TULONGE KILIMO : Usikurupuke kulima, jipange

Saturday March 30 2019

 

By Asna Kaniki

Ule utamaduni wa Watanzania kupenda kuigana kwenye masuala ya biashara, sasa unaonekana kuingia hata katika kilimo.
Mitaani imezoeleka, mtu akifungua duka, mwingine nyumba ya jirani atafungua duka tena linalouza bidhaa zilezile na kwa mfumo uleule wa uendeshaji.
 Kibaya zaidi maduka haya yanafunguliwa hata katika maeneo yenye wateja wa kutafuta.
Hata katika kilimo, hivi sasa uzoefu wangu unaonyesha baadhi ya watu sio kama wanalima kwa sababu wana mapenzi, dhamira na shauku ya kilimo. La hasha!
Wanafanya hivyo  kwa sababu ya kufuata mkumbo au kuiga wengine. Jirani analima, rafiki kazini ana shamba, jamaa zake katika kundi la Whatsapp wanazungumzia kilimo; kwa namna hii mtu hata pasipo kujiandaa  naye anataka kulima.
Hawa ndio wakulima ambao kilimo kikiwakataa msimu mmoja wanaanza kukiponda na mwishowe kuachana nacho.
Mkulima mwenye dhamira, mapenzi na aliyejipanga vilivyo, kamwe hawezi kuacha kulima kwa sababu ya kufanya vibaya katika msimu mmoja au katika aina fulani ya zao.
Hasara kwake huwa ni chachu ya kusonga mbele zaidi. Hasara itamkalisha chini atafakari wapi alikosea ili ajipange upya, lakini sio kukikimbia kilimo.
Niwape usia wasomaji; unaweza kuvutiwa na  mwenzako anayelima, unaweza kuhamasika na habari kuhusu kilimo mitandaoni.
Hata hivyo, kilimo sio hamasa pekee, kilimo sio kutamani pekee. Vitu hivi lazima viwe na msukumo wa  mapenzi, shauku, elimu ya kilimo na kisha kujipanga kwa hali na mali.
Usilime kwa sababu fulani analima na umesikia amepata kiasi kikubwa cha fedha. Kilimo kinahitaji ujitoe, ujifunze  masuala ya msingi kama vile menejimenti ya shamba, mbinu za kilimo, masoko na mambo mengineyo ambayo wengi wanayakosa na mwishowe kukimbilia kusema kilimo hakilipi.
Kilimo hakilipi kwa wewe uliyekurupuka, wewe usiye na subira unayedhani kilimo ni kupanda leo mbegu na kesho unavuna tena kama unavyotarajia. Kilimo kinalipa kwa anayekipenda, aliye tayari kukabiliana na changamoto na aliye tayari kuutoboa mfuko wake.

Advertisement