumu ya kesi hiyo hapana shaka itatumika katika kesi ya MV Nyerere.

Mazingira ya ajali ya kivuko cha MV Nyerere na hatua za kisheria zitakazochukuliwa dhidi ya watuhumiwa waliotiwa mbaroni na watakaoendelea kutiwa mbaroni, kuhojiwa na hatimaye kushtakiwa, yanafanana na yale ya Mv Bukoba.

Hapa ndipo kumbukumbu ya kesi na hukumu ya MV Bukoba inapoibuka ndani ya kesi ya MV Nyerere. Hivyo ni dhahiri hukumu ya MV Bukoba itakuwa ni rejea muhimu katika kesi ya MV Nyerere, si tu kwa upande wa utetezi bali hata kwa upande wa mashtaka.

Wakati upande wa utetezi unatarajiwa kuitumia hukumu ya kesi hii ndani ya mahakama kuionesha mahakama kuwa washtakiwa hawana kesi ya kujibu wala hatia, upande wa mashtaka hautakuwa na budi kuitumia nje ya mahakama kama kioo cha kuangalia upungufu kwenye kesi hiyo na kufanya marekebisho.

Ni kwa sababu hii tunafanya mapitio ya hukumu ya kesi ya MV Bukoba, hoja zilizokuwa zikibishaniwa na hitimisho la uamuzi wa mahakama kuelekea kesi ya MV Nyerere, ambao unaweza kutoa taswira kamili ya kesi hii.

Kufuatia ajali hiyo, watu kadhaa walikamatwa waliokuwa wakihusika kwa namna moja na uendeshaji na usimamizi wa meli hiyo na walioonekana kuwa na makosa walipandishwa kizimbani wakikabiliwa na mashtaka ya kuua bila kukusudia.

Baada ya kukamilika kwa mchakato wa mahojiano dhidi ya wale wote waliotiwa mbaroni na upelelezi wa awali, hatimaye waliopandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka hayo walikuwa ni watu wanne.

Katika kesi hiyo washtakiwa walikuwa ni pamoja na aliyekuwa Nahodha wa meli hiyo (mshtakiwa wa kwanza), Jumanne Rume Mwiru na aliyekuwa Mkaguzi wa Mamlaka ya Bandari (THA), Gilbert Mokiwa (mshtakiwa wa pili)

Wengine walikuwa ni Mkuu wa Bandari ya Bukoba, Alfred Sambo (mshtakiwa wa tatu, aliyefariki dunia muda mfupi baada ya kesi hiyo kuanza) na Mkuu wa Bandari ya Kemondo, Prosper Lugumila (mshtakiwa wanne).

Washtakiwa hao kwa pamoja walikuwa wakikabiliwa na jumla ya mashtaka 159 ya kuua bila kukusudia kinyume cha kifungu cha 195 cha Kanuni za Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania.

Walikuwa wakidaiwa kuwa Mei 21, 1996 majira ya saa 7:30 Asubuhi, karibu na lango la ghuba ya Mwanza, katika Ziwa Victoria, ndani ya Manispaa na Mkoa wa Mwanza, kinyume cha sheria waliwaua watu 159 (kama majina yao yalivyobainishwa kwenye kila shtaka katika mashtaka hayo 159).

Washtakiwa wote walikana mashtaka hayo na hivyo upande wa mashtaka kulazimika kuwasilisha ushahidi mahakamani kuhakikisha kuwa mahakama inawatia hatiani kwa mashtaka hayo na hatimaye kuwahukumu adhabu stahiki kwa mujibu wa sheria.

Kesi hiyo namba 22 ya mwaka 1998 ilisikilizwa na Jaji Juxon Mlay, katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza na upande wa mashtaka uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, William Magoma akisaidiana na Wakili wa Serikali, Eliezer Feleshi.

Feleshi baadaye aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kisha Jaji wa Mahakama Kuu na sasa ni Jaji Kiongozi.

Washtakiwa kwa upande wao wote walitetewa na mawakili Salum Magongo akisaidiana na wakili Galati Mwantembe.

Katika kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa, upande wa mashtaka uliwaita jumla ya mashahidi 32 na kuwasilisha mahakamani hapo jumla ya vielelezo vya ushahidi 15 kupitia kwa mashahidi hao.

Kupitia kwa mashahidi wake 31, na vielelezo hivyo upande wa mashtaka ulitaka kuthibitisha kuwa washtakiwa hao kwa nafasi zao walitenda au hawakutenda mambo yaliyosababisha uzembe uliosababisha meli hiyo kupinduka Mei 21, 1996 na kusababisha vifo vya watu hao 159 waliobainishwa.

Baada ya kusikiliza ushahidi wa mashahidi wote hao wa upande wa mashtaka na kupokea vielelezo hivyo, mahakama iliwaona washtakiwa kuwa wana kesi ya kujibu na kuwataka wajitetee.

Pamoja na mambo yote hoja ya msingi ambayo mahakama iliizingatia katika uamuzi wake ni uzembe gani uliofanywa na kila mshtakiwa au lipi ambalo hawakulifanya lililosababisha ajali ile.

Usikose kufuatilia kile walichokisema baadhi ya mashahidi wa upande wa mashtaka, washtakiwa walivyojitetea, walichokiamua washauri wa mahakama na uamuzi alioutoa Jaji na sababu za uamuzi huo Jumamosi.

Summar

Advertisement