Breaking News

Kilimo cha Pareto kilivyompa utajiri Wema

Saturday July 13 2019

 

By Jacob Qorro, Mwananchi

Kijijini kwake Bashanet katikia jamii jamii ya Kiiraqw ambayo inatumia zaidi majina ya asili, anajulikana kwa jina la Hando Wema.

Hata hivyo, jina la ubatizo wanamwita Emanuel Wema. Huyu ndiye mkulima pekee mkubwa wa zao la pareto nchini.

Japo Bashanet au Manyara siyo eneo linalozalisha kwa wingi pareto nchini kama ilivyo katika mikoa ya Mbeya na Iringa, lakini Bashanet anapatikana mzalishaji wa pareto bora zaidi nchini kama si duniani.

Mafanikio yake ni ya kuigwa kwani yanajulikana kwa kila mkazi wa kitongoji chake cha Mandagew. Uchapakazi wake unamtambulisha kwa kila mtu na kwake sio ajabu kumuona akifanya kazi hadi usiku huku wakati mwingine akishindwa kula chakula cha mchana.

Mapato ya kilimo cha mahindi na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na unenepeshaji wa madume, ndiyo yaliyomwezesha kujipanua kabla hajaanza kilimo cha pareto.

Anayo nyumba ya wageni ya vyumba kumi na nyingine mpya na ya kisasa iliyofunguliwa na Mwenge wa Uhuru tarehe 28 Agosti 2014. Ina vyumba vinane vya “self contained” na kumbi mbili za kupumzikia au mikutano ikiwa na ulinzi mkali na mahali pazuri pa kuegeshea au kuhifadhi magari. Hayo yote ni matunda ya kilimo. Nani kasema jembe linamtupa mkulima?

Advertisement

“Licha ya kuipatia Serikali fedha za kigeni pareto kwa mkulima ni zao lenye fedha ya haraka na ya uhakika, kwani hata hali ya hewa ikiwa mbaya au nzuri utavuna tu na hutaacha kutekeleza mipango uliyojiwekea labda tu kasi ya utekelezaji ipunguke,’’ anasema na kuongeza:

‘’Ni fedha za ya haraka kwa kuwa kwa pareto ya ekari moja ifikapo Agosti unapanda vitalu vinne vya mita mbili kwa kumi kila moja na kumwagilia kwa miezi minne. Novemba unapandikiza na mwezi Machi mwakani unaanza kuvuna na kupata Sh 70,000 kwa mwezi na mwezi Mei unapata sh 150,000 kwa mwezi hadi mwezi wa tisa unapopata sh 250,000 kila mwezi kwa miaka mitatu mfululizo”.

Anasema pareto ni zao la kumuinua maskini hata mtoto mdogo. Haitaki malighafi kama mbolea za viwandani na hata ya mifugo inatakiwa kidogo tena kama ni lazima sana. Haitaki kabisa viatilifu kama viua wadudu wala busta wala madawa ya ukungu.

Kazi pekee kubwa kwenye pareto ni kupandikiza, ambayo ni kazi ya mara moja katika miaka mitatu, halafu palizi ya kila mara na kwa mbolea kidogo.

‘’ Pareto huvunwa kila wiki yaani unaweza kuingiza fedha kila siku na kuuzwa kila baada ya wiki mbili,” anasema.

Wanavyomzungumzia

Ofisa kilimo wa Kata ya Bashanet Zahoro Madongo anasema Wema anafuata hatua zote muhimu za kitaalam hasa palizi na uvunaji wa wakati ndio maana amekuwa na mafanikio ya kupigiwa mfano.

‘’Juhudi zake zimeinua hadhi ya pareto ya Bashanet na Tanzania kwani Bashanet inaongoza nchini kuwa na pareto yenye sumu kali,’’ anasema na kuongeza:

Wema huchanganya utaalamu na uzoefu wake. Pia hutafuta njia ya kuboresha pareto wakati akiona maelekezo ya kitaalamu hayatoi matokeo mazuri katika eneo husika. Si mtu wa kulaumu kwamba utaalamu hauna kazi na hakati tamaa.”

Kilimo cha pareto

Pareto ni zao lenye kichaka kifupi hadi magotini kinachotoa maua meupe yanayochumwa yanapochanua vizuri.Maua hayo hukaushwa mara baada tu ya kuyachuma ili kuhifadhi sumu. Maua hayo husagwa kiwandani ili kupata sumu ya ‘pyrethrin’.

Zao hilo huota kila mahali lakini hutoa sumu zaidi ikioteshwa katika maeneo yenye mwinuko wa mita 1500 hadi 3000 kutoka usawa wa bahari na maeneo baridi. Bashanet iko mita 2080 hadi 2090 toka usawa huo.

Sumu ya pareto yaani pyrethrin huwa nyingi kwenye maua yaliyotunzwa vizuri kwa kuoteshwa kwenye hali ya hewa nzuri, udongo mzuri usio na mbolea nyingi, kuvunwa kwa wakati, kukaushwa vizuri na kuchakatwa mapema.

Sumu ya pareto hutumika katika kilimo cha mazao ili kuua wadudu waharibifu na haiharibu mazingira kwani haidumu hewani kwa muda mwingi wala kuganda kwenye mimea husika wala kubadilisha rangi ya mimea na haidhuru sana watu na wanyama wenye damu baridi.

Lima kwa tija

Unawezaje kupata mafanikio katika kilimo cha pareto kama ilivyo kwa mkulima huyu? Wakala wa kampuni ya Pareto Tanzania (PCP) mkoa wa Manyara, Christopher Bocha anasema;

“ Ili kuzalisha pareto nyingi na bora kwa eneo tunahakikisha kuwa mashamba hayana magugu, eneo halituamanishi maji yanayoozesha mizizi na kuua mazao,maua yanachumwa kwa wakati na kukaushwa kwa haraka mara tu yanapovunwa. Anasema maua hayo yanakaushwa juani kati ya siku sita hadi 12 au kwa moshi kwenye kiwanda kidogo kwa nusu saa.

Pamoja na mafanikio ya Wema na hata wakulima wengine wa Bashanet, Serikali haina budi kuwahakikishia wakulima hao soko la uhakika na zuri, kwani kwa mara zaidi ya tano kati ya 1957 na sasa, soko la pareto limeyumba na kuwaacha wakulima na sumu hiyo nyumbani au mashambani bila msaada

Advertisement