Diwani aliyegeuza taka mtaji, atumia faida kusaidia jamii

Sunday December 1 2019

 

By Hawa Mathias, Mwananchi [email protected]

Katika mitaa, barabara kubwa na ndogo kuna marundo ya takataka ngumu na laini.

Wakati watu wakilalamikia kuwapo kwa taka hizo, Aida Haule, msichana wa miaka 29 amezigeuza mtaji wa kujiingizia kipato.

Aida ambaye ni diwani wa viti maalum (CCM) kata ya Utengule Usongwe mjini Mbalizi mkoani Mbeya anazitumia taka hizo kutengenezea mkaa.

Kwa Aida, faida anayoipata katika biashara hiyo haiishii kwa matumizi yake binafsi bali anairudishia jamii inayomzunguka, anatenga asimilia 40 ya faida hiyo kusaidia vijana wenye mahitaji maalum ikiwamo waliopungukiwa ada za shule na wengineo.

Anasema wazo la kuuza mkaa lilitokana na dhamira yake ya kukataa kuwa tegemezi kwa mwanaume hata kama ni mumewe.

Katika kutengeneza mkaa huo, Aida hukusanya mabaki ya vyakula mashambani, pumba za mpunga, maranda, udongo na kusaga kwenye mashine maalumu.

Advertisement

Vitu hivyo vikisagwa na mashine hutoa vitu mfano wa vitofali ambavyo huvianika na vikikauka hutumika kupikia kama mkaa.

“Awali nilikuwa nakausha kwa jua, lakini nilipoona wateja wamekuwa wengi vinachelewa kukauka nikatengeneza bani ya kukaushia.

“Hata kwenye hii bani ili kupata joto la kukausha haraka, nami hutumia nishati hii hii mbadala kuwasha moto,” anasema.

Anasema kama diwani, licha ya kujikwamua, anatakiwa ahakikishe anatunza mazingira na kuwatafutia ufumbuzi wananchi wa eneo lake. “Inajulikana kuwa tani moja ya mkaa ni sawa na kukata miti tani 12 jambo ambalo kwa namna yoyote ile linachangia upotevu wa rasilimali misitu na kusababisha nchi kuwa jangwa na hata majanga kama ya mafuriko na ukosefu wa mvua za kutosha,” anasema.

“Nimekuwa nikitumia mradi huu pia kutoa elimu kwa kina mama kuachana na matumizi ya mkaa ili kuzuia uharibifu wa mazingira.”

Uzalishaji kwa siku.

Aida kwa siku anazalisha tani tatu hadi tano ambazo zote zimekuwa zikiingizwa sokoni na anapata wateja maalumu ambao ni mama lishe na wale wa majumbani.

“Ukiwasha nishati hii unatumia kwa saa tatu bila kujali unapika nini ilimradi ni matumizi ya kawaida. Kilo moja nauza Sh500,” anasema.

Anasema faida nyingine inayopatikana kwenye nishati hiyo ni majivu yake, yanatumika kuulia wadudu waharibifu kama mchwa, kusugulia masufuria, mbolea ya mbogamboga na matunda.

Namna anavyowapata wateja

Anasema amekuwa akipata wateja wengi kwa kutumia mawasiliano ya simu kwa njia ya WhatsApp na marafiki na watu aliowasevu kwenye simu yake anawatangazia bidhaa hiyo na kuwaonyesha, kisha wateja hao hao wanakuwa mabalozi kwa wenzao.

Ili kuwafikia wateja, Aida ameajiri vijana 19, wasichana wakiwa wanane ambao kwa siku huwalipa Sh5,000 hadi Sh9,000 kulingana na kazi.

“Pia nimetenga asilimia 40 ya mapato yangu kusaidia vijana wenye mahitaji maalumu kama wanaopungukiwa na fedha wanapotaka kwenda shule.

Anasema pia anatengeneza majiko ya udongo ambayo huuza kati ya Sh15,000 mpaka 50,000 kulingana na ukubwa.

Anasema changamoto iliyopo sasa ni kuhakikisha anawahamasisha wateja wa majumbani kwani mwamko bado upo chini. “Ukilinganisha na mama na baba lishe, majumbani bado hawajaona kama nishati hii ni mkombozi hivyo nikihudhuria mikutano naitumia kuwahamasisha.

Anasema nyingine ni namna ya uendeshaji ambao unatakiwa kuwa na mtaji mkubwa, hususan ununuzi wa mashine, uboreshwaji wa miundombinu katika maeneo ya uzalishaji wa nishati hiyo.

“Tunaomba halmashauri iwekeze kwetu wawekezaji wadogo ili kukuza mitaji yetu, hususan kinamama wa kwenye vikundi kwa kuwapatia mikopo ya waanzish miradi, “anasema.

Mikakati yake

Kwa mwaka ujao 2020, Aida pamejipanga kuhakikisha anawapa mikataba ya ajira vijana wote wanaofanya kazi katika kiwanda chake ili wapate stahiki zao kama watumishi wa sekta nyingine.

Anasema anatambua changamoto za ajira kwa vijana na kukosekana kwake kunavyochangia vijana kuingia katika mambo ya kidunia, hasa matumizi ya dawa za kulevya na pombe.

Mbali na ajira pia, ameandaa fursa za mafunzo kwa vijana ili kuwajengea uwezo wa kujiajiri katika nyanja mbalimbali za kiuchumi ili kuungana na Serikali kutatua changamoto za ajira.

Aida anawashauri wanawake walio katika sekta binafsi na serikalini kupanua wigo wa kifikra kwa kuanzisha miradi itakayowaongezea kipato. “Fursa ni nyingi sana za kiuchumi lakini kuna kinamama wamelala wanasubiri kupata mitaji mikubwa.

Anasema hata yeye hakutumia mtaji mkubwa na hakufundishwa darasani, bali kwa kuona wenzake wanafanya nini.

Pia anawataka wanawake kuacha kulalamika na kuwa tegemezi kwa wanaume. “Kulalamika, kuwategemea wanaume hata kama wametuoa ni kuwaonea na kujionea sisi wenyewe, kama unajishughulisha mnaongeza kipato cha familia,” anashauri.

Kuhusu siasa Aida anasema kuwa amegombea udiwani ili apate nafasi ya kuwasaidia vijana kujiajiri. “Lengo langu ni kuhakikisha nawatoa tongotongo za macho vijana wasioamini kwenye mafanikio ya uthubutu, wanaosubiri wawezeshwe na wenye fedha badala ya kujikwamua wenyewe kwa kiwango kidogo cha fedha walicho nacho.

“Nikifanikiwa kuwa diwani tena kwa muhula wa pili utakuwa ndiyo wa mwisho, naamini hapo nitakuwa nimewapa vijana na kina mama elimu ya kutosha kuhusu ujasiriamali, ”anasema Aida.

Advertisement