Nyalandu atauweza mfupa ‘uliomshinda fisi’ dodoma?

Wednesday January 22 2020

 

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Uchaguzi ndani ya chama kikuu cha upinzani nchini cha Chadema umemalizika hivi karibuni huku mbunge wa zamani wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu akichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kanda ya Kati ya kichama inayojumuisha mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida.

Baada ya kunyakua wadhifa huo, Nyalandu ametaja vipaumbele kadhaa vya utekelezaji, ikiwamo kushinda uchaguzi katika Jimbo la Dodoma Mjini na majimbo mengine ya mkoani humo katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.

Majimbo ya uchaguzi yaliyopo katika Mkoa wa Dodoma ni Bahi, Chemba, Kondoa, Chilonwaa, Mpwapwa, Kibakwe, Kongwa na Mtera ambayo tangu mfumo wa vyama vingi uingie nchini mwaka 1992 hayajawahi kuongozwa na mbunge kutoka vyama vya upinzani.

Swali la kujiuliza ni je, Nyalandu na timu yake mpya ya uongozi wataweza kuvunja rekodi hiyo kwa kupata kiti cha ubunge?

Akijibu swali hilo, Nyalandu anasema anayo mikakati ya siri na isiyo ya siri itakayofanikisha hilo kwa kuiwa ndicho kipaumbele namna moja.

“Kipaumbele namba moja cha Chadema Kanda ya Kati kitakuwa ni kuhakikisha mwaka 2020 ni tunashinda na kuliongoza Jiji la Dodoma ambalo ni makao makuu ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania,” anasema.

Advertisement

“... Kwa kwa wale wanaotazama ushindi wa majiji yanayoongozwa na Chadema kwa jicho la husuda kwanza wajiandae kwa sababu tunakwenda kushinda Jiji la Dodoma,” anasema Nyalandu.

Anasema wanalishinda jiji hilo kwa mbinu zitakazojulikana na zisizojulikana huku akiwaomba viongozi wa Chadema katika kanda hiyo kusimama kidete ili kuhakikisha wanatimiza lengo lao.

Bila kutaja idadi ya wanachama wa Chadema katika jimbo la Dodoma wala Kanda nzima ya kati, Mwenyekiti huyo anasema wanao wanachama wengi kuliko chama kingine chochote cha siasa jijini hapa.

Anasema pia kwamba viongozi wengi wa Serikali walihamia Dodoma ni wanachama chama hicho.

Anasema ushindi huo utaipa raha Chadema na anauhakikishia umma kuwa chama hicho kitakuwa ni cha uwazi, dhabiti na kitawatendea watu wote sawa.

“Na pia tutahakikisha tunashinda majimbo mengine yaliyoko Singida na Morogoro,” anasema.

Anaulizwa uhakika wa kushinda majimbo yote, anasema unapokwenda kushindana ni lazima kupanga kushinda majimbo yote na ikitokea maeneo mengine umenyang’anywa hiyo ni sehemu ya ushindani.

“Azma yetu ni kwenda kata kwa kata, jimbo kwa jimbo na wilaya ili kuhakikisha tunawaweka wanachama wa kutosha kwenye uchaguzi.

“Chadema Kanda ya Kati tunadai na tunasisitiza kwa wote wenye mamlaka kuhakikisha kuwa Tume ya Uchaguzi inakuwa huru. Kuna msisitizo kuwa (serikali) imefanya mambo mengi na mazuri, kama umefanya unaogopa nini? Twende kwenye ulingo wa kisiasa tukiwa na Tume Huru ya Uchaguzi,” anasema.

Anasema uwepo wa Tume huru utaipa Tanzania heshima si tu kwa Afrika Mashariki lakini katika ukanda wa nchi za Kusini mwa Afrika na katika ukanda mzima wa Afrika.

“Tujivunie kutengeneza mifumo ambayo itaishi maisha… Tume Huru ya Uchaguzi itaisaidia sana CCM itakapokuwa chama cha upinzani. Tume Huru ya Uchaguzi itawasaidia wanachama wa CCM waondoke kifua wazi wakiamini kazi ya mwanasiasa ni kushawishi,” anasema.

Hata hivyo, anasema ili washinde wanaomba na kusisitiza mchakato unaoendelea wa kurekebisha daftari la wapiga kura ufanyike kwa weledi kila eneo.

“Mahali penye wanachama wa Chadema au vyama vingine kusitokee ufundi wa kukwepa yale maeneo kwamba hapa kuna wanachama wengi. Wale ambao wako kwenye Tume tunawasihi wafanye kazi kwao kwa weledi, daftari lirekebishwe kabla ya uchaguzi,” anasema.

Lakini wengine kauli ya Nyalandu inaonekana nyepesi isiyo na uzito wowote, akama anavyosema Anthony Mavunde, mbunge wa Dodoma Mjini (CCM) kuwa, “ni sawa na maneno ya mfa maji ambaye haachi kutapatapa. Dodoma ni ngome imara ya CCM haiwezi kuchukuliwa.”

Anasema “Nyalandu amekuwa nje ya siasa kwa muda, hivyo hajui kazi nzuri inayofanywa na CCM na Serikali yake ambayo wananchi wanasubiri wakati wa uchaguzi wairudishe ili waendelee kunufaika na matunda yake.”

Advertisement