TUONGEE KIUME: Midomo ya wanawake wengi wa siku hizi haina nukta

Iliandikwa sehemu kama mzaha kuwa mwanamke wa enzi hizo, mume wake akirudi nyumbani jioni kutoka mihangaikoni, atamuandalia maji ya kuoga kisha chakula. Sasa ikitokea siku hiyo, mwanaume akadai kwamba hatakula kwa kuwa ameshiba, huyo mwanamke atachanganyikiwa kwa mawazo.

Atawaza ni nini amemkosea mumewe kiasi kwamba hata kula chakula chake hataki. Au labda ni tatizo gani limemkuta hata aone chakula ni kizito, hakiliki.

Unaambiwa kwa sababu hiyo tu, mwanamke anaweza kujifungia ndani siku nzima, akalia sana kwa maumivu na masikitiko ya mume wake kutokula chakula chake.

Mwanamke wa siku hizi, mume wake akirudi atamuandalia maji ya kuoga kisha chakula. Na ikitokea mwanaume akasema hajisikii kula siku hiyo – mwanamke atabeba chakula na kurudi nacho jikoni. Atafunua sufuria ya mboga, kisha ataongezea nyama nne hapo, halafu atarudi nacho sebuleni na kukifukia chote yeye mwenyewe.

Tukiachana na mzaha, ni kweli kabisa wanawake wamebadilika. Mienendo ya wanawake wa miaka 25 iliyopita haifanani hata kwa asilimia 50 na mienendo ya sasa. Cha muhimu kukumbuka kabla hatujafika mbali ni kwamba mabadiliko si dhambi, ni kitu kizuri kwa sababu huenda mienendo waliyonayo wanawake wa sasa, inakidhi mahitaji ya maisha tuliyonayo sasa.

Kitu kimoja kibaya kwenye mabadiliko ni kwamba kuna wakati yanapotokea hubadilisha hata vitu vizuri ambavyo labda tulikuwa tunavihitaji.

Mfano halisi wa moja ya lulu ambazo walikuwa nazo wanawake wa zamani, lakini imekumbwa na mafuriko ya mabadiliko, ni uwezo wa mwanamke kutunza mambo ya ndani ya nyumba – wanawake wa siku hizi wameshindwa kabisa.

Mwanzo ilikuwa inafahamika kwamba ukitaka jambo lisambae haraka mwambie mwanamke, hasa likiwa jambo baya. Lakini niamini mimi, kama jambo lenyewe likiwa linamuhusu yeye binafsi, hawezi hata kulizungumza kwa sababu wanawake ni wazuri kwenye kusambaza mambo ambayo hayawahusu.

Lakini hawa wa siku hizi tofauti kidogo. Linaweza kutokea jambo ndani, yeye na wewe, ambalo pengine labda hata wazee wa familia hawakutakiwa kufahamu, yeye akalichukua na kulipeka saluni kesho wakati anasuka nywele.

Humtunzi vizuri, anaweza kusimulia. Umefanya ufisadi nje ya ndoa, hashindwi kusimulia. Una mapungufu kidogo, anaweza kuyasema.

Hatusemi kwamba mwanamke hatakiwi kuzungumzia matatizo yenu. Lakini Je, anayazungumza sehemu sahihi.

Kuna mambo ya kuzungumza wawili, kuna mambo ya kuwahusisha watu wengine lakini wanaostahili; wakubwa kwenye familia au labda viongozi wa dini, bali si wasusi. Lakini wanawake wa kisasa hilo linawashinda kidogo. Yaani hata ndoa zao wanazichukulia kama stori za mjini wanazopishana nazo katika mitandao ya kijamii.

Hatuwezi kuzuia mvua. Tunaweza kutumia miamvuli kutembea kwenye mvua. Yaani hatuwezi kuzuia mabadiliko yao. Tunaweza kutafuta namna ya kushughulikia mabadiliko yao.