Unajua kama kukojoa kitandani ni ugonjwa wa akili?

Friday May 10 2019

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Kuna usemi usemao, “mchawi mpe mwanao alee,” ambao umewasaidia wengi kisaikolojia kuachana na tatizo la kukojoa kitandani kutokana na kuwatumia wanaochukia tabia hiyo kuikomesha.

Katika familia nyingi kuna watu wenye tatizo la kukojoa kitandani wanapokuwa wamelala, iwe watoto au watu wazima.

Hata hivyo, siyo kwamba wanaokojoa kitandani wanapenda! La hasha, bali ni tatizo walilonalo na hawajui namna ya kulikabili.

“Wifi yangu ilishindikana kumpeleka shule ya bweni alipokuwa kidato cha kwanza kwa sababu alikuwa anakojoa kitandani akilala. Hali hii ilinipa shida na kunitatiza kwa sababu ilimnyima raha yeye na familia nzima, lakini alishindwa kuacha na alishakata tamaa,” anasimulia Bahati Alfonce aliyebuni mbinu ya kumuachisha wifi yake kukojoa kitandani.

Anasema baada ya muda akapata wazo la kumtumia binti yake aliyekuwa shule ya awali kumsaidia shangazi yake kuacha tabia hiyo.

“Kila wifi yangu alipokojoa kitandani awapo usingizini, nilikuwa nampiga binti yangu aliyekuwa na miaka mitano na wifi yangu akiwa kidato cha kwanza,” anasema Alfonce.

Anasema hakufurahishwa na kitendo kile, lakini alijaribu kumsaidia wifi yake, hivyo alipokuwa akimchapa binti yake, wifi yake alikuwa anaumia na hata kushindwa kula.

“Nikawa namwambia ukitaka niache kumpiga aache kukojoa, binti yangu nikampa jukumu la kumuamsha shangazi yake usiku ili akajisaidie.

“Niliwapa hii ‘dawa’ kwa muda wa miezi mitatu, siku moja binti yangu aliamka na furaha akinikumbatia na kusema mama leo shangazi ameniamsha nikajisaidie (baada ya shangazi yake kuacha kukojoa, akamwamsha binti huyo ili naye asikojoe).”

Alfonce anasema ilimchukua kama miezi miwili ya ziada wifi yake kuacha kabisa kukojoa kitandani, baada ya kufanya hivyo mara moja moja.

Mbali na dawa mbadala ya Alfonce, mwingine aliyempa mchawi kulea mwanaye ni Rukia Mharizo ambaye aliwalaza kitanda kimoja watoto watatu.

Anasema kila siku watoto wake wa kiume wawili waliwakuwa wanamcheka mdogo wao mwenye miaka minne aliyekuwa akikojoa kitandani.

“Nilipogundua kuwa wanapomzomea anaumia, nikawaambia wawe wanamwamsha usiku ajisaidie, lakini hawakufanya hivyo.

“Nikanunua godoro la futi sita kwa sita na nikatoa kitanda chumbani mwao, nikaliweka chini na kuanzia hapo wakawa wanalala wote na mdogo wao akikojoa hakuna kuhama,” anasema Mharizo.

Pia, anasema kila mmoja alipokuwa akikumbuka kulala kwenye mikojo ya mdogo wao anakurupuka na kumuamsha akajisaidie, licha ya kufanya hivyo kwa hasira hadi wakawa wanafanya kwa mapenzi.

“Nikikaa, nasikia wanapongezana jana nilimbeba hadi kwenye poti akajisaidie maana nilivyomuamsha aligoma kabisa,” anasema Mharizo.

Anafafanua walivyoanza kufanya hivyo akajua somo limewakolea na inaweza kuwa dawa, “kweli nilifanikiwa aliacha baada ya muda, haikuwa rahisi lakini ilizaa matunda, ingawa shughuli ya kumuamsha usiku iliendelea hadi alipofikisha miaka sita.

Mharizo anashauri badala ya kuwabeza na kuwatembeza mitaani watoto kisa wamekojoa kitandani, zipo njia za kuwasaidia katika ngazi ya mwanzo.

“Kuwatembeza, kuwabeza, kuwacheka kunaweza kuwaathiri kisaikolojia na kuzalisha tatizo lingine, hivyo kama familia ni muhimu kushirikiana kutatua changamoto hiyo ikiwamo kuangalia afya ya watoto na kuwazoesha kujisaidia kabla ya kulala tangu wakiwa wadogo,” anasema Mharizo.

Mkurugenzi wa Fedha na Utawala kutoka Bodi ya Ununuzi na Ugavi nchini (PSPTB), Paul Bilabaye anasema wazazi wengi huwaandaa watoto wao kuwa vikojozi bila kujua.

Akizungumza na wafanyakazi wa Mwananchi Communications Limited (MCL) kwenye semina maalumu, anasema watoto kuendelea kukojoa kitandani hata baada ya kukua ni matokeo ya kuandaliwa tangu wakiwa wadogo.

Anasema kulingana na maisha ya sasa, watoto wengi hususani kutoka kwenye familia zenye nafuu ya maisha, huvalishwa nepi (pampers) maalumu kuzuia mkojo, zikichafuka hutupwa.

“Wengi wao huvalishwa hata baada ya kutimiza umri zaidi ya mwaka mmoja, wakionekana wamekuwa na kulala bila kuvalishwa, huendelea kukojoa kitandani.

“Tofauti na kinamama wa zamani waliowapanga watoto wao kwa ajili ya kujisaidia haja ndogo kila mara, kina mama wa sasa huwavalisha pampers ili kuepuka usumbufu wa kuamka mara kwa mata usiku na madhara yake ndiyo hayo.” Pia, anasema kuwachapa watoto kwa kosa la kukojoa kitandani ni kuwaonea.

Mtaalamu azungumza

Daktari bingwa wa magonjwa ya akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya Akili Mirembe, Damas Andrea anasema ugonjwa wa kujikojolea una sababu nyingi kama kisukari, maambukizi (Infection) katika njia ya mkojo, magonjwa mbalimbali ya kibofu cha mkojo na sababu za kisaikolojia.

Anasema kujikojolea inakuwa ugonjwa wa akili pale unaposababishwa na sababu za kisaikolojia na kuathiri utendaji kazi, uhusiano na watu wengine pamoja na kumwathiri mtu kimasomo.

Mtaalamu huyo wa afya, anasema wapo wagonjwa wenye ugonjwa wa kujikojolea, wanafanya hivyo mchana, usiku tu na wengine usiku na mchana.

“Pia, wapo wagonjwa ambao hawajawahi kuacha kujikojolea (kukojoa kitandani)tangu wazaliwe na wengine waliacha kisha wakaanza kukojoa tena. Tatizo hilo pia linakuwa ugonjwa mtu mwenye umri wa miaka mitano au zaidi anapojikojolea angalau mara mbili au zaidi kwa wiki kwa kipindi cha miezi mitatu mfululizo , ” anasema Dk Andrea.

Pia, anasema ugonjwa huo unaathiri asilimia 5 hadi 10 ya watoto wenye umri wa miaka mitano, asilimia 3 hadi 5 ya watoto wenye umri wa miaka kumi na asilimia moja ya watu wenye umri wa miaka 15 au zaidi.

“Ugonjwa wa akili wa kujikojolea hausababishwi na sababu moja ila muunganiko wa sababu za kibaiolojia, kisaikolojia na kijamii,” anasema.

Anazitaja sababu zinazoweza kuongeza uwezekano wa mtu kupata ugonjwa wa akili wa kujikojolea ( Enuresis) ni pamoja na kuchelewa kumfundisha mtoto kutumia choo, mafundisho legevu ya kutumia choo au kutumia ukali uliopitiliza wakati wa kumfundisha mtoto namna ya kutumia choo.

“Wapo watu wanaoweza kurithi vinasaba vya ugonjwa wa kujikojolea kwa wazazi wao,” anasema Dk Andrea.

Anaeleza kuwa matatizo au misukosuko mbalimbali wakati wa utoto unyanyasaji wa watoto, kufanyiwa unyama kama kubakwa, kutenganishwa na wazazi pia huchangia uwezekano wa kupata ugonjwa huo.

Matibabu

Dk Andrea anasema ugonjwa huo unatibika kulingana na chanzo na maendeleo yake.

“Ugonjwa wa kujikojolea unatibika. Ni vizuri mtu mwenye ugonjwa huo kuwaona wataalamu wa afya hasa wataalamu wa magonjwa ya akili ili aweze kupata tiba stahiki,” anashauri Dk Andrea.

Pia, anasema kuwapigia kelele, kuwazonga ni kuwaongezea tatizo badala yake itafutwe kwanza sababu ya wao kufanya hivyo ikiwa ni pamoja na kushauriana na wataalamu wa afya.

Kwa mujibu wa mtandao wa Kidneyeducation.com unaojiusisha na masuala ya kutoa ushauri wa kitabibu, suala la watoto kukojoa kitandani ni la kawaida na huisha bila dawa kadri mtoto anavyokua.

“Hali hii huzidishwa na usumbufu wa akili au wa kiafya,” inaeleza taarifa ya jarida hilo la mtandaoni.

Madaktari wanaotayarisha jarida hilo wanashauri watoto kufanyiwa vipimo vya kawaida kwa wanaohisiwa kuwa na tatizo la kiafya au za kimaumbile zinazosababisha kujikojolea ikiwamo sukari, figo, mgongo, kibofu kwa kutumia utrasound na picha nyingine ili kuona kibofu na figo.

Advertisement