Ufugaji wa Kuku una fursa tele

Saturday December 22 2018

 

By Clement Fumbuka

Wanufaika wa ufugaji ni watu wote wasiofuga na wanaofuga. Ufugaji wa kuku unatupeleka kupata mayai na nyama ya kuku, huku ufugaji wa mifugo wengine hutupeleka kupata nyama na maziwa. Haya ndiyo mazao tunayotarajia kuyaona katika ufugaji.

Swali la kujiuliza; je, unafahamu mahitaji yako ya mayai, nyama na maziwa katika lishe kitaalamu? Bila shaka ni swali ambalo umewahi ama hujawahi kulifikiria lakini takwimu zinaonyesha wastani wa kula mayai, nyama na maziwa kwa mtu mzima kwa mwaka kuwa uko chini.

Utafiti uliofanywa na shirika na chakula duniani (FAO,2011): ulaji wa mayai kwa mtu mmoja kwa mwaka ni wastani wa mayai 106 tu huku ikiwa idadi inayotakiwa kuliwa na mtu mzima kwa mwaka ni mayai 300.

Wastani wa nyama inayoliwa na mtu mzima kwa mwaka ni kilo 15 tu huku kiasi kinachotakiwa kuliwa ni kilo 50 kwa mwaka. Na wastani wa lita 47 za maziwa pekee hutumiwa na mtu mzima kwa mwaka badala ya lita 200 kwa mwaka.

Ikumbukwe kuwa Tanzania ni moja kati ya nchi tatu maarufu kwa kuwa na mifugo wengi barani Afrika. Mhadhiri wa chuo kikuu cha kilimo Sokoine, Profesa Faustine Lekule katika jarida lake la “Demand and Supply of Animal Feeds in Tanzania, 2017/18”, ameonyesha tuna ng’ombe milioni 30.5, mbuzi milioni 18.8, kondoo milioni 5.3, kuku wa kienyeji milioni 38.2, kuku wa kisasa milioni 36.6, nguruwe milioni 1.9 na punda 595,160.

Pia ameonyesha uzalishaji wa maziwa kwa mwaka 2017/18 ni lita bilioni 2.4, nyama tani 679,992 na mayai bilioni 3.16, huku uzalishaji wa nyama ya kuku ukiongezeka kwa asilimia moja ya jumla ya nyama inayopatika kutoka kwa mifugo wote.

 Kuku wa kisasa wanaongezeka kwa kasi ikilinganishwa na hapo awali. Hii ni kutokana na ongezeko la watu kusababisha kuwa na uhitaji mkubwa wa nyama ya kuku na mayai ambao kuku wa kienyeji wanazidi kuelemewa kila kukicha.

 Hali hii imehamasisha sana ufugaji wa kuku wa kisasa na kuwa mwarobaini wa kupunguza gharama ya kupata nyama kwa walaji. Zaidi ya asilimia 80 ya watu waishio mijini wanategemea kuku wa kisasa kwa mayai na nyama. 

 

 

Fursa kwa Watanzania

Upungufu wa mazao ya mifugo kulingana na mahitaji ya watu kama ilivyoainishwa na FAO, bado ni mkubwa, kwani hali inayosababisha ulaji wa mayai, nyama na maziwa kuwa chini ni pamoja na uhaba wa bidhaa hiyo kwenye jamii, kitendo kinachosababisha kupanda bei kuliko uwezo wa watu wa chini kununua.

Vile vile gharama za ufugaji kuwa juu ni sababu tosha kwa wafugaji kulazimika kuitafuta faida kwa kuuza bei ya juu mazao ya mifugo.

Naungana na  Profesa Lekule kwamba; zaidi ya asilimia 90 ya vyakula vya mifugo ambavyo hutengenezwa viwandani hutumika kulisha kuku. Ili kujenga msingi bora wa ufugaji wa kuku na wanyama wengine, ni bora kuhamasisha uzalishaji wa mazao ya nafaka na jamii ya mikunde kama vile mahindi na soya ambayo ndiyo chakula kikuu cha wanyama.

 Mifugo kama kuku ina unafuu mkubwa kwa wafugaji kuifuga ikilinganishwa na mifugo mingine. Kwa walaji pia kuku ni nafuu kupatikana ikilinganishwa na aina nyingine ya  mifugo  ambao si rafiki  kuwepo katika baadhi ya maeneo. 

Uhamasishaji wa ufugaji na ulaji wa mazao ya mifugo lazima uendane na upatikanaji wa malisho ya mifugo kwa gharama nafuu na kuuza mazao yao kwa bei nafuu. Badala ya kutumia dagaa kwenye mchanganyiko wa chakula, ipo fursa ya kutumia soya kwenye protini ya wanyama na kuacha dagaa itumike kwa lishe ya binadamu pekee.

Advertisement