Kila tunapojaribu kusogea pazuri, mitandao inatuvuta shati

Muktasari:

  • Hebu rudisha nyuma wakati kwa miaka 20. Fikiria maisha bila mtandao na aina ya viongozi tulionao. Utapata jibu kuwa tunahitaji sana kuwa na mitandao kwa sababu inatuweka karibu na wanaotuongoza na kutusaidia katika kufanya uamuzi.

Juzi kupitia mitandao nilifuatilia msiba mzito wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi. Jioni ya Mei 9 nilishuhudia jeneza lake likishushwa taratibu na Askofu aliyeongoza ibada yake alimalizia kwa maneno “Dk Mengi ulitoka mavumbini na umerudi mavumbini.”

Kila aliyekuwa katika eneo hilo alikuwa akibubujikwa na machozi. Wajane, walemavu na Watanzania kwa ujumla walimlilia kila mmoja kutokana na alivyomfahamu.

Lakini kupitia mitandao hiyo hiyo tangu mwaka huu uanze nimeshuhudia maziko ya wadau wengine wa habari: Ruge Mutahaba na Ephraim Kibonde.

Naweza kusema ni matukio yanayotukumbusha sisi ni nani na mwisho wetu ni upi. Ni matukio yanayotukumbusha kuhusu uumbaji na Mungu kwa ujumla.

Wajane, watoto na wategemezi wengine wanaobaki baada ya kifo cha mtu yeyote ni somo kwetu kwa sababu wote safari yetu ni moja. Ni suala la muda tu.

Mitandao inatusaidia kutuleta pamoja wakati wa shida kama hizi. Maili milioni nyingi kutoka katika upande mwingine wa dunia unapata taarifa, salamu na mambo mengine yanayoleta faraja.

Lakini si hayo tu, mitandao imetusaidia kufuatilia Bunge ingawa live ingawa si live kwa maana ya mubashara. Imekuwa kiunganishi kati ya wananchi na wawakilishi wao.

Juzi kati hata kiongozi wa Bunge alilalamika kwamba baadhi ya wabunge wanajirekodi na kusambaza mtandaoni taarifa ambazo hazijaingia kwenye hansadi.

Hebu rudisha nyuma wakati kwa miaka 20. Fikiria maisha bila mtandao na aina ya viongozi tulionao. Utapata jibu kuwa tunahitaji sana kuwa na mitandao kwa sababu inatuweka karibu na wanaotuongoza na kutusaidia katika kufanya uamuzi.

Sasa wakati mitandao ikituletea tija hiyo, katikati yanaibuka mambo mengi yasiyofaa na kukamata akili zetu.

Mambo haya kuibuka sio vibaya lakini kuyashabikia na kusahau misingi ya Utanzania na imani zetu ndio ulipo ubaya.

Iwe ya kutengeneza au halisi, si vitu vya kushabikia kwa sababu vinatuondoa kwenye njia kuu. Tunapotea kwa kujaza ujinga kwenye akili zetu badala ya maarifa ambayo yamejaa tele mitandanoni. Ni hayo tu