ANTI BETTIE: Huyu mtoto wangu au nimebambikiwa mbona sielewi

Sunday May 5 2019

 

Nimezaa na mke wangu, lakini kila tukigombana ananiambia huyu mtoto siyo wangu.

Anti nifanyeje?

Acha kutojiamini, mwanaume unatakiwa ujiamini. Ukiachana na hilo huyo mwanamke hana adabu na somo yake hakufanya kazi ya kumfunda ipasavyo ndiyo maana anaropoka hata kama ni kweli hakupaswa kuongea kama anaota. Ushauri wangu kama una fedha nenda kampime vinasaba bila mtoto kujua kuwa unampima kujiridhisha kama mwanao kwa sababu ukibaini ni wa kwako atakuchukia kutokana na kumtilia shaka na hata akiwa siyo wako haitakuwa picha nzuri kwa mrtoto asiye na hatia, pili washirikishe washauri wenu wandoa kuhusu suala hilo ikiwa ni pamoja na kumtaka mwanamke aseme ukweli kama mtoto ni wako au kakubambikia. Ila pole.

Uzuri wangu unaniponza

Mimi ni msomaji mzuri wa kolamu yako, swali langu ni kwa nini sisi wanawake wazuri huwa hatuolewi?

Au niende kwenye maombi?

Nashukuru kwa kuwa msomaji wangu mzuri, lakini napata ukakasi au nachelea kukubali au kukataa kuwa wewe ni mzuri kwa sababu hujaniambia nani kakuambia kuwa u mzuri na hujaniambia unapima vipi kigezo cha mzuri na mbaya.

Ninachotaka kukuambia kuwa mwanaume haoi sura, anaoa tabia kama unatabia mbaya hata ukiwa mzuri kama waridi bado utakosa vigezo vya kuolewa, uzuri wa sura humvutia mwanaume kwanza, lakini tabia humaliza mchezo wote.

Nimemuacha lakini nikimuona roho inadunda

Mke wangu kanikataa kwa sababu alinifumania na akafanya vurugu hadi tukaachana, lakini kila nikimuona roho inanienda mbio.

Nifanyeje?

Usihangaike nenda kamuombe msamaha kabla siku hazijapita sana, kwa sababu kama mlipendana hadi mkaoana ina maana na yeye anakufikiria. Ila unachotakiwa kufanya ni kumuhakikishia hautarudia na ufanye hivyo kweli, lakini kama unafanya hivyo kwa dhihaka akiondoka tena harudi.

Njia rahisi watumie watu wenye busara ambao yeye anawaamini ikiwamo viongozi wa dini. Usisahau kuwa wanawake ni wengi hautawamaliza tulia na mkeo.

Advertisement