Kahata aeleza namna Kagere alivyomng’oa Gor Mahia

Tuesday July 30 2019
pic kahata

Dar es Salaam. Meddie Kagere ni jina maarufu kwasasa nchini Tanzania, likinogeshwa na ubora wake wa kufunga mabao katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita.

Kagere akiwa na msimu wake wa kwanza tu Simba akitokea Gor Mahia ya Kenya, alitwaa tuzo ya mfungaji bora baada ya kufunga mabao 23 akifuatiwa na Salim Aiyee (18) na Heritier Makambo (17).

Mashabiki wa Simba sasa wanatambia jina la Kagere, mchezaji wa kimataifa wa Rwanda mwenye asili ya Uganda.

Kagere kwasasa ndiye mfalme wa Simba badala ya aliyekuwa nyota wa kimataifa wa zamani wa timu hiyo Emmanuel Okwi aliyeachana na klabu hiyo.

Okwi alikuwa shujaa wa Simba muda wote, alitumia vyema kipaji cha kufunga mabao na haikushangaza kugeuka mfalme ndani ya klabu hiyo kongwe.

Baada ya ufalme wa Okwi, kuondoka Simba imemleta shujaa mwingine akitokea Kenya anaitwa Francis Kahata.

Advertisement

Baada ya kuhaha kwa miaka miwili, hatimaye Simba imemnasa kiungo huyo wa pembeni mwenye kasi aliyejiunga na mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara akitokea Gor Mahia.

Kahata ametua Simba kwenda kubeba ufalme wa Okwi aliyetikisa kwa kiasi kikubwa soka ya bongo kwa miaka yote aliyodumu nchini.

Haikuwa kazi rahisi kumpata Kahata na hilo anathibitisha nyota huyo mfupi alipozungumza na Mwananchi kuhusu mikakati yake ndani ya klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam.

Kahata anasema ana wajibu wa kulipa fadhila kwa Simba kutokana na kazi kubwa iliyofanya hadi kupata huduma yake akitia saini mkataba wa miaka miwili.

“Haikuwa kazi nyepesi, Simba ilianza kunitafuta miaka miwili iliyopita, lakini walishindwa, kulikuwa na mambo mengi yaliyochangia ikiwemo suala langu la mkataba,”anasema Kahata.

Winga huyo anasema baada ya kuhangaika muda mrefu, Simba ilikuja na mbinu mpya kwa kumtumia Kagere kupata saini yake jambo ambalo imefanikiwa.

“Ngoja nikwambia, siri kubwa ya kuja Simba imetokana ukaribu wangu na Kagere. Sisi ni marafiki tangu tukiwa Gor Mahia, walimtumia yeye ili kunishawishi nije hapa.

“Pamoja na ushawishi wa Kagere bado nilisita, lakini baada ya kumuhoji sana kuhusu taarifa za klabu ya Simba alinithibitishia ni sehemu salama kwangu, nikaamua kuachana na Gor Mahia ingawa nilikuwa naipenda,” anafafanua Kahata.

Anasema alifahamu mambo mengi sana kuhusu Simba na Tanzania kwa ujumla kupitia Kagere, hivyo aliamua kuondoka Kenya akiacha familia yake kuja nchini kuanza maisha mapya.

Hata hivyo, Kahata alikaririwa na vyombo vya habari Kenya akidai kuwa Gor Mahia haikuonyesha dhamira ya kumpa mkataba mpya licha ya kuonyesha nia ya kutaka kuendelea kuitumikia klabu hiyo. “Kimsingi sikuwa na mpango wa kuondoka Gor Mahia, lakini wakati mkataba wangu ukielekea ukingoni hakuna ofisa aliyekuwa kuzungumza na mimi. Niliona kuna dalili ya kutonihitaji ingawa binafsi niliiipenda sana Gor Mahia,”alikaririwa Kahata akisema.

Simba

Kahata anasema ana malengo yake ya kuhakikisha anafanya vizuri na kuwa miongoni mwa nyota wa kutegemewa katika kikosi hicho na mkakati wake ni kuacha kumbukumbu nzuri.

“Ndani ya moyo wangu nitajituma kwenye mazoezi na mechi ambazo nitapata nafasi ya kucheza, nina imani kubwa nikiweza kufanya hivyo nitaisaidia klabu kufikia malengo yake.

“Natambua naweza kukutana na Changamoto hizo changamoto hapa na nikashindwa kufikia malengo yangu kwa wakati lakini naamini yote yatawezekana,” anasema.

Ushindani

Simba imesajili wachezaji wapya zaidi ya kumi kulingana na mahitaji ya kocha Patrick Aussems ambaye ataiongoza Simba katika Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika nafasi ya winga wa kushoto na kulia ambapo Kahata anacheza wapo mastaa Ibrahim Ajibu, Deo Kanda, Miraji Athumani, Rashid Juma, na Cletous Chama.

Kahata anasema ushindani wa namba ni jambo la kawaida katika timu, lakini atapambana uwanjani kumshawishi kocha kumpa nafasi ya kucheza kwa kuwa amekuja kufanya kazi.

Kikosi

Kahata anasema mashabiki wa soka siku zote wanapenda mafanikio, hivyo watatumia maandalizi ya mechi za msimu kujiweka vyema kwa mashindano ya msimu ujao.

Rekodi

Kahata mwenye miaka 27, katika mji wa Ruiru, Kenya kabla ya kujiunga na Simba, alicheza soka timu za vijana na mwaka 2008 alitua Thika United kabla ya kutolewa kwa mkopo akitokea timu ya Ravenna. Mwaka 2010 alitimkia University of Pretoria alipocheza hadi mwaka 2014, alipojiunga na KF Tirana akicheza mechi 29 na kufunga mabao manne na 2015 alitua Gor Mahia. Kahata alianza kucheza timu ya taifa mwaka 2011 na amefunga mabao mawili katika 31 alizocheza.

Advertisement