Unajua mastaa wanapozipeleka nguo baada ya kuzivaa kwenye ‘Red Carpet’?

Saturday January 12 2019
pic mastaa

Ni jambo la kawaida kwenda kwenye shughuli mbalimbali hususani zile zinazohusu matukio ya mastaa na kukuta kuna zulia jekundu.

Mazulia hayo ambayo kwa sasa wengine wamekuwa wakiyaweka ya rangi tofauti kama nyeusi, nyeupe, kijani na nyinginezo ambazo waandaaji wanapendelea wengi hupenda kupigia picha.

Eneo hilo pia utawakuta wapiga picha wakiwa tayari wakati wote wakiwasubiri wanaotaka kupata kumbukumbu na wakati mwingine wanapoona pembeni kuna mtu amependeza, lakini hataki kupiga picha humshawishi apige picha.

Huwa ni wale wanaotaka kwa ajili ya kupambia magazeti yao katika kurasa zinazohusu mavazi, wale wanaotaka kuzihifadhi kwa ajili ya kuzitumia katika masuala ya kihabari kwenye mitandao ya kijamii na wengine kwa ajili kuziuza.

Kwa waandishi wa habari hapa ndipo hasa wanapenda kuweka kambi ili kujua nyota gani ‘amevunja kabati’ kwa siku hiyo na wakati mwingine ndipo wanapopata nafasi ya kufanya mahojiano.

Pamoja na kuwepo na mavazi ya kila aina, yakiwemo yale ambayo mtu hawezi kuyavaa mchana na kupita barabarani, je ulishawahi kujiuliza ni wapi mastaa hao huyapeleka baada ya matukio wanayohudhuria kwisha? Hilo ndilo swali ambalo watu wengi huwa wanajiuliza. Hata hivyo baadhi ya mastaa wamefunguka mahali wanakopeleka mavazi hayo baada ya kuyavaa kwenye hafla mbalimbali.

Advertisement

Zamaradi Mketema

Akiwa mtangazaji maarufu aliyewavutia wasichana wengi kuingia katika fani hiyo, anasema swali hilo ameulizwa wakati mzuri wakati naye alikuwa akiumiza kichwa kuja na kitu ambacho kitafanya mavazi hayo yaendelee kuvaliwa ambapo anawaza kuanzisha gulio kwa ajili ya nguo hizo tu. “Wazo likanijia kuwa majibu ni kwamba wengi hawapendi kuonekana nayo tena (mavazi) mbele za watu, japokuwa kuna watu huwa wanapenda mavazi hayo yanayotupiwa na mastaa, lakini wasijue namna gani wanaweza kuyapata,” anasema.

“Kuna watu pia wamekuwa wakijaribu kushona mishono inayofanana na wao, lakini kutokana na gharama (kubwa) wanazotumia mastaa kushona nguo hizi, mafundi wa kawaida huwa zinawashinda na mhusika kutotimiza lengo alilokusudia.”

Anasema, “Ndipo nilipopata wazo kwa nini nisianzishe gulio la kuuza nguo hizo hata kwa kupitia mitandao ya kijamii kwa kuweka picha ya staa husika na nguo aliyovaa na kuweka bei iwapo kuna anayetaka kuinunua kama wanavyofanya kwenye minada.”

Anasema jambo hilo halitawasaidia wanaotaka kuvaa nguo za mastaa tu, bali hata mastaa wenyewe watafaidika na nguo zao ambapo fedha watakazopata watakwenda kufanyia shughuli nyingine za maendeleo tofauti na sasa ambapo wanakuwa hawana kazi nazo na hawawezi kuzivaa tena.

Anasema hata yeye hupata wakati mgumu kurudia nguo aliyoivaa kwenye hafla, hivyo atapata nafasi nzuri ya kurudisha angalau kiasi kidogo cha gharama anazotumia.

Rose Ndauka

Rose Ndauka, msanii maarufu wa filamu, anasema akishavaa nguo na kupita nayo kwenye zulia jekundu huwa hairudii tena. Badala yake anasema amekuwa akiziweka ndani kama kumbukumbu na wakati mwingine huigawa kwa ndugu, jamaa au marafiki.

“Unajua mimi ni staa kila ninapoonekana mbele za watu natakiwa niwe na kitu kipya ikiwamo nguo, viatu, nywele na wakati mwingine hata mapambo ya uso, hivyo ni ngumu kurudia nguo na ndiyo maana naamua tu niigawe,” anasema Rose aliyewahi kutesa ni filamu kama Bad Girl, The Diary, Swahiba, Deception na Lost Adam.

Lady Jay Dee

Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Judith Wambura ‘Lady Jay Dee’, anasema pamoja na kutorudia nguo aliyovaa kwenye zulia nyekundu, haoni sababu ya kuuziuza.

Anasema huwa anaziweka kama kumbukumbu kwa sababu hadi anazinunua na kuona zinafaa kuvaliwa mbele za watu alizipenda, vivyo hivyo anapenda kuendelea kuziona.

“Jamani mtambue na sisi tuna maisha yetu nje ya usanii, kwa nini niuze nguo niliyoinunua kwa fedha zangu kisa tu sitaki kurudia kuivaa, hapana. Kuliko kufanya hivyo bora niiweke ndani,” anasema Lady Jay Dee mwenye majina mengi likiwemo Komando, Binti Machozi na Anaconda.

“Mbali na sababu hizo, nina uwezo wa kuivaa kwenye mtoko mwingine bila shida, inauma kutupa au kugawa kitu kwa sababu tu wewe huwezi kukitumia, kama nataka kumpa mtu nguo nitainunua kwa ajili yake badala ya kumpa niliyoshindwa kuivaa.”

Juliana Kanyomozi

Juliana Kanyomozi, msanii kutokana Uganda, anasema haoni tabu kurudia kuvaa nguo ambayo alipita nayo kwenye zulia jekundu.

Msanii huyu aliyewahi kufanya ‘kolabo’ na Ruta Bushoke ‘Bushoke’ katika wimbo wa Usiende mbali anasema haoni aibu kurudia nguo.

“Siiuzi, siigawi naivaa kadri siku zinavyokwenda, ninachofanya kila inapotokea hafla kubwa ya burudani nitavaa nguo nyingine kulingana na hafla husika, hiyo haimaanishi nguo ya zamani naachana nayo,”anasema.

Kanyomozi aliyewahi kutamba na wimbo wa Kanyimbe, anasema kwa kawaida hawezi kukaa na nguo za miaka yote na huwa unafika wakati lazima aziondoe.

Maua Sama

Maua sama, nyota wa kibao cha Iokote, anasema hugawa nguo kama akiiona ni ya kawaida, lakini zile alizozipenda huzivaa kwenye shoo za mikoani au nchi nyingine tofauti na mkoa alikozivaa mara ya kwanza.

Jacqueline Wolper

Jacqueline Wolper anasema kutokana na kuwa kioo cha jamii na mbunifu wa mavazi, nguo anazovaa kwenye zulia jekundu huzigawa kwa marafiki au wanahitaji.

“Sioni haja ya kuziweka ndani ilhali sina mpango wa kurudia tena kuzivaa, hivyo nazigawa na wapo wengi wenye mahitaji ya nguo kuliko watu wanavyofikiria,” anasema.

Vanessa Mdee

Vanessa Mdee maarufu kama Vee Money, anasema kutokana na kuwa na nguo nyingi alizowahi kuvaa kwenye zulia jekundu au shughuli mbalimbali hana mpango wa kuzivaa tena, lakini ana wazo la kuanzisha makumbusho ya kuziweka.

Anasema kwa kuanzia anazo zaidi ya 140 hivyo hata leo akiamua kufungua hilo jumba la makumbusho litakuwa na nguo za kutosha.

Nandy

Faustina Charles maarufu kama Nandy, anasema nguo zake za zulia jekundu au anazopanda nazo jukwaani huzipeleka katika duka lake la kushona nguo lililopo Tabata.

“Wapo watakaopenda (nguo) kama niliyovaa na wapo watakaotaka kumjua aliyenibunia ili na wao wakapeleke mawazo yao watayarishiwe kulingana na matakwa yao. ”

Advertisement