Women Jazz Band bendi iliyokuwa na wanamuziki wanawake katika idara zote

Saturday March 9 2019

 

By Anko Kitime

Jana ilikuwa ni siku ya wanawake duniani, nimefikiria itakuwa vizuri kuongelea historia moja ya akinamama wa hapa nchini ambayo bila kufanya makusudi itapotea kama zinavyopotea historia nyingi za ushujaa za nchi hii.

Historia hii inaanzia pale Rais wa Guinea ya Conakry, Sekou Toure alipotembelea Tanzania 1965. Rais huyu alipenda sana utamaduni wa nchi yake na kama ilivyokuwa kwa Mobutu alisisitiza kurudia uasili katika shughuli za utamaduni na akaufadhili kwa hali na mali.

Alianzisha vikundi vya sanaa vya mikoa na kutokana na vikundi hivyo alitengeneza vikundi vya Taifa. Mfano mzuri sana ambao wapenzi wa muziki wa dansi wa zamani watakumbuka ni Bembeya Jazz, bendi iliyopiga wimbo maarufu wa Whisky Soda, hii ilikuwa ni bendi ya mkoani lakini ikashinda mashindano na kuhamishiwa mkao makuu ya nchi na kufanywa bendi ya Taifa.

Bendi hii iliyoanzishwa 1961 bado iko hai na inafanya maonyesho Guinea na nje ya nchi hiyo, inawezekana ndio bendi kongwe Afrika ambayo iko hai.

Mwaka 1961 pia ilianzishwa bendi ya muziki ya polisi wanawake hukohuko Guinee bendi iliyoitwa L’Orchestre Feminin De La Gendarmerie De Guinee, na wakati wa Sekou Toure ikapewa jina la Les Amazones De Guinee na kuwa na wadhifa wa Kitaifa.

Wakati wa misafara yake Rais Sekou Toure alisindikizwa na vikundi vya sanaa, na alipokuja Tanzania ndege yake ilikuwa na wasanii wengi kuliko wanasiasa, katika msafara huo alikuja na bendi hiyo ya kina mama Les Amazones.

Baadhi ya mabinti wa TANU Youth League hapa nyumbani ndio walikuwa wenyeji wa wanamuziki hawa wa kike. Rais Sekou Toure na wasanii wake walipoondoka walikuwa wamepanda wazo la vikundi vya sanaa vya Taifa na pia wazo la bendi ya wanawake.

Wale mabinti waliokuwa wakizunguka na wanamuziki, wengi wakiwa wanafanya kazi Government Press waliazimia nao kuanzisha bendi ya wanawake, japo walikuwa hawana ujuzi wa chombo chochote cha muziki, lakini nia yao ilikuwa kuwa na bendi kama Les Amazones.

Chini ya ufadhili wa TANU Youtha League akina mama hawa wakaanza kuhudhuria mafunzo ya muziki, pale Police Mgulani chini ya mwanamuziki mahiri wa Polisi Mzee Mayagilo, baadaye wakawekwa chini ya kitengo cha Polisi Jazz Band, ambako huko wakamkuta marehemu Mzee Kassim Mapili nae akawa mwalimu wao mkuu.

Hayawi hayawi yakawa hatimae Mei 31, 1966, bendi ya kwanza ya wanawake Tanzania, ikaingia katika studio za Redio Tanzania Dar es Salaam na kurekodi nyimbo, wakiwa wanapiga na kuimba nyimbo walizotunga wao wenyewe.

Nyimbo hizo zilikuwa ni Tumsifu mheshimiwa, Leo tuna furaha, Mwalimu kasema, Women Jazz, Sifa nyingi tuwasifu viongozi na TANU yajenga nchi. Kundi zima lililoingia studio lilikuwa na wanamuziki kumi na tano.

Baada ya hapo bendi ilianza kupata umaarufu mkubwa watu wakishangaa kuona kundi la wanawake wakiporomosha dansi bila sura ya mwanaume, bendi ikaanza kufanya maonyesho kwenye hafla mbalimbali za serikali na chama, na pia kuanza kuzunguka mikoa mbalimbali wakifanya maonyesho yaliyokuwa yakijaza kumbi.

Sifa zikavuka mipaka na wakajikuta wakipiga na kujaza watu kwenye kumbi mbalimbali Nairobi na Mombasa. Kutokana na urafiki uliokuwepo wakati huo kati ya Tanzania na China, ikafikia hatua ya bendi hii kuonekana ni muhimu kwenda kufanya ziara China, lakini wakati wa matayarisho ya safari hiyo, bendi ikasambaratika. Kilichofanya bendi isambaratike ilikuwa ni kudhurumiwa mapato.

Akinamama hawa walikuwa wakifanya maonyesho na yalikuwa yakiingiza fedha, lakini walikuwa hawapati chochote kutokana na maonyesho yao zaidi ya umaarufu.

Ni bahati mbaya majina ya waliokuwa wakitumbua fedha za bendi hii bila kuwagawiya wanamuziki hawa kipato chao halali, ni wanaume wenye majina maarufu katika historia ya siasa za nchi yetu.

Kufikia hatua hiyo wanamuziki hawa wakaona ni heri kurudia kazi yao ya awali Government Press kuliko umaarufu uliokosa fedha, jambo ambalo lilianza kuwaletea matatizo katika familia zao bila kuwa na sababu za msingi bendi ikasambaratika.

TANU youth League ikachukua vyombo vyake na kuvihifadhi, hatimae vyombo hivi vikawa ndivyo vyombo vilivyotumika kuanzisha Vijana Jazz band chini ya Mzee John Ondolo miaka kadhaa baadae.

Karibu akina mama wote wa bendi hii kwa sasa ni marehemu Mungu awalaze pema, lakini hakika walio hai wanastahili kupewa tuzo katika maazimisho ya siku za akinamama.

Advertisement