Mitandao ya kijamii ilivyoshika uhai wa vyama vya siasa

Ni dhahiri siasa za majukwaani kwa miaka minne iliyopita zilikuwa na changamoto kubwa lakini mitandao ya kijamii imeonekana msaada mkubwa katika kukuza uhai wa vyama vya siasa au mwanasiasa mmojammoja.

Zimekuwapo juhudi za kuwashawishi watumiaji wa mitandao ili kupata wafuasi miongoni mwao, na kunasa sehemu ya watu bilioni 2.45 wanaotumia Facebook duniani, WhatsApp (bilioni 1.6), Instagram (bilioni 1) na Twitter (milioni 330) kwa mujibu wa tovuti ya ukusanyaji wa takwimu za mitandao ya kijamii (Statista Aprili 2019).

Vyama vya siasa ni sehemu ya watumiaji hao wa mitandao nchini, ambao wananyang’anyana watu milioni 23 wanaotumia intaneti nchini, sawa na takriban asilimia 42 ya Watanzania milioni 54.2 nchini.

Vyama vitano vya siasa kati ya 19 vilivyosajiliwa nchini vimeonekana kuwa vinara wa watumiaji wa kurasa za mitandaoni kwa ajili ya kuongeza ushawishi wake, kupanua mtandao, kutangaza sera pamoja au kuelezea utekelezaji wa Ilani yake.

CCM inaonekana kuongoza kwa idadi ya wafuasi wanaoifuatilia mtandaoni, ikifuatiwa na Chadema, ACT-Wazalendo, CUF na NCCR-Mageuzi. Akaunti za vyama vingine hazikuonekana.

Lakini wachambuzi wa siasa wanasema licha ya CCM kuwa na wafuasi wengi, wafuasi wa upinzani wameonekana kuwa na nguvu kupitia hoja zao zinazoishambulia CCM kwa kila jambo linalojitokeza serikalini na ndani ya chama chenyewe.

“CCM inashambuliwa kwa sababu kila dosari ya Serikali inatajwa CCM, kwa hiyo hata watu wasiokuwa na vyama mitandaoni wanajikuta wanaishambulia CCM,” anasema Abdulfatah Lyeme, ambaye ni kada wa CCM Segerea.

Pamoja na hayo, Kanali Ngemela Lubinga, katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM anasema chama hicho kinatambua umuhimu wa mitandao ya kijamii katika ukusanyaji wa wafuasi.

“Mitandao si utaratibu rasmi kwa chama, lakini inaongeza wafuasi. Haiepukiki kwa sababu sisi hatuishi hewani, tuko katika dunia inayotumia mitandao hiyo. Kwa hiyo CCM inajifunza lakini haifanyi kazi mitandaoni. Hatujibu hoja za mitandaoni ila kila mwanaCCM anayo haki ya kutetea chama mitandaoni.”

Wafuasi mitandaoni

Takwimu za wafuasi wa vyama kati ya mwaka 2015 hadi 2020, zimeonyesha idadi kubwa ya wafuasi katika baadhi ya vyama huku vingine vikiwa chini kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kushindwa kutangaza kurasa zake, na baadhi ya wafuasi kujikuta wanafuatilia kurasa binafsi za makundi yenye nasaba na chama au za kiongozi mmojammoja. Uchambuzi haujagusia mtandao wa YouTube.

Katika mtandao wa Twitter chama cha ACT Wazalendo kimejikusanyia wafuasi zaidi ya 158,600, Chadema zaidi ya 241,100 huku CUF Habari ikipata wafuasi 296 tangu ilipoifungulia siku chache zilizopita mwaka huu, huku CCM iliyowahi kuingia katika majukwaa hayo mwaka 2011, iliongoza kwa wafuasi 371,000.

Katika mtandao wa Instagramu, ACT Wazalendo ina wafuasi 34,000, CCM wafuasi 199,000, Chadema 16,900 na CUF habari 707.

Katika Facebook, ACT-Wazalendo ina wafuasi 1,763, CCM 224,000, CUF Habari 153 na Chadema 117,431.

Chama cha NCCR-Mageuzi kina wafuasi 1,300 katika ukurasa wake wa Facebook wakati na 82 wa twitter tangu zilipoanzishwa Juni 2016. Kwa mara ya mwisho chama hicho kiliandika tangazo kwa umma Februari mwaka 2018.

Hata hivyo, wachambuzi wanasema takwimu hizo hazina maana kuwa wingi wa watu wanaofuatilia kurasa hizo mtandaoni ndiyo wanaokipenda chama husika kutokana na tabia za watumiaji wa mitandao.

Ukiachana na akaunti za vyama hivyo na nyingine za viongozi au mwanachama mmojammoja, kuna majukwaa mengi yaliyoanzishwa na wafuasi kwa mapenzi yao binafsi kwa kutumia majina ya vyama na yanayoweka maudhui yanayokisaidia chama husika.

Mkurugenzi wa Mawasiliano CUF, Maulid Kambaya anasema licha ya chama hicho kuwa na wafuasi wachache mitandaoni ndani ya mwaka mmoja baada ya kuingia kwenye siasa za majukwaa hayo, tayari mafanikio yameanza kuonekana.

“Tunayo idara maalumu ya maudhui ya mitandaoni na tumeweka utaratibu wa kuweka posti nne kila ukurasa. Kazi ya kujenga uhai wa chama inaendelea huko na tayari tumepata mrejesho mkubwa baada ya kuzindua sera nne za chama; elimu, afya, kilimo na ajira. Tumepokea maoni mengi,” anasema.

Lavern Masika, mhitimu wa Shahada ya Habari na Mawasiliano kwa Umma kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini, anasema vyama vya siasa vinatakiwa kutambua tofauti ya tabia za wafuasi katika kila jukwaa na kubuni mbinu mahususi za kufikisha maudhui yanayowalenga ili kuongeza ushawishi.

“Uzoefu unaonyesha mtandao wa Instagram una vijana sana, unataka vitu laini, Twitter ina watu wenye upeo zaidi, Facebook ina watu wa kawaida na inahusisha watu wengi zaidi, kwa hiyo ni muhimu kuangalia tabia na kutengeneza maudhui katika mfumo unaoendana,” anasema Masika.

Mbali na kurasa hizo, majukwaa ya mtandao wa WhatsApp yamekuwa ni mfano wa mikutano huru ya kisiasa inayoibua, kujadili hoja na kutangaza mafanikio na changamoto za serikali, vyama vya siasa na wanasiasa mmojammoja.

Ushiriki na ushindani

Kupitia mitandao hiyo kumekuwa na ushindani wa wazi wa kisiasa wenye kuibua hoja nyingi na kuvutia watu wengi.

Kwa mfano, misuguano ya bungeni kati ya kiti cha Spika na upinzani kuhusu masuala mbalimbali kama sakata la Tundu Lissu na kauli ya Profesa Musa Assad, mdhibiti na Mkaguzi Mkuu mstaafu wa Hesabu za Serikali (CAG) wa zamani kuhusu bunge dhaifu na waraka wa makatibu wakuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana.

Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu anasema licha ya kuchelewa kuingia katika majukwaa hayo, mafanikio yameanza kuonekana. Anasema ACT ilianzisha dawati la siasa mitandaoni baada ya zuio la mikutano na kubanwa kwa vyombo vya habari.

“ACT ni chama kichanga ndiyo maana kina idadi ndogo ya wafuasi lakini tathmini inaonyesha mafanikio. Kwa mfano ruzuku yetu ya Sh4.2 milioni haiwezi kukuza uhai wa chama kwa hiyo harambee mitandaoni kila tunapoanzisha kampeni, hukusanya kati ya Sh30 milioni hadi Sh40 milioni,” anasema

Katibu wa mambo ya nje wa NCCR-Mageuzi, Nderakindo Kessy anasema licha ya kutosikika zaidi mitandaoni, uongozi wa chama hicho umeamua kufanya siasa za kukiimarisha bila kuathiriwa, kama ilivyotokea kwa viongozi wa vyama vingine.

Lakini, Tumaini Makene, mkuu wa Idara ya Habari ya Chadema anasema ingawa mitandao hiyo haiwezi kuwa mbadala wa mikutano ya hadhara, lakini imewasaidia kwa kiwango kikubwa kuwafikia watu wengi.

Anatoa mfano wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho ambao walikwama kuurusha moja kwa moja kupitia vyombo vya habari, kuwa kupitia mitandao walikuwa wanaweza kupata watu hata 100,000 wanaofuatilia.

“Mtandaoni, kama YouTube au Facebook ukiweka kitu hakitoki, hata wale walioshindwa kufuatilia moja kwa moja, wanaweza kufuatilia kwa wakati wao,” alisema.

Makene pia amezungumzia kuwapo umuhimu wa kuzitangaza kurasa hizo ili zifahamike na kupata wafuasi wengine zaidi