TUONGEE KIUME: Desemba, Januari miezi ya wanaume kula kwa jasho

Sunday December 1 2019

 

By Kelvin Kagambo

Huko kwenye maandiko imesimuliwa baada ya Adam na Hawa kula tunda la mti wa kati Mungu aliwaadhibu; akamwambia Hawa atazaa kwa uchungu na Adam atakula kwa jasho, muda wa kuthibitisha andiko hilo kwa upande wa wanaume umeanza.

Siku zote tunakula kwa jasho letu, lakini kula kwa jasho kwa kiwango kilichoandikwa kwenye maandiko matakatifu tunapaishi Januari. Katika mwezi wa kwanza maneno kama sina hela, niko vibaya ndiyo msimu wake. Watu wanakuwa weupe, akaunti zinasoma kama namba za mawimbi ya redio 88.5 jasho linatutoka kweli kweli.

Januari si ngumu

Kila gonjwa na chanzo chake, gonjwa la kusota tunakosota Januari linasababishwa na mwezi huu.

Januari wala si ngumu kiasi hicho, ina siku 31 tu kama tunavyoona kwenye kalenda, lakini kiuhalisia huwa inafikia hadi siku 42 au 47 kwa sababu ya Desemba.

Mwezi huu una mambo mengi sana . Mwezi huu una likizo, watoto wanatakiwa wapelekwe kijijini kwa bibi yao. Bibi naye ni mgeni njoo mwenyeji apone, anategemea akitembelewa, wakati anakuja kukupokea stendi akukute umebeba vifurushi na mia mbili tatu za kununilia mafuta ya taa. Na kumbuka hadi watoto wakifika hapo, maana yake umeshawalipia nauli ya basi iliyopanda bila sababu za msingi kwa sababu tu ni Desemba.

Advertisement

Ukisema watoto wabaki mjini tu si kwamba ndo utakuwa umejiokoa, hapana. Hiyo Waswahili wanaita ‘umeruka majivu umekanyaga moto’. Desemba ina sikukuu kibao na ikikuta mjini maana yake ni pesa lazima itumike. Watoto watataka kuvaa nguo mpya wapendeze, watataka kula mapilau kuku, na bado watataka uwapeleke sehemu wakafurahi, yote haya yanahitaji pesa.

Sasa jambo la kuchekesha ni mambo yote haya yanayoongezeka yenyewe tu kamshahara kako kanabaki vile vile.

Unaingia Januari na viraka

Ili tuweze kuimudu Desemba na sikukuu zake, wengi inabidi tukope.

Maana yake ni kwamba mkopo huu tutaulipa na mshahara wa Desemba. Tukilipa tunajikuta hatujabakiwa na kitu, matokeo yake unaanza mwaka mpya na viraka, huna chochote mfukoni.

Hapo sasa ndio ugumu wa Januari unapoanza kwa sababu pesa ambayo ulijua utaitumia kufanya manunuzi ya kuwaandaa watoto kurudi shule Januari ulishaitumia kulipa madeni ya pesa ulizotumia sikukuu. Kuanzia hapa sasa ndiyo ile mwanaume atakula kwa jasho lake inaanza kuonekana kwa picha kubwa.

Kwa hiyo muhimu ni kabla hujaanza kula sikukuu za Desemba hebu jaribu kuipata picha kubwa ya kinachofuata Januari.

Mwezi wa Bebi nikwambie kitu.

Bachela mwezi huu ukipokea meseji ya ‘Baby nikwambie kitu’ usiijibu kwa sababu kifuatacho baada ya hapo itabidi uzame mfukoni ununue wigi jipya.

Advertisement