Ukifuata utaratibu utaepuka gharama kuvunja mkataba

Thursday February 21 2019Justine Kaleb

Justine Kaleb 

By Justine Kaleb

Sheria inakutaka usianze kazi kabla hujapewa mkataba wa ajira lakini inakutahadharisha utakapotaka kuuvunja. Usipokuwa makini, unaweza kupoteza muda na rasilimali nyingi kushughulikia suala hili.

Usipokuwa makini unaweza kuvunja mkataba kiholela jambo lianloweza kukugharimu fedha nyingi na kukusababishia usumbufu mkubwa ambao ungeuepuka kama ungefuata sheria.

Sheria ya Mikataba ya mwaka 2002, Sheria ya Ajira na Uhusiano kazini ya mwaka 2004 zinaeleza mkataba wa ajira unaweza kuvunjika kwa wahusika kufariki dunia, matakwa ya kisheria, mfanyakazi kujiuzulu, kwa makubaliano ya kuvunja mkataba kati ya mfanyakazi na mwajiri, mfanyakazi kutiwa hatiani kwa makosa ya jinai au kushindwa kufanya kazi kwa sababu za kiafya.

Mwajiri anaweza kumfukuza au kumwachisha kazi mfanyakazi kutokana na utovu wa nidhamu, uwezo mdogo wa kufanya kazi au sababu za uendeshaji wa taasisi.

Sheria inamruhusu mfanyakazi kuvunja mkataba wa ajira kwa kufuata matakwa ya vipengele vilivyomo katika mkataba wake.

Utaratibu ni kutoa taarifa ya maandishi ya mwezi mmoja kabla au mfanyakazi kumlipa mwajiri mshahara wake wa mwezi mmoja endapo atatoa taarifa ya saa 24 kubainisha kusudio lake.

Advertisement

Ukiacha malipo ya kiinua mgongo mfanyakazi aliyevunja mkataba bado ana haki ya kulipwa haki zake zote kama wafanyakazi wengine kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande mwingine, mwajiri ana haki ya kuvunja mkataba anapokuwa na sababu za msingi, halali na zilizozingatia kanuni za haki.

Usivunje mkataba wa kazi kwa jazba, kwa kumkomoa mfanyakazi, kwa masilahi yako binafsi au kwa sababu isiyokubalika kisheria. Itakugharimu sana.

Ni muhimu kuomba ushauri kwa wataalamu wa sheria ili wakujuze namna bora unayoweza kuvunja mkataba wa kazi pasipo kusababisha hasara kwa pande zote mbili.

Vunja mkataba wa kazi kisheria, kistaarabu na kiungwana ili kesho ukihitaji tena kushirikiana na mtu huyo usipate ugumu wa kumpata au kupata kazi.

Advertisement