Fursa bado zingalipo kwa ‘waliojikwaa’ kidato cha sita

Ieleweke kufeli kidato cha sita, si ishara mbaya maishani na wala haijawa sababu ya kuanza kuamini kuwa umeshafeli kimaisha.

Kwa kuzingatia ukweli kuwa wapo baadhi ya wanafunzi waliofanya vibaya katika matokeo hayo, lakini wanatamani kuendelea na masomo, makala haya yanaangazia fursa mbalimbali wanazoweza kutumia ili kutimiza ndoto zao.

Rudia mitihani

Njia mojawapo rahisi ya kurudisha matumaini ya ndoto zako za kusoma inawezekana kwa wewe kuamua kurudia mitihani yako kwa mara nyingine. Mfumo wetu wa elimu unatoa fursa hiyo ya kurudia mitihani na ndio maana kuna utaratibu wa watahiniwa binafsi. Rudi tena darasani kwa kusoma. Mathalani kuna shule nyingi zenye vituo vya maalumu kwa ajili ya watu wanaorudia mitihani ya kidato cha sita na aghalabu yake huwa ni nafuu.

Soma ngazi ya cheti

Fursa nyingine iliyopo kujiendeleza ni kusoma fani mbalimbali zinazoanza kwa ngazi ya cheti. Ikumbukwe badhi ya fani elimu ya cheti inatosha kuwa kipimo cha mtu kupata ajira.

Kwa mtu mwenye ndoto ya kusoma zaidi, kipato cha ajira kinaweza kutumika kama nyenzo ya kukuwezesha kuendelea na masomo ya juu.

Kwa mujibu wa mfumo wa elimu nchini, kuna vyuo vingi vya kada ya kati vinavyotoa elimu mbalimbali za astashahada ya msingi na astashahada ya juu.

Kutoka astashahada mwanafunzi anaweza kujiendeleza hadi ngazi ya stashahada na hatimaye kupata fursa ya kusoma elimu ya chuo kikuu.

Hii inaweza kuwa safari yenye mzunguko mkubwa, lakini usishau msemo wa wahenga: mvumilivu hula mbivu. Wapo waliovumilia ujanani, lakini wakiwa ukubwani wanaburudika na matunda ya safari ndefu ya elimu waliyopitia. Hawa ni pamoja na wasomi na wataalamu mbalimbali waliopo serikalini na sekta binafsi.

Kwa walio makini mlolongo huu wa kusomea astashahada na stashahda unaweza kukufikisha mbali. Unaweza kufika chuo kikuu kwa kutumia njia hii ya kusoma. Vipo vyuo vikuu vinavyowakubali wanafunzi waliopitia mfumo huu. Vyuo hivi vina ithibati ya Baraza la Usimamizi wa Elimu ya Ufundi (NACTE).

Hata hivyo, ni vyema kutoa angalizo na vyuo vinavyotoa mafunzo kwa ngazi za cheti, kwani baadhi yao havina sifa na havitambuliki na NACTE. Kabla ya kujiunga na chuo chochote, tafuta taarifa zake katika baraza hilo, ikiwamo kupitia wavuti wao wa www.nacte.go.tz

Jiunge na Veta

Hakuna ubaya kama kwa mhitimu wa kidato cha sita kusoma masomo ya ufundi katika vyuo vinavyosimamiwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Wengi wamekuwa na mtazamo hasi na vyuo vya VETA wanasahau kuwa vyuo hivi vina msaada mkubwa kiajira na hata kujiendeleza zaidi kielimu.

Zaidi ya yote wigo wa mafunzo ya VETA umekua na kuhusisha mambo mengi ya kiufundi ya kisasa na yanayolipa kiajira. Hivi sasa VETA inaendesha kozi kama masomo ya madini, utalii, Tehama na mengineyo muhimu katika zama za sasa.

Hakuna sababu ya kukata tamaa ikiwa bado una nafasi na fursa kedekede za kujiendeleza kielimu. Kama una ndoto ya kufanikiwa kielimu, fuata kilichosemwa katika makala haya utafanikiwa.

Elimu masafa

Uzoefu unaonyesha hapa nchini kuna watu wengi baadhi yao leo ni maprofesa maarufu waliowahi kufeli katika madaraja fulani ya kielimu siku za nyuma, lakini kwa kuwa tu walikuwa na dhamira ya dhati waliweza kujiendeleza na kufika kiwango hicho cha elimu kinachotamaniwa na kila mtu.

Watu hawa pamoja na wengine kuamua kuanza maisha ya familia au kikazi, bado walijiendeleza kupitia mfumo usio rasmi. Hawakukaa darasani bali walisoma kwa kutumia njia ya posta ambayo zamani ilikuwa maarufu.

Hii ndiyo inayoitwa elimu masafa inayotumiwa kwa kiwango kikubwa na watu wasiopata fursa ya kukaa darasani ama kwa kubanwa na kazi au kwa kuwa na majukumu mengine.

Elimu masafa ni mfano mmoja wa fursa za kielimu kati ya fursa nyingi wanazoweza kutumia wanafunzi waliofeli kidato cha sita, lakini bado wana ndoto za kujiendeleza kielimu, hasa ikizingatiwa kuwa elimu haina mwisho.

Kwa sasa taasisi maarufu za elimu masafa nchini ni pamoja na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Kupitia vituo vya taasisi hizi vilivyosambaa kila kona ya nchi, uwezekano wa kujiendeleza ni mkubwa na hatimaye mtu anaweza akaifikia ndoto yake ya kupata elimu ya juu.

0754990083