USHAURI WA DAKTARI: Dawa za kilimo, rangi zinaweza kusababisha ugumba kwa wanaume

Zipo sababu zinazochangia ugumba kwa wanaume kama matatizo ya kuzaliwa au ya kupata ukubwani. Matatizo yafuatayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara kama chanzo cha ugumba kwa wanaume.

Utengenezwaji wa mbegu dhaifu

Yako mambo yanayosababisha utengenezaji wa mbegu zisizo na ubora zinazokosa ufanisi wa kazi yake, mambo hayo ikiwamo kuzaliwa na korodani ambazo hazijashuka kutoka tumboni.

Kwa kawaida kabla kuzaliwa kokwa za kiume huwa zipo ndani ya pango la tumbo, hutakiwa zishuke kuelekea sehemu za uzazi baada ya kuzaliwa, kushindwa kushuka na kuhifadhiwa katika korodani husababisha mbegu au kokwa kuharibika kutokana na joto kali la tumboni. Kushuka na kuning’ia korodani ni maumbile sahihi ya kibailojia yenye tija kiafya ambayo huwezesha kupata joto la wastani, hivyo kutengenezwa mbegu zenye kiwango.

Mfumo wa chembe za urithi

Mwanadamu anaweza kurithi chembe za urithi zenye maelekezo ya kimwili yasiyo ya kawaida hivyo kujikuta akizalisha mbegu zisizo na ubora.

Maambukizi ya virusi hatari ikiwamo virusi vya mumps na maambukizi sugu ya magonjwa maeneo ya uzazi.

Ajali za bahati mbaya zinazotokea wakati wa upasuaji wa kurekebisha matatizo ya kiafya ikiwamo katika korodani au ngiri (hernia) na aina ya kizamani ya upasuaji wa tezi dume.

Kuwahi kuasiliwa na kufungwa kitanzi katika mrija kama njia za uzazi wa mpango.

Kuongezeka ukubwa wa mishipa inayorudisha damu mwilini kutoka katika kende/kokwa huweza kusababisha damu kwenda kwa kasi eneo hilo na kuongeza joto hivyo kuathiri ufanisi wa utengenezaji wa mbegu hizo, ikiwamo wingi wake na maumbile.

Vizuizi utolewaji mbegu za kiume

Matatizo ya kujamiiana, kama wanaume kuwa na tatizo la kutoa mbegu haraka isivyo kawaida wakati wa tendo, tatizo la mbegu kuchepukia katika kibofu cha mkojo badala ya kupitia katika mrija wa mkojo.

Matatizo ya kimaumbile, ikiwamo uwepo wa vizuizi katika kokwa, mirija na inayobeba mbegu. Kuugua magonjwa ya zinaa mpaka kufikia madhara ya kuharibu mfumo mzima wa utengenezwaji mbegu za kiume.

Kemikali, sumu mbalimbali

Zipo baadhi ya kemikali ambazo kama mwanaume zitamwingia mwilini au kukaa katika maeneo yenye kemikali hizo kwa muda mrefu huweza kumsababishia ugumba. Kemikali hizo ni kama dawa za kilimo, rangi, mipira, mionzi na dawa za steriods

Unywaji pombe kupindukia ni tatizo linaloongezeka. Hii ni kutokana na maendeleo ya kichumi. Watu wengi hujiingiza katika aina hii wakiiona kuwa ni starehe. Matumizi ya dawa za kulevya kama cocaine, bangi, hashishi, mihadarati hupunguza idadi na kiwango cha manii. Matumizi ya baadhi ya dawa za matibabu kama cimetidine, spironolactone na Nitrofurantoin.

Madhara ya saratani na matibabu yake ambayo huhusisha mionzi na kemikali tiba za saratani nazo zinaweza kuathiri utengenezwaji wa mbegu za kiume. Uondolewaji wa kokwa za kiume baada ya kupata saratani au uvimbe. Kupata ajali maeneo ya uzazi.

Kukaa sehemu zenye joto kali muda mrefu ikiwamo wafanyakazi wa viwanda vya makaa ya mawe, kiwanda cha kuoka mikate, waendesha magari ya mizigo maeneo ya jangwani.

Kutumia dawa za vichocheo vya mwilini ama kukosekana kwa baadhi ya vichocheo mwilini na kuwa na msongo wa mawazo uliopitiliza.