JACK UMEME: Kujiamini, kuthubutu, ndiyo siri ya mafanikio

Sunday December 15 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Wanawake ni kundi linalokabiliwa na changamoto nyingi karibu katika kila jambo wanalolifanya, iwe nyumbani, kazini na hata kwenye shughuli binafsi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Jarida la Forbes kuhusu changamoto zinazowakabili wanawake kwenye ujasiriamali mwaka 2018, jarida hilo lilionyesha kuwa ni kawaida wanawake kukataliwa mikopo kwa sababu ya upendeleo wa kijinsia.

Jarida hilo lilitaja vipengele vinane wanavyokabiliana navyo wanapoamua kuwekeza ni ukosefu wa fedha, kutokana na taasisi za mikopo kuwabagua na kuwapendelea zaidi wanaume.

Lilieleza kuwa biashara za wanawake ni kati ya shughuli zinazoongoza ambazo hazina msaada wa kifedha, kwa sababu taasisi nyingi huwa zinafadhili biashara zinazomilikiwa na wanaume.

Kutokana na sababu hizo na nyingine, wengi wao wamekuwa wakiogopa kuanzisha shughuli za ujasiriamali kwa kuhofia kushindwa.

Hata hivyo sababu hizo hazikuwa kikwazo kwa Shukurani Joseph ambaye licha ya kutokuwa na mtaji aliamini anaweza na sasa anamiliki duka la spea za magari.

Advertisement

Ukimuangalia kwa haraka utadhani ni msichana ambaye hajawahi kufanya kazi za nguvu katika maisha yake. “Sikufaulu kuendelea na elimu, ila niliamini nina kitu ndani yangu, nilipambana kukitoa nje kwa mustakabali wa maisha yangu,” anaanza kueleza Shukurani anayetambulika zaidi kwa jina maarufu la Jack Umeme.

Jack Umeme nilikutana naye hivi karibuni katika utoaji tuzo za kuandika insha kwa wanafunzi wa kike wa shule za Sekondari kuhusu Elimu ya wasichana katika fani ya uhandisi, teknolojia na hesabu iliyoandaliwa na Taasisi ya Women and Electronic Tanzania( WET).

Kati ya wageni waliokuwa meza kuu, yeye alikuwa mmoja wa waliokuwa wakitoa shuhuda za mafanikio yao katika masuala ya kazi za ufundi na teknolojia kama njia ya kuwahamasisha watoto wa kike kutoogopa kazi hizo kwa kuwa zinaweza kufanywa na jinsi zote.

Moja ya jambo lililonivutia kwake ni kueleza namna alivyoweza kuifanya kazi ya ufundi umeme tangu akiwa na miaka 16.

Katika mahojiano maalumu Jack Umeme anasema, “ilikuwa mwaka 2002 nilipomaliza elimu yangu ya msingi kwa bahati mbaya sikuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari, kuanzia hapo ilinichukua zaidi ya miaka 10 kupata Sh15 milioni kutimiza ndoto niliyoianza.

Anasema baada ya kukosa nafasi ya kuendelea kidato cha kwanza, baba yake aliamua kumsomesha ufundi.

“Kutokana na utundu niliokuwa nao wakati nakua, ikiwa ni pamoja na kuwa na marafiki wavulana kuliko wasichana, baba alisema nikasomee ufundi magari katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji(NIT) kilichopo Mabibo Jijini Dar es Salaam.

Anasema licha ya utundu aliokuwa nao, mwanzoni alimkatalia baba yake kwenda kusomea fani hiyo, “Baba alisema kama sitosoma alichoniambia ambacho anaamini nitaweza hatanihudumia kwa lolote.

Anafafanua kuwa kutoka moyoni alitamani kuendelea na masomo ya sekondari, lakini baada ya kuona hana namna akaazimia kusomea alichosema baba yake lakini kwa kujituma zaidi.

“Azma niliyojiwekea ndiyo imenifikisha hapa nilipo, sikuogopa kushindwa, wala sikujali watu watasema nini, nilijiamini nitatoka kwa kazi hii,” anasema.

Kwa sababu hakuwa amesoma elimu ya sekondari ambako angejua walau lugha ya Kiingereza kidogo ambayo ndiyo ya kufundishia vyuoni, alilazimika kujiandaa kwa hilo kwanza.

“Safari yangu ilikuwa ndefu sana, kwani nililazimika kwanza kujiunga na Chuo cha Upendo kilichopo Kijitonyama ambapo nilisoma kozi ya Kiingereza kwa miezi sita.

“Mwaka 2004 nikajiunga NIT nikasoma miaka mwili, mwaka 2006 nikaanza kufanya shughuli za ufundi magari kwenye maeneo ya Ilala, kwenye maduka na gereji za watu,” anasema.

Mazoea hayo yalisababisha wenye maduka kumuamini na hata wakati mwingine kumpa mali kwa njia ya mali kauli.

“Hata hivyo wakati naenda kununua vifaa hivyo nilikuwa nikizidisha gharama kwa kila kifaa kwani wateja wangu wengi waliniamini na kunipa hela nikanunue mwenyewe.

“Ilipofika mwaka 2011 nikashauriana na baadhi ya wenzangu watatu tuliokuwa tukifanya kazi hiyo ya ufundi kwa nini tusifungue duka letu la spea kwa kuwa kama wateja tunao wa uhakika badala ya kuwapelekea watu wengine hiyo hela ibaki kwetu,” anasema.

Anasema jambo hilo wenzake hao ambao ni wanaume waliliafiki na hatimaye kukodisha eneo la kufanyia biashara hiyo japokuwa alidumu nao kwa miezi minne na kuamua kuachana nao.

Hii ni baada ya kuona hapati kile alichotarajia, kwani kama ni Sh200,000 imeingia kama faida iliwabidi kugawana Sh50,000 kila mmoja huku matamanio yake ilikuwa faida hiyo yote iwe yake.

“Nilijikusanya mwenyewe kwa kuweka fedha ninazopata katika ufundi na zile tunazouza spea kidogokidogo mpaka nikafikisha Sh15 milioni na kuamua kufungua duka langu mwenyewe mwaka 2014.

Anafafanua kuwa umaarufu wake wa kazi hiyo, umemsaidia kufanya mambo mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo kumiliki nyumba mbili, kuwa na viwanja vinne na daladala moja.

Kuhusu changamoto alizowahi kukutana nazo anasema wakati anaanza kazi hiyo baadhi ya wasichana walikuwa wakimchukulia ndivyo sivyo, huku wanaume nao kumuona kama mwanamke asiyefaa katika jamii.

“Kuna baadhi ya wanaume walinidhihaki na kusema sina sifa za kuwa hata mke wa mtu kwa namna nilivyojiweka na shughuli ninazozifanya na wateja wengine hata kudharau kuwa siwezi kufanya kazi hiyo, lakini nashukuru kwani kuna walioniamini hawakusita kurudi tena,” anasema.

Hata hivyo nilipomuuliza kuna uhusiano gani wa mwanamke anapofanya kazi zinazodhaniwa ni za kiume kujiweka kama mwanaume, Jack anasema ni kutokana na aina ya kazi wanazozifanya zinasababisha wawe hivyo.

“Hivi mimi kazi yangu hii ya kuingia hadi chini ya magari unategemea siku unikute nimevaa kucha za bandia au kujiremba kama wale wanawake wanaoshinda kwenye ofisi zenye viyoyozi au zisizo na kazi za purukushani, la hasha hivyo ndio maana mnatuona tunakuwa kama wanaume wakati mwingine,” anasema.

Wito wake kwa wasichana ni kutochagua kazi kwa sababu hakuna mahali pameandikwa hii kazi ni ya mwanamke na hii ni ya mwanaume.

Anasisitiza muhimu zaidi wa vijana, wasichana kuwaamini wazazi kwani wana maono juu ya hatma ya watoto wao.

“Baba alinichagulia cha kufanya, nimemsikiliza na sasa nakula matunda, ”anasema.

Advertisement