Breaking News

KALAMU HURU: Wananchi wamehukumiwa kwa makosa ya Serikali kuzima laini za simu

Wednesday January 22 2020Elias Msuya

Elias Msuya 

Hatua ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzima laini za simu ambazo hazikusajiliwa ni kuwahukumu wananchi kwa makosa ya Serikali.

Usajili wa laini za simu ulioanza Mei 1, 2019 ulitakiwa kwisha ndani ya muda mfupi, lakini sharti la kuwa na kitambulisho cha Taifa ndiyo limeleta nongwa.

Tangu awali ilishaonekana kuwa kasi ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) haiendani na muda uliowekwa wa kusajili laini za simu.

Ndiyo maana hata Rais Magufuli alipokuwa akizungumza jijini Mbeya Aprili 26, 2019 aliiagiza TCRA kuongeza muda hadi Desemba 31, 2019 kwa sababu ya changamoto ya upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa.

Alisema wazi kuwa “kama vitambulisho vya Taifa havijatolewa kwa Watanzania wote, ile tamko kwamba mtu mwenye simu lazima asajiliwe kwa kitambulisho cha Taifa, haiwezekani. Hicho ni kitu ambacho hakiwezekani.”

Mbali na Rais Magufuli, Novemba 13, 2019, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alitoa kauli bungeni Dodoma akiwaondolea wasiwasi Watanzania kwamba licha ya tarehe ya mwisho kuwa Desemba 31, hakuna Mtanzania ambaye simu yake itazimwa.

Advertisement

Pamoja na kuondolewa wasiwasi huo, bado utoaji wa vitambulisho vya Taifa uliendelea kusuasua tu. Ilipokaribia kwisha mwaka 2019, Rais Magufuli akaongeza tena siku 20 yaani hadi Januari 20, 2020 ili kukamilisha usajili huo.

Bado nyongeza ya muda huo haijatosha kuwasajili Watanzania kwa sababu hiyo ya vitambulisho vya Taifa.

Lakini kwa kuwa muda wa mwisho wa usajili ulishawekwa, TCRA ndiyo wameshaanza kuzima laini za simu ambazo hazijasajiliwa. Hapo kosa ni la nani?

Baadhi ya viongozi wamefikia kuwalaumu wananchi waliochelewa kusajiliwa, wakisema walikalia umbea, lakini wangejiandikishaje bila vitambulisho vya Taifa?

Je, huu ni wakati wa kuwalaumu wananchi kwa kutosajili laini zao? Au ilaumiwe Nida kwa kuchelewesha vitambulisho vya Taifa? Au TCRA kwa kuzima laini akijua vitambulisho hakuna?

Hapa wa kulaumiwa ni Serikali yenyewe kwa sababu Nida na TCRA ni mamlaka za Serikali zinazopaswa kuratibiwa ili zisiwaumize wananchi.

Tunakumbuka mwaka 2016, Nida ilisitisha mikataba ya kazi ya wafanyakazi 597, kwa maana nyingine walifukuzwa kazi kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kubana matumizi.

Suala la upungufu wa watumishi lilielezwa hata na Naibu Waziri Mambo ya Ndani, Hamad Masauni alipotembelea kituo cha kuchakata taarifa za waombaji nchi nzima kilichopo Kibaha, Pwani Januari 2, 2020 ambapo aliitaka Nida kuongeza watumishi.

Hata kama Nida ingetekeleza agizo la Masauni isingeweza kuwahi tarehe mwisho yaani Januari 20.

Ikiwa Serikali ilijua wafanyakazi hawatoshi, kwa nini ilitoa tarehe ya mwisho haitekelezeki?

Advertisement