ANTI BETTIE: Mama mkwe ni tatizo, hanitaki anamwambia mwanaye aniache

Ninapendana sana na mume wangu, lakini mama mkwe hanitaki. Kibaya zaidi ni mnafiki nikikutana naye anaonyesha upendo wa hali ya juu kwangu, lakini kila siku anamshinikiza mwanaye tuachane. Nifanyeje?

Pole sana. Kwanza umejuaje kama mama mkwe anamshinikiza mwanaye akuache? Kama mumeo ndiyo alikuwa anakuambia basi muogope kwa sababu anakuchonganisha na mtu unayetakiwa kumuheshimu na umchukulie kama mshauri wenu katika ndoa. Pili inawezekana mumeo ana tamaa ya kuoa mke mwingine hivyo anakuandaa kisaikolojia kuwa mama yake anamshinikiza kukuacha.

Ukipata uhakika kama ni kweli mama yako anamshinikiza mumeo kuoa na akikuona anakuonyesha upendo ina maana upo karibu naye, siku funga safari nenda nyumbani kwake au anakoishi, msaidie kazi kuleni pumzikeni kisha mwite faragha umueleze masikitiko yako kwa kile anachotaka kitokee.

Atastuka sana kwa sababu ilikuwa siri yake na huyo aliyekuwa akizungumza naye, lakini ujumbe kuwa umejua njama zake utakuwa umemfikia na kama ana aibu ataacha.

Hakikisha unazungumza naye kwa upole, huku ukisisitiza kama kuna kosa uliwahi kumfanyia akusamehe kuliko kuvunja ndoa yako.

Jambo la kuzingatia ni uwasilishaji wako, hakikisha unamsihi na kumuhakikishia mazungumzo hayo ni kati yenu wawili. Kuna wakati anaweza kuwa mkali kwa madai unamvunjia heshima, jishuhe mtulize kwa hekima kubwa, usipaze sauti na akitaka kufanya hivyo msihi. Ukiona kuna ulazima wa kupiga magoti ili mwende sawa fanya hivyo,

Mume wangu amemkataa mwanaye tangu mimba, nifanyeje?

Habari Anti! Mimi ni mama wa mtoto mmoja, niliishi na mume wangu miaka miwili bila kupata ujauzito, nilipoupata mume wangu aliukataa ujauzito ukiwa na miezi mitatu. Nilipojifungua siyo baba wa mtoto, ndugu, jamaa wala rafiki aliyeulizia hali ya mtoto, nimemlea huu ni mwaka wa tatu. Nifanyeje?

Wewe ni mwanamke na una sifa hasa ya kuitwa mama. Kwa sababu umeshapambana hadi amefikisha miaka mitatu, natamani uendelee hivyo hivyo badala ya kuanza kusumbuana naye katika vyombo vya sheria kwa sababu itakurudisha nyuma.

Hukusema ulijifungulia wapi na unaishi naye au mmeachana, kama unaishi maisha yako peke yako na huu ni mwaka wa tatu unamlea mwanao sidhani kama kuna kitakachombadili mawazo huyo mwanaume ukizingatia ameungana na ndugu zake kukudharau na kumtelekeza mtoto wao.

Vyombo vya sheria vipo ikiwamo Ustawi wa Jamii, lakini jiandae kuacha shughuli unayofanya na kuanza kufuatana fuatana na mtu ambaye alionyesha hana nia na huyo mtoto tangu ukiwa na ujauzito wa miezi mitatu.

Kama angekuwa na nia, miaka mitatu ni mingi angekuwa anatuma hata marafiki zake wanakuja kumuona mtoto.

Usimtie mwanao unyonge kwa kuhangaika na mtu asiyewataka. Naam hawataki, kumpeleka ustawi wa jamii ni kudai haki ya matunzo ya mtoto, lakini kuna mawili anaweza kutoa au akakataa, kuliko kupoteza mwelekeo kwa kuanza kufungua kesi huku na kule nakushauri endelea na maisha yako.

Kizuri hujasema unapata taabu, pambana kumlea mwanao mtu kama huyo hesabu kama amefariki siku akifufuka atakuja kumchukua mtoto wake. Unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha mwanao anatambua baba yake ni nani na yupo wapi kama unajua alipo.

Usimjengee chuki mtoto na baba yake kwa sababu haitasaidia sana sana itamfundisha mwanao tabia mbaya ukubwani