Vijue vigezo vya kutafuta ajira ya ndoto zako

Unatafuta kazi ya ndoto zako? Una ajira lakini bado unahisi haikutoshelezi? Jifunze mbinu tatu muhimu unapotafuta kazi uipendayo.

Wengi wetu tunakumbuka ndoto tulizowahi kuwa nazo tukiwa watoto. Enzi hizo tulisimuliana matamanio yetu ya kitu gani hasa tungependa kukifanya tukiwa wakubwa.

Ingawa wapo ambao kwa sababu moja au nyingine, mfumo wa elimu ulizima ndoto zao mapema, lakini kuna wachache waliofanikiwa kusoma fani zinazoendana na ndoto walizokuwa nazo.

Hata hivyo, ukiwauliza hawa waliobahatika kusomea mambo waliyotamani wakiwa wadogo, miongoni mwao watakwambia hawafurahii kile wanachokifanya leo. Sababu zinaweza kuwa nyingi.

Kwanza, wakati mwingine watu hulazimika kusoma na kufanya kazi zisizoendana na ndoto zao kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao. Vijana wengi, kwa kukosa uwezo wa kiuchumi hulazimika kusoma fani zinazowahakikishia mikopo.

Lakini, tunafahamu ndoto nyingi za utoto huwa hazina uhalisia. Mara nyingi ndoto hizo hujengwa katika matamanio ya kufanya kazi zinazosifika zaidi katika jamii maarufu, lakini baadaye tunapozifanya tunaweza kugundua tuliiga ndoto zisizo zetu.

Ndoto isiyoanzia ndani ya mtu haidumu, mara nyingi hufa. Utafanya kazi muda mfupi, lakini unashangaa unaanza kukosa utoshelevu. Mazingira yanakutengenezea ndoto mpya inayofubaza ndoto uliyokuwanayo awali.

Katika makala haya, ningependa kukusaidia kuelewa vigezo muhimu vya kujitathimini unapotafuta kazi ya ndoto yako.

Una suluhisho la tatizo gani?

Kila ndoto hubeba suluhisho fulani katika maisha ya watu. Hapa tunazungumzia namna gani una uwezo na ujuzi wa kuona na kuleta suluhisho la changamoto zinazowakabili watu. Inaweza kuwa kuzorota kwa afya za watu, migogoro katika jamii, umaskini, ustawi wa jamii, huduma na mahitaji mengine waliyonayo watu. Unapotafuta ajira, lazima kujua kwa hakika unataka kutatua tatizo gani linalowakabili watu wanaokuzunguka.

Nafahamu wakati mwingine tunalazimika kutafuta ajira zinazoendana na sifa za kitaaluma tulizonazo.

Hatusumbuki kujua tunafumbua tatizo gani katika jamii. Athari yake, hata hivyo, ni kujikuta tunagundua kile tulichofikiri ni cha maana, hakina umaana ule ule wa awali. Matokeo yake tunachoka kazi na kupoteza msisimuko.

Pia, tulitangulia kugusia awali, si mara zote watu husomea fani zenye mizizi inayoanzia ndani yao. Lakini yale tunayoyaona wakiyafanya yanaweza kutujengea matamanio yanayoanzia nje.

Katika mazingira haya, ni vizuri ‘kuchukua’ ajira yoyote unayoipata kama mwanzo wa safari ya kukufikisha kule unakotaka kwenda. Safari huanza na hatua moja. Muhimu ni kutokata tamaa na kujitahidi kuendelea kujiongezea thamani ukiwa kazini.

Umebeba thamani ipi?

Thamani ni ule uwezo wa kipekee, aghalabu maarifa, uzoefu na ujuzi, ulionao unaokusaidia kutatua matatizo yanayowakabili watu. Thamani hii ndiyo inayomvutia mwajiri makini kwa sababu atapata tija akikuajiri.

Unapotafuta ajira lazima ujiulize, umebeba thamani gani? Kwa nini mwajiri akuajiri? Una nini cha ziada?

Watu wengi, kwa kufikiri thamani yao inaamuliwa na cheti, hukosa ubunifu wa kujieleza wanapoomba ajira ya ndoto zao.

Badala ya kutumia mifano inayoonyesha uwezo wao wa kuleta tofauti kwenye kampuni, wanaishia kutaja kiwango cha elimu na maelezo ya majukumu waliyowahi kuyafanya katika ajira zao za zamani.

Hiyo ni mojawapo ya sababu za watu wengi kukosa fursa ambazo, kama wangekuwa wabunifu kidogo, wangezipata.

Pia, fahamu kuwa huwezi kusonga mbele bila kujenga thamani yako. Hata kama unafanya kazi usiyoipenda, jiulize, kwa mfano, unafanya kipi cha ziada baada ya majukumu uliyopewa?

Unajitofautishaje na wafanyakazi wengine? Thamani unayoionyesha kwenye ajira isiyo ya ndoto zako ndiyo inayoweza kuwa daraja lako la kukuvusha kuelekea kwenye ajira ya ndoto zako.

Unaposhindwa kuonyesha thamani kwenye ajira uliyonayo, usitegemee ajira uipendayo itakuja kwa muujiza.

Unautumiaje mtaji jamii?

Watu ni mtaji muhimu katika safari yako ya kufikia ndoto zako. Aina ya watu unaofahamiana nao inaweza kuamua wapi unaweza kufika. Jifunze kutumia vizuri mtaji huu.

Katika kujenga mtaji wako wa watu, fahamu kuwa watu, kwa kawaida, wanapenda kuhusiana na watu wenye thamani fulani.

Jitahidi kuuza thamani uliyonayo. Hapa nina maana ya kuhakikisha kuwa watu wanafahamu unaweza kufanya nini.

Unafanyaje sasa?

Tumia kila fursa inayojitokeza kuonyesha ujuzi ulionao. Tunayo mitandao ya kijamii, kwa mfano, unaitumiaje? Unaandika nini kwenye mtandao wa Twitter, Instagram?

Huko ndiko watu wanakoweza kukufahamu hata kama hujawahi kuonana nao. Jenga wasifu wako kupitia taarifa unazoweka na mijadala unayoshiriki.

Sambamba na hilo, fanya bidii kukutana na watu ambao tayari wanafanya kile unachotaka kukifanya. Kutana nao. Fanya nao kazi. Hakikisha unajenga kuaminika.

Mbinu unayoweza kuitumia unapofanya kazi na watu ni kuwasaidia kufikia malengo yao. Kumbuka unapomsaidia mtu kufanikiwa, unamtengenezea deni la kukusaidia zamu yako itakapowadia.

Christian Bwaya ni Mhadhiri Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi. Kwa ushauri wasiliana naye kwa 0754870815