TUONGEE KIUME: Mahari ni mabaki ya utumwa yaliyopewa jina zuri

Moja ya vitu vinavyonikwaza linapokuja suala la ndoa ni mahari. Ni kama nywele za kichwa, zipo hapo siku zote lakini zipo kwa ajili ya kazi gani hujui.

Mahari ipo miaka nenda rudi kama mila au desturi, huku idadi kubwa ya watu wanaoitekeleza wakiitafsiri kama pesa au kitu ambacho hutolewa na mwanaume kama malipo kwa familia ya mwanamke pindi anapotaka kumuoa.

Lakini kimantiki, vitu pekee vinavyolipiwa chini ya jua ni bidhaa na huduma. Tunalipia sabuni ya kuogea na dawa za meno dukani, tunalipia mafuta ya kupikia na sukari kwa mangi hizo ni bidhaa.

Wakati tukienda hospitali tunalipia matibabu, kwenye basi tunalipia nauli, huku Tanzania na Algeria zikicheza kwenye Afcon tunalipia ili kuingia uwanjani kutazama mechi, hizo ni huduma.

Sasa tukirudi kwenye mahari, kwa nini tunailipa familia ya mwanamke ili kumuoa binti yao? Je, ni kwa sababu mwanamke ni bidhaa au ni huduma? Kama sio ni kwa nini tunalipa ili kuoa?

Kuna baadhi ya watu wanajenga hoja kwa kusema kuwa unalipa kama zawadi kwa familia ya mwanamke kwa kumtunza binti kipindi chote hicho sawa ni kitu kizuri, lakini kwa upande wa pili, hata mwanaume ana wazazi, alitunzwa kipindi chote na familia yake, itakuwaje kama familia ya mwanamke nayo ikitoa zawadi ya pesa nyingi au ng’ombe kwa familia ya mume, haitapendeza?

Lengo hapa si kwamba na wanaume pia wawe wanatolewa mahari, lengo ni kujaribu kuona mahari ipo hapo siku zote kwa ajili gani? Kama ipo kwa sababu zisizokuwa na msingi, kwa nini iendelee kuwepo? Yaani kwa nini tusiitoe kama ina sababu zisizoeleweka. Au kama tunaipenda sana, basi familia ya mwanaume itoe kwa mwanamke na familia ya mwanamke ifanye kinyume chake, itoe kwa mwanaume pia.

Kuna watu watabeza tunachokizungumza hapa, kwamba wanaume siku hizi wamekuaje? Wanadai kulipiwa mahari pia. Lakini kama watatokea watakaobeza hivyo, wajiulize kwa nini wanabeza mwanaume kulipiwa mahari, watagundua kuwa kumbe hii kitu mahari ina kawaida ya kumshusha mtu anayelipiwa, anaonekana mdogo, anaonekana hana nguvu, anaonekana hajiwezi, anaonekana ni bidhaa, anaonekana ni mtoa huduma tu jambo ambalo kiukweli halistahili kuwemo ndani ya ndoa.

Kwa mtazamo wangu, mahari kwenye ndoa ni kama kipande cha utumwa kilichobaki, na kikapewa jina lingine zuri zuri ili kuufanya utumwa kuwa halali.

Natamani siku moja nione wanaharakati wanaotetea haki za wanawake, waamke na hii ya kupinga mahari kwa mwanamke pindi anapoolewa kwa sababu inamshusha thamani mwanamke.