Wimbi la mimea inayobatilishwa kwa GMO

Sunday June 10 2018Freddy Macha

Freddy Macha 

Miaka sitini (hadi 100) iliyopita- sigara, ilivutia sana.

Sinema na TV zilionyesha waigizaji wakiivuta mithili ya starehe ya hali ya juu sana. Nikiwa kijana tuliambiwa mwanamke alipovuta sigara kisha akampulizia mwanaume moshi usoni ni ishara ya kum-enzi, kumhitaji, kumtaka.

Sigara haikuonekana ni dhara. Ila saratani ilipounganishwa na sigara makampuni ya tumbaku yalichachamaa. Mvutano huu wa kibiashara ulichukua muda mrefu kupingika hata mauaji na rushwa vilipita.

Vitisho, ufisadi, mabavu

Hapa Ulaya matangazo ya biashara –kuhusu pombe na sigara- redioni na TV yalianza kuzuiwa kama miaka 30 iliyopita. Leo ni kawaida kabisa kutoona matangazo hayo. Karibuni sigara zimepigwa marufuku ndani ya majumba ya hadhara na vyombo vya usafiri. Paketi za sigara zinatakiwa kisheria kuonyesha uharibifu wake kiafya – kwa picha zenye mapafu au viungo vilivyovimba, kuoza na kusinyaa.

Karibuni madhara ya simu za mikononi yameongelewa. Ila kwa kuwa utafiti haujafanywa vya kutosha, bado mada i jikoni.

Halafu, sasa kuna GMO

Neno hili ni geni-si tu Afrika, hata kwa Waafrika tunaoishi Uzunguni. Hatari na maana havifahamiki kwa wengi.

GMO ni kifupi cha “Genetically Modified Organisms.” Kama hukuwahi kusikia, tafadhali baada ya kusoma safu hii ingia mitandaoni fanya utafiti zaidi.

Genetic imetokana na “gene”- kifupi cha DNA-tafsiri ya kamusi ni tabia, umbile, nasaba, ukoo, kizazi cha kiumbe hai. Mfano mzuri ni pale askari anapochukua alama ya kidole cha mhalifu. Kila mtu ana alama au mistari asilia tofauti. DNA au “gene” (tamka “jinn”), ni msingi unaomtofautisha kila mnyama, mwanadamu au mmea. “Modify” ni kubatilisha.

Sayansi ya GMO iligunduliwa kujaribu kupambana na adha za kiafya. Njia mosi ilitengeneza vidonge vilivyopigana na magonjwa Bab-Kubwa. Ya pili iliingilia sasa mimea. Chukua mfano wa magugu au virusi haribifu shambani.

Dawa zilizotumika kupambana na bakteria ziliposhindikana, wanasayansi waliingia maabarani na kuunda chembe hai (hizo ‘genes’ tulizozisema juu) na kuzipachika na mbegu bora za mimea mingine. Mbegu mpya zilitumiwa sasa kuchapana na magugu. Sayansi hii imetumika kuunda wanyama bomba (super) mfano kumwekea kondoo mbegu za mbuzi nk. Kiumbe anayezaliwa atakuwa na nguvu kuliko wenzake asilia.

Leo GMO ni biashara bomba

Wakulima wa mazao na mifugo ya kibiashara wanaihodhi taaluma kubatili mimea kutengeneza mazao bora zaidi. Mathalan, ukiona matunda na mboga kubwa zaidi, zilizofanana na kupendeza kitaswira, zimebatilishwa ZIUZIKE.

Huku Ulaya ukiingia baadhi ya masoko bomba utashangaa namna nyanya mathalan zinavyokuwa kubwa rangi nyekunduuuu. NI kawaida kuona matunda na mimea isiyokuwa na mbegu. Hapo ndipo lilipo somo. Mungu kaumba mimea na mbegu vipi hizi hazina mbegu?

Afya za wanadamu kidogo zimeanza kuathirika. Wanaume na wanawake wanashindwa kuzaa, kutokana na mayai yao kuwa tasa. Unene usiojulikana unachapuka, nk. Ingawa GMO imeyafaidisha makampuni makubwa, kibiashara; afya zetu hazijatafitiwa sawasawa. Na ndiyo maana umezuka upinzani mkali wa bidhaa za GMO. Hapa Ulaya mapapai kutoka Hawaii ambayo ni GMO mfano hayaruhusiwi. Unga wa mahindi ( kwa ugali Afrika Kusini) unatumia GMO.

Tuendelee na mada hii muhimu wiki ijayo.

Advertisement