TUONGEE KIUME: Aina mbili za jinsi mkeo, familia, baamedi watakavyokukumbuka ukishaaga dunia

Ungependa ukiondoka duniani watoto wako wakukumbuke namna gani? Kwamba ni mwanaume mmoja aliyebahatika kuwa na uhusiano na mama, kisha wakaoana, tukapatikana sisi.

Au mwanaume aliyewahi kumpenda mama yetu, akashindwa kuvumilia kuwa mbali na anachokipenda akamuoa, kisha tukapatikana sisi, wakatuleta duniani na kutukuza kwa upendo licha ya kwamba kuna wakati maisha yalikuwa yanalazimisha isiwe hivyo. Akatupambania sisi kama wanae kuhakikisha tunapata kila kitu kinachostahili kutoka kwa baba, kisha Mungu alipoona inatosha hapa duniani akamchukua, kumtanguliza mbinguni ili nasi, mama yetu, siku tukienda huko tukute ametuandalia sehemu nzuri kama alivyotufanyia hapa duniani. Unapenda wakukumbuke vipi?

Na mkeo naye akukumbaje? Kwamba ni mwanaume niliyekutana naye nikidhani ananipenda, nampenda, tunapendana, tukafunga pingu za maisha na tangu hapo maisha yangu yote yakawa ni kifungo cha ukweli, sina uhuru, furaha, amani kiasi kwamba sijui kwa nini Mungu alibariki ndoa yetu?

Au ungependa akukumbuke kwamba ni mwanaume ambaye nilipokutana naye, niligundua hakutokea tu, Mungu alimleta kwenye maisha yangu ili awe kiongozi wangu, kesho na kesho kutwa na siku baada ya kesho kutwa niishi nikifurahia pumzi niliyopewa. Nikashindwa kuvumilia maumivu ya kumpoteza, tukafunga pingu za maisha naye, kwa maana ya kwamba tulivifungia vitu vyote vinavyopoteza utamu na maana halisi ya uhai, amani, furaha, raha, upendo na uhuru ndiyo ilikuwa sehemu kuu ya maisha yetu. Nikampa zawadi ya watoto, akanipa zawadi ya kuwalea na kuwapenda na sasa Mungu akasema nauchukua mwili wake, naurudisha ulipotokea mavumbuni, lakini roho na nafasi naicha kwenu, ataishi moyoni mwako milele daima...Nauliza ungependa mkeo akukumbukeje?

Familia yako nayo ikukumbuke vipi? Kwamba ni yule mtoto wa mjomba anayeishi Nyegezi, yule mwaka juzi kwenye msiba wa marehemu shangazi alikuja amelewa, akaamka usiku na kuanza kutapikia watu wakiwa wamelala.

Au ungependa iwe? Yule ndugu yetu anayeishi Kasulu mtoto wa mjomba. Yule mwaka juzi wakati tupo kwenye msiba wa marehemu bibi alitoa wazo kwamba tuanzishe kikundi cha kusaidiana kwenye shida na raha kwa ajili ya watu wote tuliowahi kukulia kijijini kwetu, ili matatizo yakitokea tusipate taabu kama ilivyokuwa kwenye msiba wa bibi. Ungependa wakukumbukeje?

Na mhudumu wa baa unayopenda kunywa unataka amwambie vipi mwenzake kwamba wewe umekwenda? Amwambie, hulijui lile baba jeusi jeusi hivi, lile likilewa linapenda ugomvi. Si lile lilikuwa linamshika shika Suzi siku ile hadi meneja akamuitia mabaunsa wamtimue.

Au aseme, ‘Jamani! humjui yule baba huwa anakuja na wenzake watatu, akilewa anakuwa na stori za kuchekesha. Anapenda sana kukaa viti vya hapa kaunta? Ungependaje?

Sasa hapa kupenda ni jambo moja tu, la pili na ndilo ambalo la msingi zaidi ni kwamba unatakiwa uishi katika matendo ambayo ndiyo yataamua ukiondoka watu wakukumbuke kwa namna gani. Kumbuka hakuna atakayedumu duniani.