Yaliyotokea na maswali yasiyo na majibu Serikali za mitaa

Wednesday November 27 2019

 

By Peter Saramba, Mwananchi

Tayari viongozi wa Serikali za mitaa wamepatikana kupitia uchaguzi uliofanyika Novemba 24, 2019 ambao hata hivyo ulisusiwa na vyama vikuu vya upinzani vilivyotangaza kujitoa kwa madai ya kufanyiwa hujuma wakati wa kuchukua na kurejesha fomu hadi uteuzi.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeibuka na ushindi mkubwa ambao viongozi, wanachama, wapenzi na wafuasi wa chama hicho tawala wameita wa kishindo.

Wakati nikichukua fursa hii kuipongeza CCM na wagombea wake kwa ushindi huo, pia nieleze mambo yaliyotokea katika mchakato huo ambayo yameibua maswali na hoja za kikanuni, kiutaratibu na utashi wa siasa za ushindani nchini.

Miongoni mwa mambo hayo ni msimamo wa Serikali kupitia kwa Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo na Naibu wake, Naibu wake Mwita Waitara wa kusisitiza kuendelea kuwatambua wagombea ambao vyama vyao vilitangaza kujitoa na ambao baadhi yao waliandika barua za kujitoa.

Kwa nyakati tofauti, Waziri Jafo na Naibu wake Waitara wamekaririwa wakisisitiza siyo tu kuwatambua wagombea ambao vyama vyao vimetangaza kujitoa, bali hata matumizi ya nembo na majina ya vyama hivyo.

Kuwatambua wagombea ambao vyama vilivyowadhamini vimejitoa a mujibu wa kifungu cha 19 (1) ya kanuni uchaguzi wa uenyekiti wa vitongoji sura ya 287 na kifungu cha 20 (1) ya kanuni ya uchaguzi wa mitaa na wajumbe wa kamati za mitaa sura ya 288.

Advertisement

Kanuni hizo zilizotangazwa katika gazeti la Serikali namba 271 na 272 zinatoa fursa kwa wagombea kujitoa hata baada ya uteuzi.

Vifungu hivyo vinasema, “Endapo, baada ya uteuzi kufanyika, mgombea aliyeteuliwa kugombea nafasi (uenyekiti wa mtaa/kitongoji na ujumbe wa kamati ya mtaa) atajitoa, msimamizi msaidizi wa uchaguzi atatengua uteuzi wa mgombea huyo na wagombea waliobaki watapigiwa kura ili kupata mshindi.”

Kanuni ya 14 (f) yenyewe inataja kuwa mwanachama wa chama cha siasa na kupata udhamini wa chama husika kuwa miongoni mwa masharti na sifa ya kuwa mgombea.

Kanuni hiyo inasema mkazi yeyote anaweza kugombea uenyekiti wa kitongoji/mtaa au ujumbe wa kamati ya mtaa endapo “Ni mwanachama wa chama cha siasa na amedhaminiwa na chama hicho,”

Kwa vifungu hivyo, Waziri na naibu wake kusisitiza kuwatambua wagombea waliojitoa au ambao vyama vyao vimejitoa vinasimamia kanuni ipi?

Hoja nyingine ni madai ya baadhi ya wagombea walioenguliwa kudaiwa kujiandikisha zaidi ya mara moja kinyume cha sheria na kanuni za uchaguzi.

Kwa mujibu wa kanuni ya 45 (1) (c) ya uchaguzi wa uenyekiti wa vitongoji sura ya 287 na kanuni ya 47(1) (c) ya uchaguzi wa mitaa na wajumbe wa kamati za mitaa sura ya 288, kujiandikisha mara mbili siyo tu inastahili adhabu ya kuenguliwa kugombea na kupiga kura, bali pia ni kosa la jinai.

Kwa pamoja, kanuni hizo zinasema “Mtu yeyote atakuwa ametenda kosa la uchaguzi endapo atajiandikisha au kupiga kura zaidi ya mara moja kwa wagombea wa nafasi moja,”

Adhabu kwa mtu anayetiwa hatiani kwa kosa la kujiandikisha au kupiga kura mara mbili ni faini isiyozidi Sh300, 000 au kifungo cha kisichozidi mwaka mmoja au adhabu zote mbili kwa pamoja.

“Mtu yeyote atakayepatikana na hatia kwa kosa lolote chini ya kanuni ndogo ya (1) atahukumiwa adhabu ya faini isiyozidi shilingi laki tatu au kifungo kisichozidi miezi kumi na miwili au vyote kwa pamoja, yaani faini na kifungo,” kinasema kifungu cha 45 (2) cha kanuni za uchaguzi

Adhabu kwa kosa lolote kinyume cha kanuni za uchaguzi pia inatajwa katika kifungu cha 47 (1) (k).

Uwepo wa vifungu vinavyoeleza kosa na kutaja adhabu kwa anayetiwa hatiani kunaibua swali la kwa nini hadi mchakato wa uchaguzi unakamilika, walioenguliwa kwa madai ya kujiandikisha zaidi ya mara moja hawajachukuliwa hatua za kisheria?

Kuachwa huko ni kwa hisani au huruma ya mamlaka zinazosimamia uchaguzi na utekelezaji wa sheria na kanuni au ni uthibitisho kuwa huenda kuenguliwa kwao kulifanyika figisu kama vyama vilivyojitoa vilivyodai?

Vyovyote iwavyo; na bila kujali makundi yetu ya kimaslahi kijamii na kisiasa, tutambue kuwa haki kwa wote hujenga Taifa na kutenda tofauti ni kinyume chake.

Sote kwa umoja wetu bila kujali makundi yetu ya kimaslahi tutambue kwamba hatuna Taifa lingine zaidi ya Tanzania; na vyote tunavyofanya iwe kwa makusudi au bahati mbaya vinatuathiri sasa na vizazi vyetu.

Mungu ibariki Tanzania! [email protected], +255 766 434 354.

Advertisement