Masoko haya ya asali nje yanakusubiri wewe

Thursday March 28 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Upatikanaji wa soko la mazao ya nyuki yanayojumuisha asali na nta, hivi sasa upo wazi katika mataifa 24 duniani ambayo yanahitaji bidhaa hiyo kutoka Tanzania.

Tanzania inatajwa kuwa ya pili duniani kwa uzalishaji wa asali kutokana na kuvuna tani 38,000 mwaka jana ikichuana na Ethiopia inayopata tani 50,000.

Hata hivyo, uzalishaji wa asali uko chini kwani Tanzania inasafirisha asilimia 10 tu ya asali inayozalisha nje ya nchi.

Ingawa usafirishaji huo upo chini na mahitaji ya ndani bado ni makubwa, Watanzania wanapaswa kujielekeza katika uzalishaji asali nyingi zaidi kujihakikisha kipato kutoka katika mataifa hayo.

Kaimu meneja mawasiliano wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Tulizo Kilaga anasema soko kubwa la asali lipo Afrika Kusini, India, Botswana, Namibia, Canada, Dubai, Kuwait, Iraq, Iran, Japan, China na Lebanon.

Nchi nyingine zinazotaka asali na nta, Kilaga anasema ni Saudi Arabia, Oman, Rwanda, Uganda, Kenya, Ufaransa, Uholanzi, Norway, Ujerumani, Uingereza, Marekani na Ireland.

Advertisement

“Hizi ndizo nchi ambazo soko lake liko mikononi mwetu Watanzania na sisi kama wakala, tuko tayari kuwaunganisha wananchi wenye uwezo wa kuzalisha asali yenye viwango vinavyokubalika kimataifa ili wanufaike na soko hilo,” anasema Kilaga.

Anasema wastani wa pato linalotokana na asali nchini ni Sh818.4 milioni na nta kwa mwaka huingiza wastani wa Sh2.6 bilioni na mazao hayo yote pato lake linaweza kuongezeka kama uzalishaji utaimarika.

“Ufugaji wa nyuki ni fursa ya uwekezaji ambayo haijachangamkiwa sana na Watanzania hivyo ni vyema wakachangamka hivi sasa ili waweze kufanikisha masuala yao ya kiuchumi. Mahitaji ya asali huko duniani ni makubwa mno,” anasisitiza.

Wakati Kilaga akisema hayo, mkazi wa Liteli-Buchosa wilayani Sengerema, Magdalena Luhimbi anasema amekuwa akijihusisha na kazi hiyo kwa miaka mingi lakini hajui iwapo kuna soko kubwa kiasi hicho nje ya nchi.

“Ndio kwanza nasikia…kumbe huko nje kuna soko la asali, mimi ni mfugaji wa nyuki, mfanyabiashara na ninao uwezo wa kuanzisha ufugaji mkubwa maana huku kwetu misitu ni mingi, lakini sijui nianzie wapi kupata hili soko,” anasema.

Hata hivyo, Kilaga anasema soko la asali na nta lililopo nje lina vigezo vyake ambavyo ni lazima kuvikidhi kabla ya mfugaji au mfanyabishara hajapewa ithibati ya kusafirisha mazao hao.

“Siyo suala la kulala na kuamka unapeleka asali, muhimu ni kuzingatia ubora. Hili la ubora liko hivi, Serikali huchukua sampuli ya asali katika maeneo mbalimbali nchini na wake, huko ndiko ubora huangaliwa,” anasema.

Kilaga anasema, baada ya hapo maabara hiyo hutoa ithibati na kwa kipindi chote Tanzania imekuwa ikipata ithibati bora.

Kwa mujibu wa Kilaga, mtu anayetaka kuuza asali nje anatakiwa kupata kibali kutoka TFS iliyo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii huku akizingatia vigezo muhimu vya kila soko kwa muda wote atakaotakiwa kupeleka bidhaa hiyo.

“Hapa napo kuna changamoto kidogo, soko lipo, lakini mahitaji ya soko ni kigezo kingine ambacho mhusika anatakiwa kukizingatia. Je, ataweza kulitosheleza soko linalotakiwa?” anatahadharisha.

“Hatujawahi kulitosheleza (soko), hivyo ni muhimu pia mtu ajue ni kigezo mojawapo cha kupata hati.”

Meneja huyo anasema inaweza kuwa rahisi kwa wafugaji wa nyuki kupata asali nyingi iwapo watatumia mitambo maalumu kuikamua kutoka kwenye masega na kuachana na ukamuaji wa kienyeji.

“Unajua asali nyingi sana huwa inabakia kwenye masega, TFS tunayo mitambo maalumu pale Sao Hill (Mufindi) na Itigi kule Manyoni ambayo inakamua asali vizuri. Hii ni mitambo ya Serikali na wananchi wanaweza kuitumia kupata asali iliyo bora wakakidhi soko la ndani na nje pia wakasafirisha,” anasema Kilaga.

Kuhusu ufugaji, mtaalamu wa maisha ya nyuki na ufugaji, Juma Ismail wa TFS - Itigi wilayani Manyoni mkoani Singida anasema viumbe hao wana koo ambazo zinapoishi pamoja huzalisha asali kwa wingi.

Anasema, nyuki wanaofugwa vizuri katika misingi ya aina hiyo wanaweza kuzalisha asali ya kiwango cha juu ambayo inapoingia katika soko lolote, liwe la ndani au nje, inakuwa imejitosheleza kwa vigezo hivyo siyo rahisi kukataliwa na walaji.

“Kwanza inakuwa nzuri, tamu na nzito. Wao wanajua namna ya kuilainisha na kuifanya ivutie. Hata ikipimwa vipi haiwezi kukutwa na dosari zinazoweza kuikosesha ubora,” anasema Ismail.

Advertisement