Ufaulu wa kusikitisha wa walimu 2019

Tuesday July 23 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Hali sio nzuri kwa wahitimu wa ualimu ngazi ya diploma ualimu wa sekondari (DSEE). Matokeo ya mtihani wa ualimu yaliyotangazwa hivi karibuni na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), yanaonyesha zaidi ya nusu ya wahitimu wamepata ufaulu wa chini, huku wahitimu 22 pekee wakifaulu kwa daraja la juu (distinction)

Kati ya wahitimu 7424, wahitimu 4992 sawa na asilimia 67.2 wamepata daraja la pass (ufaulu wa chini). Kwa mujibu wa taratibu za kielimu nchini, ufaulu huu unawaweka katika nafasi ngumu ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu hasa katika vyuo vinavyohitaji vigezo vya juu kiufaulu. Njia inayoweza kuwasaidia ni kurudia mitihani ya kidato cha sita kwa minajili ya kusafisha cheti.

Ukiondoa wahitimu 22 waliopata ufaulu wa juu, wengine wenye nafasi ya kujiendeleza ni wahitimu 1,947 waliopata ufaulu wa kati (credit) sawa na asilimia 26.2.

Hali ni mbaya zaidi kwa upande wa ualimu wa cheti daraja A (GATCE). Kati ya wahitimu zaidi ya 4000 ni mhitimu mmoja pekee aliyepata ufaulu wa juu.

Uchambuzi wa Mwananchi umebaini wanafunzi waliopata ufaulu wa kati ni 977 sawa na asilimia 20.4, huku waliopata ufaulu wa chini wakiwa 3814.

Kwa upande wa ualimu wa cheti, elimu maalumu (GATSCCE) hakuna aliyepata ufaulu wa juu kati ya wahitimu 98. watatu wamepata daraja la kati (credit), huku waliofaulu kwa kiwango cha chini wakiwa 87. Watahiniwa wanane wamefeli kabisa.

Advertisement

Matokeo mengine ni ya Diploma ya Ualimu na Ufundi (DTE), ambayo pia hakuna aliyepata ufaulu wa juu kati ya wahitimu 113. Aliyepata ufaulu wa kati ni mhitimu mmoja, huku 54 wakipata ufaulu wa kawaida. Wanaorudia ni wahitimu 58.

Maoni ya wadau

Mwalimu mstaafu Bakari Kheri anasema matokeo hayo sio tu yamemstua, lakini yanathibitisha madai ya baadhi ya wadau wa elimu kuhusu uwezo wa kitaaluma wa walimu nchini.

“Ufaulu kama ndio huu unaosema kuwa Ni wanafunzi 20 tu wenye ufaulu wa juu na maelfu wamepata ufaulu wa chini, kwa Nini tusiwe sahihi sisi tunaolalamika kila siku kuwa walimu wetu wenyewe hawajimudu? anasema.

Anaongeza: ‘‘Hiyo mithani ina masomo ya ualimu na pia yale wanayokwenda kufundisha, unapofaulu kwa daraja la chini, maana yake ualimu wako ni wa chini lakini pia hata masomo utakayofundisha, utawafundisha wanafunzi ukiwa na maarifa ya chini.”

Kheri anazitaka mamlaka husika kutafakari na kuchukua hatua ili mitihani ijayo wahitimu wengi waangukie katika ufaulu wa juu na wa kati

“ Tunahitaji walimu wa distinction na credit. Hawa ndio watakaosaidia watoto wetu kufika mbali n kulipa Taifa maendeleo. Sisi huku sekondari hawa wa ufaulu wa chini tunawaona lulu, hilo halipo vyuo vikuu. Kule ili uwe mhadhiri ni ama ufaulu kwa first class (daraja la kwanza au upper second (daraja la pili la juu) ...tuige huko, anaongeza kusema.

Mwalimu Damas Lukasi, anasema hashangazwi na matokeo hayo kwa kuwa mfumo wa elimu ya ualimu nchini unaruhusu watu wasio na sifa kusomea taaluma ya ualimu.

‘‘ Sishangazwi kabisa kwa hilo, ndipo tulipotoka walimu hata mimi ninayezungumza. Usiulize matokeo yao, jiulize walipoomba nafasi hizo walikuwa na sifa? Kama tunachukua watu waliofeli kusomea ualimum unategemea miujiza wafaulu? anasema?

Advertisement