Wema Sepetu amepunguza kilo 26 ndani ya miezi mitatu

Saturday February 9 2019

 

Umekutana na Wema Sepetu hivi karibuni? Utamshangaa. Ndani ya miezi mitatu amepungua kilo 26! Kwa kuwa wanawake siku hizi wanapenda kupungua, wakimuona wanamfurahia ila bibi kule kijijini huenda atashtuka vipi tena mwili umepukutika.

Lakini si kweli kwamba watu wote wanafurahia namna Miss Tanzania huyo wa 2006 alivyopungua, hata meneja wake, Neema Ndepanya anasema hapana. ‘Wema nenepa kidogo’.

Katika mahojiano yake na Mwananchi, Ndepaya anasema kutokana na hilo ameanza kumshauri ale walau arudishe mwili kidogo kwani amekonda sana mpaka havutii.

Alisema kwa namna anakoelekea sasa nafasi nyingi katika filamu huenda zikamshinda kucheza kutokana na muonekano wa mwili wake.

“Kiukweli Wema kwa alikuwa anapendezea kucheza nafasi ya mama mwenye nyumba, bosi flani na nafasi nyingine lakini muonekano wake wa sasa unaweza ukamnyima hiyo nafasi.

“Kwani watu wanapaswa kuelewa kuwa katika nafasi za uigizaji hatumuweki tu mtu hivihivi ni lazima aendane na nafasi husika hivyo alipofikia Wema anaenda kwenye uanafunzi,” anasema Neema.

Hata hivyo amekanusha taarifa kwamba kukonda kwake kumetokana na kukatwa utumbo.

Alibainisha kuwa amekuwa akifanya mazoezi kwa takribani miezi sita ambayo yamemuwezesha kupungua kutoka kilo 96 hadi kufika kilo 70.

Advertisement