Atiki: Safari ya mafanikio kikapu ilianzia Mnazi Mmoja

Hakuna aijuaye kesho yake. Ndivyo imekuwa kwa mchezaji wa kati wa timu ya Taifa ya kikapu, Atiki Ally Atiki.

Mchezaji huyo hakuwahi kufikiria kama ipo siku ataishi nchini Canada, lakini mpira wa kikapu umebadili mwelekeo wa maisha yake na kumfikisha nchini humo.

Atiki anaeleza namna alivyoanza kujifunza kikapu, lakini awali hakuwa na ndoto kuwa mchezo huo utampa fursa ambayo anaipata kwa sasa.

“Nilicheza kwa kujifurahisha tu kama michezo mingine, wakati ule nilikuwa mdogo na sikujua mbeleni hatima yangu itakuwa nini,” anasema.

Atiki ambaye amebakiza hatua chache kunyemelea nafasi ya kucheza kwenye Ligi ya Kikapu nchini Marekani (NBA), anasema hakuwa akifahamu umuhimu wa mchezo huo na namna ambavyo ungekuja kubadili maisha yake.

“Nilikuwa Shule ya Msingi Nyanza (iliyopo Mwanza), pale shuleni hakukuwa na vifaa vya kutosha kwa ajili ya mchezo huo, lakini tulicheza kibishi wakati wa mapumziko (ya masomo), niliingia kwenye kikapu kutokana na umbo langu (kubwa).”

Anasema siku moja katika harakati zake za kucheza ndipo alipokutana na kocha maarufu wa mchezo huo, Bahati Mgunda, ambaye ni mchezaji nyota wa zamani wa mpira wa kikapu, na hapo ndipo safari ya mafanikio ilianzia.

“Mgunda aliniambia nataka nikupeleke Dar es Salaam kucheza huko, wakati huo nilikuwa darasa la sita,” anasema Atiki.

Anasema alijua ni maneno tu ambayo hayakuwa na ukweli, kwani kutoka Mwanza alikozaliwa na kwenda Dar es Salaam kucheza kikapu kwa umri aliokuwa nao aliona kuwa ni ndoto.

“Sikuitia safari hiyo akilini, nilijua ni utani tu wa kawaida, lakini baada ya siku kadhaa kupita kocha aliniambia nijiandae kesho tunaanza safari ya kwenda Dar es Salaam.

“Nilishtuka, sikutarajia kwani hata taarifa za safari yenyewe zilikuwa za kushtukiza kwangu, kwa kuwa nilikuwa natamani kwenda Dar es Salaam wala sikujiuliza mara mbili mbili.”

Anasema mchakato wa safari ulianza na kupewa baraka na familia yake, ambayo ilimtakia kila la heri katika maisha mapya ya jijini Dar.

Atiki ambaye alizaliwa Januari 12, 2001 anasema mchakato wa uhamisho kutoka Shule ya Msingi Nyanza ulifanikiwa na kujiunga na Shule ya Msingi Gerezani (Ilala, Dar es Salaam) ambako alisoma na kuhitimu darasa la saba. “Nilifaulu, lakini kutokana na kipaji changu nilipata ofa ya kimasomo Shule ya Sekondari Highview,” anasema.

Safari ya Canada

Safari ya Canada anakoishi kwa sasa ilianzia Mnazi Mmoja

Atiki anasema wakati anasoma alikuwa akicheza na kufanya mazoezi ya kikapu katika Kituo cha Jakaya Mrisho Kikwete Youth Park (JMKYP), Kidogo Chekundu, Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam chini ya Kocha Bahati.

“Walikuja makocha Wazungu wakifanya skauti ya wachezaji wakati ule Kocha Bahati ndiye alikuwa akiniendeleza, nilipata fursa ya kuchaguliwa katika watu ambao makocha wale waliona wana vipaji vya kuendelezwa nje ya nchi baada ya kuonyesha kiwango kwenye mashindano yaliyofanyika pale.

“Sikuamini, nilipiga magoti nikasali kumshukuru Mwenyezi Mungu, Kocha Bahati alinitia moyo sana, aliniambia naweza, nikapambane, nikipata nafasi,” anasema.

Anasema alipata ofa ya kimasomo ya elimu ya juu ya sekonsari kwenye Shule ya Thames Valley District School Board nchini Canada wakati huohuo akicheza kwenye timu ya London Basketball Academy ya nchini humo.

Tofauti na Tanzania

Atiki ambaye aliondoka nchini mwaka 2018 na kuanza maisha mapya nchini Canada, anasema tangu amewasili nchini humo amekuwa akipewa ushirikiano wa hali ya juu na wenzake pamoja na wakufunzi. “Tofauti na nilivyotarajia kuwa huenda nitapata changamoto ya kuishi huku, lakini imekuwa tofauti, tangu siku ya kwanza mpaka sasa nimekuwa nikipewa ushirikiano mkubwa. Wenzetu huku wamepiga hatua kubwa katika mchezo wa kikapu ambao ni mchezo unaofanya vizuri kimataifa.”

Anasema nchini humo kuna viwanja vya kutosha, mazingira na mifumo ya kuendeleza wachezaji iko juu kulinganisha na hapa nchini.

Matarajio baada ya kuitwa All Stars

Atiki ambaye amewahi kucheza timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 18 kabla ya kuwa kwenye Akademi ya JMK Elite Training kisha kutua kwenye klabu ya Yellow Jackets na kuichezea klabu ya mabingwa wa RBA, Vijana City Bulls, hivi karibuni alichaguliwa kwenye kikosi cha kwanza cha nyota wa mashindano ya shule na vyuo nchini Canada.

Katika nyota watano wa mashindano hayo, Mtanzania huyo alikuwa ni miongoni mwao.

“Ni Mungu tu na kujituma ndiko kumenifikisha hapa, tulikuwa wachezaji wengi, lakini makocha wameniona nastahili kuwa kwenye timu ya All Stars, hii ni hatua kubwa sana kwangu,” anasema Atiki.

Anasema kama siyo makocha wa Tanzania kumpa misingi bora katika mchezo huo, basi asingefika hapo alipo.

“Ndoto yangu ni kucheza NBA, najua ugumu wa kucheza ligi hiyo, lakini wanaocheza sasa hawana tofauti na mimi, naamini nitaweza na Watanzania waendelee kuniombea.”

Atiki ambaye anahitimu masomo ya juu ya sekondari mwakani, anahitaji kufaulu na kujiunga na chuo nchini humo na kama akionyesha kiwango bora huo utakuwa mtihani wake wa mwisho ili kusaka nafasi ya kucheza NBA. “Nasoma na kucheza kwa bidii mno, naamini ndoto yangu ya kufika NBA itatimia, huo ndiyo mkakati wangu hivi sasa,” anasema huku akiwashukuru waliofanikisha safari yake.

Kocha Bahati amzungumzia

Bahati, kocha wake wa zamani, licha ya kumtoa Atiki mjini Mwanza na kumpeleka Dar es Salaam kwa ajili ya kuendeleza kipaji chake, anakumbuka namna mchezaji huyo alivyokuwa kivutio katika shule yake ya msingi ya Nyanza wakati akiaga ili kuanza maisha mapya jijini humo. “Siyo walimu hadi wanafunzi wenzake walivutiwa na mafanikio ya Atiki, shule ilizizima wakati akiaga, wengi walitamani kufuata nyayo zake na hatua aliyofikia hajawaangusha Watanzania, ndugu zake wa Mwanza na familia yake pia,” anasema.

Bahati anasema mbali na kumlea katika mpira wa kikapu, lakini alimuwezesha mchezaji huyo kushiriki kikamilifu mafunzo maalumu ya Basketball Without Borders (BWB) ambayo yanaandaliwa na NBA na Shirikisho la Kikapu Afrika (Fiba) yaliyofanyika Afrika Kusini na yale ya Giants of Afrika ya nchini Kenya.

“Amefika hapo alipo kwa kuwa alipenda kujifunza na alikubali kukosolewa alipokosea, haikuwa kazi nyepesi kwake, lakini jitihada na nidhamu ya mchezo ndivyo vimemfikisha hapo.”

Anasema endapo atahimtimu masomo ya sekondari na kujiunga na chuo nchini humo, atapata fursa ya kucheza Ligi ya vyuo Vikuu (Division One), ambayo ni hatua ya mwisho inayowafanya wachezaji kuonwa na timu za NBA.

“Ili kucheza NBA, lazima utokee chuoni, hivyo Atiki amebakisha hatua ndogo kufika huko, cha msingi apambane ili kupata chuo kule,” anasema.